Vatican News
Tarehe 22 Februari ya kila mwaka, Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, Mtume: Umoja wa Kanisa! Tarehe 22 Februari ya kila mwaka, Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, Mtume: Umoja wa Kanisa!  (Vatican Media)

Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, Mtume! Umoja wa Kanisa

Ukulu wa Mtakatifu Petro ni kielelezo cha mamlaka aliyopewa na Kristo Yesu ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifu watu wa Mungu katika kifungo cha upendo. Kwa namna ya pekee katika maadhimisho haya, tumkumbuke na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ili aweze kutekeleza vyema mapenzi y Mungu, licha ya changamoto mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 22 Februari, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, aliyemkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu mwenyewe akamtibitishia Ukulu huu kwa kumwambia “Wewe ndiwe Petro na juu ya Mwamba huu nitalijenga Kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda”. Mt. 16:18. Ukulu wa Mtakatifu Petro ni kielelezo cha mamlaka aliyopewa na Kristo Yesu ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifu watu wa Mungu katika kifungo cha upendo.

Mtume Petro alikirimiwa neema ya pekee iliyomwezesha kumkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu na hivyo kupewa funguo, kama Askofu wa kwanza wa Roma na baada yake wako waandamizi wake, waliopewa dhamana ya kutangaza na kushuhudia: huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Maadhimisho haya ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ambaye kwa sasa ni Baba Mtakatifu Francisko. Maadhimisho haya iwe ni fursa kwa ajili ya kuombea umoja na mshikamano wa Kanisa katika masuala, imani, maadili na utu wema! Tumkumbuke na kumwombea kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ili daima aweze kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake.

Ukulu wa Mt. Petro

 

 

21 February 2020, 14:59