Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 26 Februari 2020, Jumatano ya Majivu, Mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2020 ataongoza Ibada ya Misa Takatifu. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 26 Februari 2020, Jumatano ya Majivu, Mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2020 ataongoza Ibada ya Misa Takatifu. 

Maadhimisho ya Jumatano ya Majivu, 2020 mjini Vatican

Baba Mtakatifu anasema, Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ndicho kiini cha toba na wongofu wa ndani. Utambulisho makini wa waamini. Mama Kanisa anakianza Kipindi cha Kwaresima kinachosimikwa katika misingi ya toba na wongofu wa ndani; sala, tafakari na matendo ya huruma kwa kupakwa majivu, kielelezo cha toba ya ndani

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2020 unaongozwa na kauli mbiu “Twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: Mpatanishwe na Mungu.” 2 Kor. 5:20. Baba Mtakatifu anasema, Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ndicho kiini cha toba na wongofu wa ndani, unaowawezesha waamini kumgusa Kristo Yesu kwa njia ya imani, kwa wale wote wanaoteseka. Mama Kanisa anakianza Kipindi cha Kwaresima kinachosimikwa katika misingi ya toba na wongofu wa ndani; sala, tafakari na matendo ya huruma kwa kupakwa majivu, kielelezo cha toba ya ndani!

Katika maadhimisho ya Jumatano ya Majivu, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Anselmi, Jimbo kuu la Roma. Ibada hii itaanza saa 10:30 jioni kwa saa za Ulaya na baadaye kutafuatia maandamano kuelekea kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Sabina. Maandamano haya yanawashirikisha Makardinali, Maaskofu, Mapadre, Watawa na waamini walei, kielelezo cha hija ya toba na wongofu wa ndani tayari kuanza maandalizi ya kushiriki maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Watakapowasili kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Sabina, Baba Mtakatifu atabariki majivu na hatimaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Itakumbukwa kwamba, hija hii inafanywa kwenye Makanisa ambayo yanahifadhi masalia ya watakatifu na wafiadini, walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni fursa ya kupyaisha tena imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake, ili hata wakristo wa nyakati hizi, waweze kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa.

Taarifa inabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 27 Februari 2020 ataongoza Ibada ya Upatanisho, mwanzoni mwa Kipindi cha Kwaresima kwa wakleri wa Jimbo kuu la Roma. Kardinali Angelo De Donatis, atato tafakari na baada ya hapo, wakleri wataingia kwenye “Mahakama ya toba na huruma ya Mungu” kwa kuungama dhambi zao. Kama kawaida, Baba Mtakatifu atatumia fursa hii pia kujipatanisha na Mungu na baadaye, atawaungamisha wakleri kadhaa. Mwishoni, atawapatia Neno na kitabu kwa ajili ya tafakari ya Kipindi cha Kwaresima. Radio Vatican daima, imejipanga kikamilifu ili kuhakikisha kwamba, inakujuza yale yote yatakayojiri katika kipindi hiki cha Kwaresima.

Papa: Ibada ya Jumatano ya Majivu 2020

 

25 February 2020, 17:26