Kardinali Luis Tagle anasema, Kwaresima ni muda muafaka wa kutafakari kwa makini maana ya Kipindi cha Kwaresima katika maisha ya mwamini! Kardinali Luis Tagle anasema, Kwaresima ni muda muafaka wa kutafakari kwa makini maana ya Kipindi cha Kwaresima katika maisha ya mwamini! 

Virusi vya Corona, COVID-19: Muda wa kugundua maana ya Kwaresima

Katika kipindi hiki cha hofu na mashaka kuhusu kuenea kwa kasi kwa maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19; tafakari ya kina ya Neno la Mungu, kusali, kufunga, matendo ya huruma na maisha ya Kisakramenti ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele katika kipindi hiki ambacho waamini wengi wanakabiliana na ukame wa maisha ya kiroho kutokana na athari za Virusi vya Corona.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwaresima ni kipindi cha mapambano ya “Jangwa la maisha ya kiroho” kwa kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha. Kwa kufunga na kusali; kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, sanjari na kujikita katika maisha ya kisakramenti ili kupata: neema na baraka, toba na wongofu wa ndani. Kwaresima ni muda uliokubalika kwa waamini kujizatiti katika maisha ya kiroho kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Kwa njia hii, waamini wanakuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Kristo Mfufuka kwa watu wa Mataifa! Huu ni mwaliko wa kujibu wito huu kwa uhuru mkamilifu unaochota nguvu zake katika Fumbo la Pasaka.

Waamini wawe wepesi kukubali na kupokea upendo wa Mungu ambao umefunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu, ili kujenga mahusiano wazi na majadiliano yenye tija na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani kwa njia ya Sala, matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwa kujenga na kudumisha moyo wa uvumilivu na utayari wa kusamehe na kusahau! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2020 unaongozwa na kauli mbiu “Twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: Mpatanishwe na Mungu.” 2 Kor. 5:20. Anasema, Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ndicho kiini cha toba na wongofu wa ndani, unaowawezesha waamini kumgusa Kristo Yesu kwa njia ya imani kwa wale wote wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Mpatanishwe na Mungu ni tema inayoongoza ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2020 maana yake ni: wongofu na mwaliko kwa binadamu kumrudia tena Mungu wake.

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu ambaye pia ni Askofu mkuu Mstaafu wa Jimbo kuu la Manila katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa watu wa Mungu nchini Ufilippini, anawataka kutumia fursa hii kugundua maana na umuhimu wa Kipindi cha Kwaresima katika maisha yao ya kila siku. Katika kipindi hiki cha hofu, wasi wasi na mashaka kuhusu kuenea kwa kasi kwa maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19; tafakari ya kina ya Neno la Mungu, kusali, kufunga, matendo ya huruma na maisha ya Kisakramenti ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika kipindi hiki ambacho waamini wengi wanakabiliana na ukame wa maisha ya kiroho kutokana na athari za Virusi vya Corona, COVID-19. Huu ni wakati muafaka wa kumwilisha matendo ya huruma na mapendo kwa waathirika wa magonjwa mbali mbali, lakini kwa namna ya pekee wagonjwa wanaosumbuliwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Kufunga kunaweza kupewa maana nyingi, yaani kwa kujikatalia mambo yasiyo na msingi sana katika maisha, kwa kuambata na kuzingatia mambo muhimu zaidi. Ni wakati muafaka wa kujikita katika kanuni maadili na utu wema na kamwe wafanyabiashara wasitumie athari za ugonjwa wa Corona, COVID-19 kujipatia faida kubwa! Kwa wale waliobahatika katika maisha, wawe wepesi kuwagawia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii utajiri wa maisha yao: kiroho na kimwili. Katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19 kuna haja ya kushinda hofu na wasi wasi usiokuwa na mashiko. Huu ni wakati wa kusali zaidi ili kujenga na kuboresha mahusiano na Mwenyezi Mungu. Ni wakati wa kusikiliza na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha. Virusi vya Corona, COVID-19 hadi kufikia tarehe 14 Machi 2020, watu 98 tayari walikuwa wamekwisha kuambukizwa na virusi hivi nchini Ufilippini.

Kardinali Tagle
16 March 2020, 14:18