Idara ya Toba ya Kitume imetoa Tamko Kuhusu Waamini wanaoweza kupata Rehema Kamili wakati huu wa mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Idara ya Toba ya Kitume imetoa Tamko Kuhusu Waamini wanaoweza kupata Rehema Kamili wakati huu wa mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. 

Virusi vya Corona, COVID-19: Tamko Kuhusu Rehema Kamili

Idara ya Toba ya Kitume imetoa Tamko Kuhusu Rehema Kamili inayotolewa na Mama Kanisa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo vinaendelea kupelekea vifo vya makundi makubwa makubwa ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Waamini wanahimizwa kudumu katika imani, matumaini na sala katika kipindi hiki kigumu cha mahangaiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rehema hupatikana kwa njia ya Kanisa, ambalo, kwa nguvu ya uweza wa kufunga na kufungua, lililopewa na Kristo Yesu, huingia kati kwa manufaa ya Mkristo na hufungua hazina ya mastahili ya Kristo na watakatifu ili kupata kwa Baba wa huruma msamaha wa adhabu za muda zinazotokana na dhambi zao. Hivi Mama Kanisa hataki tu kutoa msaada kwa watoto wake hawa, bali pia kuwachochea kwa kazi za uchaji, toba na mapendo. Katekisimu ya Kanisa Katoliki (n.1471), mintarafu rehema kamili inatuelewesha kwamba: Rehema ni msamaha mbele ya Mungu ambao kosa lake lilikwishafutwa, msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata kutoka katika hazina ya malipizi ya Kristo na ya Watakatifu. Rehema inaweza kuwa ya muda au Kamili. Rehema ya muda huondoa sehemu ya adhabu ya adhabu za dhambi na rehema kamili huondoa adhabu zote (Rej. KKK, n.1472).

Mkristo huweza kupata rehema kamili kwa ajili yake yeye mwenyewe au kwa ajili ya marehemu kama atatimiza yafuatayo: Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa. Pili apokee Sakramenti ya Upatanisho. Tatu, apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa rehema kamili. Nne; asali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu. Mwishoni atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa rehema Kamili. Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Toba ya Kitume kwa kushirikiana na Monsinyo Krzysztof Nykiel, Hakimu wa Idara ya Toba ya Kitume "Penitenzieria Apostolica" wametoa Tamko Kuhusu Rehema Kamili inayotolewa na Mama Kanisa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo vinaendelea kupelekea vifo vya makundi makubwa makubwa ya watu sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Mauro Piacenza anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kudumu katika imani, matumaini na sala katika kipindi hiki kigumu cha mateso, mahangaiko pamoja na majanga asilia. Kanisa ambaye ni Mama na Mwalimu anawahimiza watoto wake kugundua Fumbo la Mateso katika maisha ya mwanadamu, kama sehemu ya kazi ya ukombozi wa mwanadamu. Ni katika mateso, mwanadamu anagundua utu, heshima na utume wake. Katika kipindi hiki kigumu, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha ukaribu wake kwa njia ya sala na sadaka kwa wale wote walioathirika kwa Virusi vya Corona, COVID-19. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali, kufunga na kuwasaidia waathirika wa ugonjwa huu. Wagonjwa watumie fursa hii kuuona mpango wa ukombozi ulioletwa na Kristo Yesu, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Huu ni mwaliko kwa waamini kutubu na kumwongokea Mungu.

Idara ya Toba ya Kitume, “Penitenzieria Apostolica” inatoa Rehema Kamili kwa watu walioshambuliwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Rehema hii inatolewa kwa waamini ambao wamewekewa karantini wakiwa hospitalini au majumbani mwao. Ikiwa kama kutoka katika undani wa mioyo yao wataweza kutubu na hatimaye, kujiunga na vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa ajili ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Kwa kusali Rozari Takatifu, Kufanya Njia ya Msalaba au kuhudhuria Ibada nyingine zinazotolewa na Mama Kanisa. Wajitahidi walau kusali: Kanuni ya Imani, Baba Yetu na Salam Maria kwa kutolea mahangaiko yao kwa Mwenyezi Mungu katika imani na upendo kwa jirani zao, kama njia ya kutimiza malipizi ya dhambi zao pamoja na kusali kwa njia za Baba Mtakatifu, pale itakapowezekana.

Rehema hii inatolewa pia kwa wafanyakazi katika sekta ya afya na wanafamilia wote wanaowahudumia wagonjwa kwa kufuata mfano wa Msamaria mwema. Rehema hii inatolewa kwa waamini watakaoweza pia kuabudu Ekaristi Takatifu, watakaoweza kusoma walau Neno la Mungu kwa muda wa nusu saa, au kusali Rozari, kufanya Njia ya Msalaba au kusali Rozari ya Huruma ya Mungu, ili kuomba huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka, ili kuwaondolea watoto wake balaa la ugonjwa huu wa Virusi vya Corona, COVID-19. Mama Kanisa anaendelea kusali kwa ajili ya waamini ambao hawataweza kupata fursa ya kupokea Mpako wa Wagonjwa, kwa kuwaweka chini ya huruma ya Mungu, nguvu na umoja wa watakatifu, ili hatimaye, waweze kupokea fumbo la kifo kwa amani na utulivu wa ndani. Kanisa linakimbilia ulinzi wa Bikira Maria, Mama wa Mungu na wa Kanisa, Afya ya wagonjwa likiomba tunza yake ya kimama, ili kuwaombea watoto wake wote ili waweze kupona dhidi ya ugonjwa huu.

Rehema Kamili

 

21 March 2020, 16:45