Vatican News
Wafanyakazi wa "Curia Romana" wapanda kwenda mlimani ili kujichimbia katika mafungo ya kiroho! Baba Mtakatifu Francisko hatashiriki mafungo haya kwa mwaka 2020. Wafanyakazi wa "Curia Romana" wapanda kwenda mlimani ili kujichimbia katika mafungo ya kiroho! Baba Mtakatifu Francisko hatashiriki mafungo haya kwa mwaka 2020.  (Vatican Media)

Wafanyakazi wa "Curia Romana" Wapanda mlimani, kujichimbia kwa mafungo!

Tafakari wakati wa mafungo haya ya maisha ya kiroho inaongozwa na Padre Pietro Bovati, SJ, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa ya Biblia na Mtaalam wa Sayansi ya Maandiko Mtakatifu. Kauli mbiu inayoongoza mafungo haya ni “Kile kijiti kiliwaka moto: mkutano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu mintarafu mwanga wa Kitabu cha Kutoka, Injili ya Mathayo na Sala ya Zaburi”. Jangwani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwaresima ni kipindi kinachodumu kwa muda wa Siku Arobaini, kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, kiini cha Mwaka wa Liturujia na imani ya Kanisa. Hii ni hija ya kumfuasa Kristo, ambaye kabla ya kuanza utume wake hadharani, alijitenga kwa ajili ya kusali na kufunga; hatimaye, akajaribiwa Jangwani kwa muda wa Siku Arobaini. Jangwani ni mahali pa kimya kikuu, pasi na kelele isipokuwa upepo mwanana. Ni mahali pa mwamini kujitenga na malimwengu, ili kutoa nafasi ya kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, ili kuleta faraja katika sakafu ya moyo wa mwamini. Kristo Yesu katika Maandiko Matakatifu anazungumzia mara kwa mara kuhusu “Jangwa”. Mwenyezi Mungu kwa njia ya Musa aliwapatia Amri Kumi kule Jangwani. Waisraeli wakatembea Jangwani kwa muda wa miaka 40 ili kutakaswa kabla ya kuingia kwenye Nchi ya Ahadi!

Safari ya Jangwani katika kipindi cha Kwaresima, anasema Baba Mtakatifu Francisko inasimikwa katika: Sala, kufunga, pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Mwenyezi Mungu amewawekea waja wake ahadi ya kutenda mambo mapya kwa kufanya njia hata jangwani na mito ya maji nyikani! Hii ni njia inayotoka katika kifo na kuelekea katika uzima. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuanza safari ya kwenda Jangwani wakiwa wameambata na Kristo Yesu, ili kusherehekea Fumbo la Pasaka kwa kuonja nguvu ya upendo na huruma ya Mungu inayopyaisha maisha yao ya kiroho! Mi katika muktadha huu, wafanyakazi kutoka "Curia Romana" kuanzia tarehe 1-6 Machi 2020 watapanda kwenda Jangwani ili kusali, kutafakari na kujiwekea mikakati ya maisha na shughuli za kichungaji, huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma. Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka huu 2020 hatahudhuria kutokana na kusumbuliwa na mafua!

Tafakari wakati wa mafungo haya ya maisha ya kiroho inaongozwa na Padre Pietro Bovati, SJ, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa ya Biblia na Mtaalam wa Sayansi ya Maandiko Mtakatifu. Kauli mbiu inayoongoza mafungo haya ni “Kile kijiti kiliwaka moto: mkutano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu mintarafu mwanga wa Kitabu cha Kutoka, Injili ya Mathayo na Sala ya Zaburi”. Utamaduni wa kumsikiliza Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha ya mtu ni mang’amuzi ya kinabii kama yanavyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu. Vielelezo vikuu hapa ni kijiti kilichokuwa kinawaka moto, Neno la Mungu lililokuwa linatoka katika moto huu na kuiangazia njia hii ya maisha. Mafungo ya kiroho ni fursa muafaka ya kukutana na kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha ya mwamini.

Mafungo ni nafasi ya kuzama zaidi katika kusoma na kulitafakari Neno la Mungu ambalo kimsingi ni faraja, dira na mwongozo wa maisha. Washiriki wa mafungo wanayo nafasi kusikiliza Neno la Mungu katika Sala kama sehemu ya mang’amuzi ya kinabii, kama alivyofanya Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Kama ilivyokuwa kwa Musa na Kristo Yesu, hata wafuasi wa Kristo wanahimizwa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, ili mwisho wa siku waweze pia kuwasaidia ndugu zao kupata mang’amuzi ya kinabii. Unabii kutoka katika Kitabu cha Kutoka kadiri ya mang’amuzi ya Musa, Mtumishi wa Mungu, Sala ya Zaburi na baadhi ya sehemu za Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo ni kati mambo msingi yatakayowazamisha washiriki katika mafungo haya katika mazingira ya Kipindi cha Kwaresima. Huu ni mwaliko wa kufuata ile Njia ya Watu wa Mungu Jangwani, wakiwa njiani kuupanda Mlima wa Bwana, ili hatimaye, waweze kukutana na Mwenyezi Mungu na hivyo kuonja mang’amuzi ya Fumbo la Pasaka.

Hii ni tafakari ya kina mintarafu mwanga wa Neno la Mungu unaogusa na kuangaza wito, maisha na utume wa Kikasisi; tabia ya kukataa kupokea neema ya Mungu na mwishoni wataangalia dhamana na wajibu wa viongozi ndani ya Jumuiya ya waamini. Hatimaye, wataweza kugundua ukaribu wa Mungu katika maisha ya binadamu; Mwenyezi Mungu anayejitaabisha kumfuata binadamu, ili kumwongoza katika safari ya maisha, tayari kumpyaisha, ili aweze kung’ara mwanga wa Mungu. Sala ni majadiliano kati ya Mungu na mwamini, lakini pia inaonesha undani wa maisha ya mwamini, ambaye yuko tayari kusikiliza kwa makini. Uzoefu na mang’amuzi yanaosimikwa katika utamaduni wa kumsikiliza Mwenyezi Mungu mara kwa mara ni sehemu ya mang’amuzi ya kinabii kama ilivyokuwa kwa Musa, Mtumishi wa Mungu, aliyebahatika kuyafahamu na hatimaye, kuyatekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake.

Hapa kinachohitajika ni: fadhila ya utii, uaminifu na imani; mambo msingi katika mang’amuzi ya maisha ya kiroho. Ni kutokana na changamoto hii, mwamini anapaswa kuzama katika maisha ya sala, kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini bila ya kuwa na mioyo migumu kama ilivyokuwa kwa Waisraeli kule Jangwani. Kimsingi maisha ya Sala sanjari na usikivu wa Neno la Mungu ni mang’amuzi maaluma ya kinabii kama ilivyokuwa kwa Manabii katika Agano la Kale, Kwa Kristo Yesu na Mitume wake katika Agano Jipya. Mwamini katika hali ya sala anakuwa na uwezo wa kumpokea Roho Mtakatifu; kielelezo cha mang’amuzi ya Kipentekoste kwa kila mwamini. Huu ni uzoefu unaomwezesha mwamini kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano binafsi na Mwenyezi Mungu. Neno la Mungu linapaswa kuwa ni dira na mwongozo wa maisha ya mwamini, kwani huu ni mwanga angavu unaotoa maana halisi ya historia na maisha ya binadamu katika uhalisia wake.

Ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwamba, kila mwamini aweze kuwa ni kielelezo cha mwanga angavu, kiongozi na chombo cha matumaini; tayari kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Changamoto hii inapewa kipaumbele cha kwanza na viongozi waliopewa dhamana na nyajibu mbali mbali ndani ya Kanisa Mwishoni mwa mahojiano maalum na Radio Vatican, Padre Pietro Bovati, SJ, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa ya Biblia na Mtaalam wa Sayansi ya Maandiko Mtakatifu anasema, yataka moyo kusimama mbele ya Baba Mtakatifu na wasaidizi wake wa karibu na kuanza kuwamegea amana na utajiri wa Neno la Mungu; uzoefu na mang’amuzi ya maisha ya kiroho yanayobubujika kutokana na kusikiliza Neno la Mungu, chemchemi ya sala na ukweli katika maisha ya mtu binafsi. Anasema, atakuwa kati yao kama ndugu yao katika imani, ili kuwasaidia kulipenyeza Neno la Mungu katika undani wa maisha yao.

Lengo ni kuwawezesha kuonja: upendo, huruma na msamaha kama ulivyofunuliwa na Kristo Yesu, ili kuupokea na kuweza kuuishi kikamilifu na kwamba, utimilifu wake utafikia siku moja kule mbinguni! Ratiba elekezi inaonesha kwamba, wakati wote wa mafungo kutakuwepo na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu ili kutoa nafasi kwa wahusika kwenye mafungo kuweza kuzungumza na Kristo wa Ekaristi. Masifu ya Asubuhi, Tafakari, Ibada ya Misa Takatifu na Masifu ya Jioni. Radio Vatican itaendelea kukushirikisha kwa muhtasari yale yatakayokuwa yanaendelea kujiri katika mafungo haya, ili hata wewe uweze kuonja raha ya kupanda mlimani kwa Bwana!

Mafungo ya Kiroho
29 February 2020, 17:11