Vatican News
Mafungo ya Kiroho Kipindi cha Kwaresima: Mapambano ya maisha ya kiroho katika sala inayomwilishwa kwenye huduma makini kwa watu wa Mungu! Mafungo ya Kiroho Kipindi cha Kwaresima: Mapambano ya maisha ya kiroho katika sala inayomwilishwa kwenye huduma makini kwa watu wa Mungu!  (Vatican Media)

Mafungo ya Kiroho: Mapambano ya kiroho katika sala na huduma!

Mafungo ya kiroho kipindi cha Kwaresima mkazo zaidi ni: Kuhusu mapambano ya maisha ya kiroho kwa kutumia silaha ya sala! Viongozi wa Kanisa wanapaswa kusimama kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwaendeleza watu wa Mungu katika maeneo yao. Kanisa katika Ulimwengu mamboleo linakabiliana na mashambulizi makali dhidi ya maisha na utume wake. Ushuhuda na huduma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafungo ya Kiroho: “Msiogope na Safari ya Jangwani” ndiyo mada kuu mbili zilizoongoza tafakari, Jumatano tarehe 4 Machi 2020 ambayo Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuifuatilia akiwa kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha, mjini Vatican. Katika ulimwengu mamboleo watu wamegubikwa na woga na wasiwasi kwa sababu wanajihisi kuwa kama mavumbi au maua ya kondeni yanayochanua asubuhi na kunyauka jioni! Safari ya Jangwani ilisheheni uasi uliozimwa na huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Kama ilivyokuwa kwenye Agano Jipya, hata leo hii, Kristo Yesu anataka kuwaambia waja wake “Jipeni moyo, ni mimi, msiogope”. Hii ni changamoto kwa viongozi wa Kanisa kuwashirikisha huruma na upendo wa Mungu wale wote waliokata tamaa na kuanza kutembea katika uvuli wa mauti. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa faraja kama wao wenyewe walivyofarijiwa na Mwenyezi Mungu katika safari ya jangwa la maisha ya kiroho!

Tafakari wakati wa mafungo maisha ya kiroho Kipindi cha Kwaresima kwa wasaidizi wa karibu wa Baba Mtakatifu Francisko yaani, “Curia Romana” kuanzia tarehe 1 Machi hadi 6 Machi, 2020 huko Ariccia nje kidogo ya mji wa Roma, inaongozwa na Padre Pietro Enrico Bovati, SJ, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa ya Biblia na Mtaalam wa Sayansi ya Maandiko Mtakatifu. Kauli mbiu ya mafungo haya ni “Kile kijiti kiliwaka moto: mkutano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu mintarafu mwanga wa Kitabu cha Kutoka, Injili ya Mathayo na Sala ya Zaburi”. Padre Pietro Enrico Bovati, katika tafakari yake, Alhamisi tarehe 5 Machi 2020 amegusia kuhusu mapambano ya maisha ya kiroho kwa kutumia silaha ya sala! Viongozi wa Kanisa wanapaswa kusimama kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwaendeleza watu wa Mungu katika maeneo yao. Kanisa katika Ulimwengu mamboleo linakabiliana na mashambulizi makali dhidi ya maisha na utume wake.

Wakristo wanahamasishwa kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, huku wakiendelea kukita maisha yao katika sala, silaha madhubuti ya maisha ya kiroho. Mwenyezi Mungu anawataka waamini kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano thabiti pamoja naye kwa njia ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hiki ni kielelezo cha moyo wa shukrani kwa wito na zawadi maisha ambayo Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake! Kwa wale wote ambao Mwenyezi Mungu amewapaka mafuta na kuwaweka wakfu kuwa ni makuhani wake wanapaswa kutambua kwamba, huduma ya kwanza wanayopaswa kuipatia kipaumbele katika maisha, wito na utume wao ni sala kwa ajili ya kuwaombea walimwengu ambao wanakumbana na magonjwa na wengi wao wamejeruhiwa sana. Wakleri wajenge utamaduni wa kusali daima, kwa kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha tafakari hii katika maisha na utume wao kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Wawe ni watu wakarimu kwa kutambua kwamba, wameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni mashuhuda na vyombo vya neema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Musa Mtumishi wa Mungu katika Agano la Kale alisali sana kwa ajili ya kuwaombea Waisraeli, lakini pia aliwaonesha kwa vitendo huruma ya Mungu pale walipotopea katika dhambi na ubaya wa moyo; akawaonjesha huruma ya Mungu inayoganga, inayoponya na kuokoa. Musa alitikiswa katika msingi wa imani yake pale Waisraeli walipomwomba maji Jangwani, haya ndiyo “Maji ya Masa na Meriba”. Waisraeli walitaka kujaribu kuona ikiwa kama Mwenyezi Mungu alikuwa kati yao! Padre Pietro Enrico Bovati anasema, haya yalikuwa ni majaribu hatari sana katika: wito, maisha na utume wa Musa. Katika muktadha huu, Musa akafanya tafakari ya kina, akapambana na hali iliyokua mbele yake na hatimaye, akajiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala. Akapigana na Waamaleki na Waisraeli wakashinda vita hii na kutambua kwamba kwa hakika, Mwenyezi Mungu alikuwa kati pamoja nao! Dhamana na wajibu wa Mapadre katika Jumuiya ni kuongoza kwa hekima na busara ili kukabiliana na adui anayetishia maisha, ustawi na maendeleo ya watu wao. Kanisa tangu mwanzo wa maisha na utume wake, limekumbana na dhuluma, nyanyaso na mashambulizi mbali mbali kutoka kwa viongozi wa kisiasa na sheria kandamizi.

Kumekuwepo na manabii wa uwongo ambao wamepandikiza mbegu ya chuki na uhasama kati ya watu, kiasi kwamba, hata leo hii, Wakristo wengi sehemu mbali mbali za dunia wanaendelea kudhulumiwa, kunyanyaswa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Kama ilivyokuwa kwa Waamaleki waliokuwa na nguvu za kijeshi hata leo hii, Kanisa linapambana kufa na kupona na sera pamoja na mikakati ya kiuchumi inayolenga kudumisha mafao ya watu wachache ndani ya jamii, dhidi ya utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi. Katika hali na mazingira kama haya, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa njia ya maisha adili na matakatifu sanjari na kuendelea kujikita katika sala inayomwilishwa katika matendo, kama kielelezo makini cha imani tendaji. Waamini wasimame kidete kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Waamini wanapaswa kuwa na maandalizi kamambe ili kupambana kikamilifu katika vita hii. Maandalizi makini katika elimu dunia, maisha ya kiroho, kimaadili ni kiutu ni muhimu sana ili kuweza kukabiliana kwa ukamilifu zaidi na mafundisho potofu na ukanimungu unaokuja kwa kasi kubwa kama majeshi ya Waamaleki. Katika mapambano haya, waamini wasisahau kumwita na kumshirikisha Mungu ambaye daima yuko kati pamoja nao kama alivyofanya Musa kwenye Agano la Kale. Musa alipata ushindi kwa njia ya Sala. Umoja, upendo na mshikamano ni mambo msingi katika mchakato mzima wa kuhakikisha kwamba, ushindi wa kishindo unapatikana. Sala na tafakari inayomwilishwa katika matendo ni mambo muhimu sana katika kutafuta ushindi.

Mwinjili Mathayo katika sura ya 17:14-21 anaonesha jinsi ambavyo Yesu alimponya kijana aliyekuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kifafa! Wanafunzi wake hawakufua dafu mbele ya ugonjwa huu kwani pepo wa namna ya hii anatolewa kwa kuwa na imani thabiti, kwa sala na kufunga. Hii ndiyo nguvu ya maisha ya kiroho inayoweza kuwasaidia Wakristo kupambana na matatizo na changamoto mbali mbali za maisha. Bila ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ni bure! Sala ipate chimbuko lake kutoka katika sakafu ya maisha ya kiroho, kwa kumshikirisha Mwenyezi Mungu katika hali ya unyenyekevu, tayari kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani!

Padre Pietro Enrico Bovati anasema, viongozi wa Kanisa wamepewa dhamana ya kusali na kuwaombea watu wa Mungu. Wao ni mashuhuda, wajenzi na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake. Huduma hii inapaswa kukita mizizi yake katika sakafu ya maisha ya watu, kwa kuwaondolea watu dhambi zao, tayari kuwapatanisha na Mungu pamoja na jirani zao. Waamini wajenge utamaduni wa kuchunguza dhamiri zao, kutambua dhambi zinazohatarisha mahusiano yao na Mwenyezi Mungu tayari kuzikiri na kuziungama. Utamaduni wa maisha ya sala unamwezesha mwamini kutambua uzito wa dhambi na hivyo kuwa tayari kuziungama. Waamini watambue udhaifu wao tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa na hasa zaidi Sakramenti ya Upatanisho.

Mwinjili Mathayo katika Sura ya 18 anagusia kwamba, uongozi ndani ya Kanisa unasimikwa katika huduma ya upendo. Viongozi wa Kanisa wanapaswa kujizatiti katika mchakato wa kuwatafuta wale waliopotea; kujenga utamaduni wa kusahihishana na kuonyana kidugu; kusamehe, kusahau na kusali pamoja, ili kumwilisha huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Viongozi wa Kanisa waendelee kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za watoto, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wakeshe na kusali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa; wawe tayari kusamehe na kusahau, tayari kuandika ukurasa mpya wa maisha na utume wa Kanisa. Kimsingi, huruma ya Mungu haina mipaka. Mtakatifu Petro, Mtume ni shuhuda makini wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake! Alimkana Kristo Yesu mara tatu, akatubu na kujuta sana, kielelezo cha wale wote wanaotubu na kumwongokea Mungu kwani wanabarikiwa na kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu!

Mafungo ya Kiroho: Sala
06 March 2020, 16:41