Kanisa Katoliki nchini DRC kuanzia tarehe 4-14 Juni 2020 linaadhimisha Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa. Kardinali Luis Antonio Tagle, anamwakilisha Baba Mtakatifu Francisko. Kanisa Katoliki nchini DRC kuanzia tarehe 4-14 Juni 2020 linaadhimisha Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa. Kardinali Luis Antonio Tagle, anamwakilisha Baba Mtakatifu Francisko. 

Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa, DRC: 4-14 Juni 2020

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kuwa mwakilishi wake maalum katika Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa, litakaloadhimishwa kuanzia tarehe 4-14 Juni 2020, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo. Kongamano hili linapania kuwa ni katekesi ya kina kuhusu Ekaristi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameteuwa Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kuwa mwakilishi wake maalum katika Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa, litakaloadhimishwa kuanzia tarehe 4-14 Juni 2020, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo. Maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu katika ngazi mbali mbali ni sehemu ya utekelezaji wa sera ma mikakati ya shughuli za kichungaji ziliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu umuhimu wa Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa ni katekesi endelevu na ya kina: kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu kuna mkate na divai, ambavyo kwa maneno ya Kristo Yesu na kwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu hugeuka kuwa Mwili na Damu ya Azizi ya Kristo Yesu, chakula cha kiroho na masurufu ya njiani.

Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo; zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa, kuwasha na kupyaisha mapendo kwa Mungu na jirani. Ni Sakramenti ya Altare, mahali pa kukutana mubashara na Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai; Mwili na Damu yake Azizi. Ekaristi Takatifu ni Fumbo na muhtasari wa imani ya Kanisa. Hii ni zawadi ya upendo inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kwa kumwonesha Kristo Yesu kuwa kweli ni Mwanakondoo wa Mungu na sadaka hai inayotolewa kwa ajili ya maondoleo ya dhambi na maisha ya uzima wa milele! Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha Kristo anayejitoa mwenyewe kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa pamoja na utendaji wake. Hii ni Sakramenti ya umoja wa Kanisa, inayoimarisha na kudumisha upatanisho kati ya Mungu na jirani.

Mababa wa Kanisa wanasema, Ekaristi Takatifu ni Fumbo linalopaswa kuadhimishwa kwa Ibada, Uchaji wa Mungu na Uaminifu, ili kuonja: uzuri, ukuu na utakatifu wa Sakramenti hii ya ajabu, inayoonesha Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu kama inavyofafanuliwa na Mtakatifu Thoma wa Akwino! Ekaristi Takatifu ni Fumbo la imani ambalo linapaswa kusadikiwa, kuadhimishwa na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mwamini kama kielelezo cha ushuhuda wa uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya upendo, zawadi kuu kutoka kwa Yesu Kristo mwenyewe, katika maumbo ya mkate na divai. Ni chakula cha kweli katika maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Ekaristi kwa jirani zao kwa njia ya matendo ya huruma yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kielelezo makini cha imani tendani.

Maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu ni kipindi cha katekesi ya kina kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, Sala na Tafakari ya kina ya Neno la Mungu inayofanywa na Jumuiya ya waamini wa Kanisa mahalia mintarafu Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kama njia ya kuendelea kuzungumza na Kristo katika safari ya maisha ya waamini. Ni muda wa kuimarisha katekesi kuhusu Sakramenti ya Upatanisho, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Kongamano Ekaristi Takatifu DRC
19 March 2020, 14:45