Tafuta

Vatican News
Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na ni kikolezo cha maendeleo fungamani ya binadamu Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na ni kikolezo cha maendeleo fungamani ya binadamu  (ANSA)

Siku ya Maji Duniani 2020:Maji na Mabadiliko ya Tabianchi!

Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu ana haki ya kupata maji safi, salama! Binadamu anapaswa kujifunza kutumia rasilimali maji kwa unyenyekevu. Haki ya maji safi na salama ni kati ya changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo. Kuna baadhi ya nchi ambazo zinapinga maji kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Maji ni uhai na kikolezo cha maendeleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, maji ni hitaji muhimu sana katika maisha ya binadamu na linachangia katika mchakato wa kuweka uwiano sawa katika mazingira na maisha ya watu katika ujumla wake. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, watu wanapata maji safi na salama kwa ajili ya mahitaji yao. Kila kukicha hitaji la maji safi na salama linaendelea kuongezeka maradufu sehemu mbali mbali za dunia. Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu ana haki ya kupata maji safi, salama na yenye ubora! Binadamu anapaswa kujifunza kutumia rasilimali maji kwa unyenyekevu bila kuyachafua. Haki ya maji safi na salama ni kati ya changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba kuna baadhi ya nchi ambazo bado hazijatambua kwamba, maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na baadhi ya nchi zinapinga maji kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu.

Rasilimali maji inapaswa kushughulikiwa kikamilifu kwani hii ni sehemu muhimu sana katika mchakato wa maboresho ya maisha ya binadamu sanjari na mapambano dhidi ya umaskini duniani. Rasilimali maji inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika sera za kitaifa na kimataifa kutokana na umuhimu wake kwa maisha ya binadamu. Sera hizi ziwe na mwelekeo wa kisiasa na kisheria, kama ilivyokubaliwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2010 mintarafu haki ya maji safi na salama pamoja na afya bora. Wadau mbali mbali wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu, kwani hii ni sehemu ya mustakabali wa binadamu kwa siku za usoni. Vijana wa kizazi kipya waelimishwe kuhusu umuhimu wa rasilimali maji katika maisha ya binadamu.

Monsinyo Fernando Chica Arellano, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye: Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo wa Umoja wa Mataifa, IFAD pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP anasema, Jumuiya ya Kimataifa imeadhimisha Wiki ya Maji kuanzia tarehe 16-22, Machi 2020. Maadhimisho haya yameongozwa na kauli mbiu “Water and Climate change” yaani “Maji na Mabadiliko ya Tabianchi”. Kulikuwa hakuna kishindo kikubwa kutokana na tahadhari ya maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Takwimu za Umoja wa Mataifa zilizotolewa na UNESCO zinabainisha kwamba, kuna jumla ya watu bilioni mbili hawana maji safi wala salama. Hii ni sawa na idadi ya watu 3 kati ya watu 10 duniani na sehemu kubwa ya watu hawa ni kutoka Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara. Takwimu za UNICEF zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu bilioni 4 ambao hawana huduma bora za afya.

Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani! Kwa mwaka 2020 mkazo unawekwa juu ya upatikanaji wa maji safi na salama, ubora na usawa wa upatikanaji wa huduma za afya.

Maji ni uhai na ni kikolezo kikuu cha maendeleo fungamani ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, upatikanaji wa maji safi na salama unazidizi kupungua kila kukicha kutokana na tabia ya baadhi ya watu katika jamii kutaka kuibinafsisha rasilimali maji na kuifanya kuwa sawa na bidhaa zilizoko chini ya sheria za soko. Lakini ikumbukwe kwamba, maji safi na salama ya kunywa ni haki msingi ya binadamu, maji ni lazima kwa uhai wa mwanadamu na pia ni sharti la utekelezaji wa haki nyingine za binadamu. Kumbe, kuna haja ya kulinda na kutunza vyanzo vya maji sanjari na kujenga utamaduni wa matumizi bora ya maji. Uchafuzi na matumizi mabaya ya maji ni jambo ambalo linaonekana kuanza kuzoeleka hasa huko Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini, maeneo ambayo kwa kiasi kikubwa yameathirika kutokana na kuenea kwa Jangwa.

Mama Kanisa ameendelea kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu wanapata huduma bora ya maji safi na salama; kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote pamoja na kuhakikisha kwamba, kilimo kinakua ni endelevu. Sera na mikakati ya huduma ya maji haina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi badala ya kugeuza rasilimali maji kuwa ni bidhaa inayoratibiwa na nguvu ya soko. Utamaduni wa kulinda vyanzo vya maji upewe kipaumbele cha pekee, ili watu waweze kuwa na uhakika wa ubora na kiwango cha maji kinachotolewa kwa ajili ya mahitaji ya binadamu. Mahitaji ya maji yanazidi kuongezeka kila mwaka lakini upatikanaji wake, unaendelea pia kupungua kila kukicha. Matumizi bora ya maji yasaidie kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambacho kwa sasa ni kati ya vyanzo vikuu vya majanga na umaskini duniani.

Siku ya Maji Duniani 2020

 

26 March 2020, 10:55