Tafuta

Vatican News
Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu: Hati: Aqua Fons Vitae: Maji Chanzo Cha Uhai: Mwelekeo wa Matumizi Bora wa Maji: Alama ya Kilio cha Maskini na Dunia Mama. Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu: Hati: Aqua Fons Vitae: Maji Chanzo Cha Uhai: Mwelekeo wa Matumizi Bora wa Maji: Alama ya Kilio cha Maskini na Dunia Mama.  (ANSA)

Aqua Fons Vitae: Maji Ni Chanzo Cha Uhai: Mwelekeo wa Matumizi Bora ya Maji

Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya binadamu limechapisha Hati: “Maji Ni Chanzo cha Uhai; Mwelekeo wa Matumizi Bora ya Maji: Alama ya Kilio cha Maskini na Kilio cha Dunia Mama” “Aqua Fons Vitae”. Hati hii ni tafakari ya kina inayoonesha umuhimu wa maji kama chanzo cha maisha na kikolezo cha maendeleo fungamani; utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, maji ni hitaji muhimu sana katika maisha ya binadamu na linachangia katika mchakato wa kuweka uwiano sawa katika mazingira na maisha ya watu katika ujumla wake. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, watu wanapata maji safi na salama kwa ajili ya mahitaji yao. Kila kukicha hitaji la maji safi na salama linaendelea kuongezeka maradufu sehemu mbali mbali za dunia. Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu ana haki ya kupata maji safi, salama na yenye ubora! Binadamu anapaswa pia kujifunza kutumia rasilimali maji kwa unyenyekevu mkuu. Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu limechapisha Hati Juu ya “Maji Chanzo cha Uhai; Mwelekeo wa Matumizi Bora ya Maji: Alama ya Kilio cha Maskini na Kilio cha Dunia Mama” “Aqua Fons Vitae”. Hati hii ni tafakari ya kina inayotoa sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu kwa kazi ya uumbaji inayoonesha umuhimu wa maji kama chanzo cha maisha na kikolezo cha maendeleo fungamani ya binadamu.

Hati hii ni muhtasari wa mafundisho ya Mababa wa Kanisa kuhusu rasilimali maji ambayo ni kwa ajili ya mafao ya wengi, inayohitaji kuheshimiwa na kutumiwa kwa ukarimu na upendo, mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Rasilimali maji inagusa: Utu, heshima na haki msingi za binadamu. Inafumbatwa katika mchakato wa mshikamano unaratibiwa na kanuni auni, kwa ajili ya mafao ya wengi. Hii ni sehemu ya ekolojia na maendeleo fungamani ya binadamu yanayotoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hati hii inapania kuendeleza tafakari kuhusu rasilimali maji, maendeleo na maisha ya mwanadamu kwa siku za usoni. Ni sehemu ya utume wa Kanisa katika kukuza na kudumisha majadiliano na wadau mbali mbali katika sekta ya maji na maendeleo fungamani ya binadamu. Ni mwaliko na wito wa kutumia maji kwa heshima na nidhamu; kwa uwajibikaji na upendo, kama kielelezo cha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ili kufikia malengo haya, kuna haja ya kuwa na wongofu wa kiekolojia. Hati ya “Aqua fons vitae” imegawanyika katika sehemu kuu nne: Utambuzi wa umuhimu wa maji; Maji kwa matumizi ya binadamu; Maji kwa shughuli za binadamu na hatimaye, Eneo la Maji.

Utambuzi wa Umuhimu wa Maji: Kanisa kama Mama na Mwalimu limeendelea kutafakari rasilimali maji kama chanzo cha uhai, kikolezo cha maendeleo fungamani ya binadamu na kwamba, watu wanawajibika kutunza vyema vyanzo vya maji, ili kudumisha afya bora. Kama sehemu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030, Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama. Utamaduni wa kulinda vyanzo vya maji upewe kipaumbele cha pekee, ili watu waweze kuwa na uhakika wa ubora na kiwango cha maji kinachotolewa kwa ajili ya matumizi ya binadamu. Mahitaji ya maji yanazidi kuongezeka kila mwaka lakini upatikanaji wake, unaendelea pia kupungua kila kukicha. Matumizi bora ya maji yasaidie kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambacho kwa sasa ni kati ya vyanzo vikuu vya majanga na umaskini duniani. Maji yana thamani kubwa katika maisha ya kiroho kwa waamini wa dini mbali mbali kwani yanagusa undani wa mtu na utakaso wake. Maji yana thamani katika maisha ya kijamii, kitamaduni na yana uzuri wake katika kazi nzima ya uumbaji. Maji ni kiungo muhimu sana cha tunu msingi za maisha ya binadamu na kikolezo cha amani duniani. Maji yana thamani kubwa katika shughuli mbali mbali za kiuchumi ndiyo maana Kanisa linasema kwamba, maji kamwe haiwezi kugeuzwa kuwa sawa na bidhaa nyingine zinazopimwa kwa nguvu ya soko. Maji yanagusa utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Sehemu ya Kwanza: Maji kwa Matumizi ya Binadamu. Kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama duniani kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ongezeko kubwa la watu duniani. Kuna uchafuzi wa vyanzo vya maji wakati wa vita na kinzani; ukataji wa miti ovyo na uchomaji wa misitu. Uchafuzi wa vyanzo vya maji umekuwa pia ni sababu ya kuenea kwa magonjwa ya milipuko sehemu mbali mbali za dunia na hivyo kuhatarisha afya za watu. Wakati mwingine maji yametumika kama silaha ya maangamizi. Kutokana na changamoto zote hizi, Kanisa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali linapenda kuragibisha umuhimu wa maji katika maisha ya mwanadamu kama sehemu ya Mafundisho Jamii ya Kanisa na haki msingi za binadamu, ili kuwasaidia watu wa Mungu kuibuka na sera na mikakati itakayolinda na kutunza maji kwa ajili ya wengi! Makanisa mahalia yanapaswa kujihusisha kikamilifu katika mchakato wa utunzaji bora wa maji, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Sehemu ya Pili: Maji kwa Shughuli za Binadamu: Maji yamekuwa yakitumika katika kilimo cha umwagiliaji, ufugaji, uzalishaji wa umeme pamoja na shughuli mbali mbali na kama mahali pa mapumziko. Lakini kutokana na shughuli kubwa zinazofanywa na binadamu baadhi ya mito kwa sasa imeanza kukauka. Kuna baadhi ya sehemu maji baridi yamegeuka kuwa ni maji ya chumvi yasiyofaa tena kwa matumizi ya binadamu. Uvunaji ovyo wa misitu umeharibu vyanzo vya maji pamoja na uchafuzi mkubwa wa maji unaofanywa na viwanda. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la mahitaji na matumizi ya maji kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu pamoja na kupanuka kwa miji. Vipaumbele vimekuwa vikitofautiana kati ya nchi na nchi. Hakuna usawa katika upatikanaji wa maji safi na salama. Maji kwa matumizi ya maendeleo ya viwanda ni changamoto kubwa. Changamoto zote hizi zinapaswa kuvaliwa njuga ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama.

Sehemu ya Tatu: Eneo la Maji. Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya asilimia 70% ya eneo lote la uso wa dunia linafunikwa na maji. Lakini kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote, eneo la maji linaweza kuongezeka maradufu na hivyo kutishia usalama wa maisha ya watu na mali zao. Kumekuwepo na migogoro ya mipaka mintarafu shughuli za uvuvi pamoja na uvuvi usiozingatia kanuni maadili na utu wema. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi. Waamini washirikiane na watu mbali mbali katika kulinda na kudumisha mazingira bora. Mama Kanisa anapenda kushirikiana na: Serikali, Taasisi na Mamlaka mbali mbali za Maji ili kulinda na kuendeleza rasilimali ya maji duniani. Watu wajenge utamaduni wa utunzaji bora wa maji, kwa kuzingatia haki msingi za binadamu na utawala bora. Umefika wakati wa kuimarisha Utume wa Bahari; Kupambana na biashara ya binadamu na viungo vyake; kuadhimisha Siku za Kimataifa zinazohusiana na Matumizi ya Maji.

Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu linahitimisha Hati Juu ya “Maji Chanzo cha Uhai; Mwelekeo wa Matumizi Bora ya Maji: Alama ya Kilio cha Maskini na Kilio cha Dunia Mama” “Aqua Fons Vitae” kwa kukazia elimu fungamani kwa ajili ya ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu; ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza kwa makini; majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na kuonesha utashi wa kutaka kuelewa na hatimaye, kutenda kwa haki. Watu wanapaswa kusimama kidete kupambana na rushwa na ufisadi unaohatarisha rasilimali ya maji duniani. Hati hii inachota utajiri wake kutoka katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, Katekisimu ya Kanisa Katoliki pamoja na Nyaraka mbali mbali za Mababa wa Kanisa tangu baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Hati ya Maji

 

 

31 March 2020, 15:20