Tarehe 29 Februari 2020 Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Magonjwa Adimu Duniani ambao kwa sasa wamefikia zaidi ya milioni 300. Tarehe 29 Februari 2020 Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Magonjwa Adimu Duniani ambao kwa sasa wamefikia zaidi ya milioni 300. 

Ujumbe wa Vatican kwa Siku ya XIII ya Magonjwa Adimu Duniani, 2020

Tarehe 29 Februari 2020 inaadhimisha Siku ya XIII ya Magonjwa Adimu Duniani (Rare disease, Malattie Rare). Haya ni magonjwa ambayo yanawaandama watu wachache sana katika jamii, kiasi kwamba, hata tiba yake pia inakumbana na ukakasi mkubwa. Ni magonjwa ambayo hayana tiba na ni ya kudumu. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya wagonjwa milioni 300 duniani kote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 29 Februari 2020 inaadhimisha Siku ya XIII ya Magonjwa Adimu Duniani (Rare disease, Malattie Rare). Haya ni magonjwa ambayo yanawaandama watu wachache sana katika jamii, kiasi kwamba, hata tiba yake pia inakumbana na ukakasi mkubwa. Ni magonjwa ambayo hayana tiba na ni ya kudumu. Watu walioathirika kwa magonjwa adimu ni changamoto kubwa katika mfumo mzima wa huduma inayotolewa na Sekta ya Afya. Hawa ni wagonjwa ambao wanataka kuona kwamba, utu, heshima na haki zao msingi zinaheshimiwa na kuthaminiwa na wote. Wanamani siku moja waweze kupata dawa na tiba muafaka itakayowaondolea au kuwapunguzia maumivu makali wanayokumbana nayo katika safari ya maisha yao hapa duniani!

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, katika ujumbe wake kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku XIII ya Magonjwa Adimu Duniani anasema, kiini cha maadhimisho haya kwa mwaka 2020 ni usawa kwa watu walioathirika na magonjwa haya, kwani takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya wagonjwa milioni 300 sehemu mbali mbali za dunia wanaoshambuliwa na magonjwa adimu. Idadi hii ni kubwa na kamwe haiwezi kufumbiwa macho! Haya ni magonjwa ambayo si rahisi sana kufanyiwa uchungu na kwa sehemu kubwa wagonjwa pamoja na familia zao, wanaishi katika mazingira magumu kiasi hata cha kunyanyapaliwa na jamii. Kuna wagonjwa wengine wanaoishi katika upweke hasi kiasi cha kukata tamaa na kuanza kuchungulia kaburi. Kuna baadhi ya wagonjwa hawawezi kupata msaada wanaohitaji kutokana na udhaifu mkubwa unaooneshwa kwenye mifumo ya huduma mbali mbali katika sekta ya afya.

Ikumbukwe kwamba, wagonjwa wanayo haki msingi ya kuhakikisha kwamba, wanapata tiba ya magonjwa yanayowasumbua, kama kielelezo cha haki kinachodai ugawaji na matumizi sawa ya rasilimali za nchi. Hiki ni kielelezo makini kinachoonesha kujali haki ya afya bora na utu wa kila mtu, lakini kwa wahitaji zaidi na maskini. Tafiti za kisayansi zinao mchango mkubwa katika mchakato wa maboresho ya tiba na afya kwa watu wenye magonjwa adimu. Jambo la msingi ni kutambua dalili, kutoa tiba muadaka na huduma bora zaidi inayohitajika. Tafiti za kisayansi zinahitaji pia ushiriki mkamilifu wa wagonjwa wenyewe, ili kuweza kupata matokeo yanayolenga tiba muafaka kwa magonjwa yanayowasibu. Kumbe, ufahamu wa magonjwa haya kisayansi na utafiti wa dawa muafaka unaofanywa na viwanda vya dawa, ni mambo yanayopaswa kuzingatia utu, heshima na haki msingi za wagonjwa hawa kupata tiba muafaka.

Mshikamano huu wa huruma na upendo katika Jumuiya ya Kimataifa unapaswa kuongozwa na kanuni auni ili kuratibu sera na mikakati ya huduma bora ya afya inatolewa kwa wote, kwa kuzingatia haki na usawa; katika uchunguzi wa magonjwa na hatimaye, kuweza kupata tiba muafaka, bila kusahau msaada wa hali na mali kwa wagonjwa na familia zao. Magonjwa adimu yanayo athari kubwa kwa wagonjwa wenyewe pamoja na familia zao katika medani mbali mbali za maisha; yaani kisaikolojia, kihisia, kimwili na kiuchumi. Mara nyingi wagonjwa wa namna hii hawapati huduma stahiki kutoka kwa jamii inayowazunguka, kiasi kwamba, mzigo wote wa mgonjwa unaielemea familia. Kuna haja ya kupembua kwa kina mapana, ili kuweza kuangalia shughuli mbali mbali zinazofanyika kuwazunguka wagonjwa husika, ili waweze kushirikishwa katika yale mambo ambayo yako kwenye uwezo wao. Lengo ni kukuza na kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano na wagonjwa. Hii ni changamoto ya kukuza na kudumisha udugu wa mshikamano, ili kuhudumiana kama ndugu wamoja; kwa kuunganisha tiba na shughuli mbali mbali za kijamii, ili hata wagonjwa hawa waweze kujisikia kuwa ni sehemu hai ya jamii.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, anahitimisha ujumbe wake katika Siku ya XIII ya Magonjwa Adimu Duniani kwa Mwaka 2020, kwa kuwaweka wagonjwa wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Wagonjwa, “B. Maria Salus Infirmorum”, ili aweze kuwasaidia watu wote kuwa makini zaidi kwa mahitaji ya jirani zao, hususan wagonjwa, ili hatimaye, kujisadaka bila ya kujibakiza huku wakiwa na moyo safi unaobubujika ukarimu na upendo wa dhati!

Siku ya Magonwa Adimu

 

29 February 2020, 16:53