Jumuiya ya Kiekumene ya Taize inaadhimisha Siku ya 42 ya maadhimisho hayo huko mjini Wroclaw, nchini Poland: Ushuhuda wa imani. Jumuiya ya Kiekumene ya Taize inaadhimisha Siku ya 42 ya maadhimisho hayo huko mjini Wroclaw, nchini Poland: Ushuhuda wa imani. 

Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè: 28 Desemba-1 Januari 2020: Imani!

Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè inasema kwamba, Siku ya 42 ya Vijana wa Kiekumene Barani Ulaya inazinduliwa rasmi tarehe 28 Desemba 2019 hadi tarehe Mosi, Januari 2020 huko mjini Wroclaw, nchini Poland. Na hii itakuwa ni mara ya tatu kwa mji wa Wrocław, baada ya maadhimisho yaliyofanyika kunako mwaka 1989 na 1995. Lakini hii ni safari ya tano kwa Poland kuwa mwenyeji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Machi 2019 akiwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto, aliweka sahihi kwenye Wosia wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”. Wosia huu umezinduliwa rasmi, tarehe 2 Aprili 2019. Wosia huu ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa Mwaka 2018, yaliyoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Mang’amuzi na Miito”. Huu pia ni mwendelezo wa mchakato wa Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia, kwani utume wa Kanisa kwa familia na vijana ni sawa na chanda na pete; unategemeana na kukamilishana! Sura ya nne ni mbiu kwa vijana wote kwamba, “Mungu ni upendo”, Kristo Yesu anaokoa na kwamba, yu hai kabisa na kwa njia ya Roho Mtakatifu, vijana wanaweza kuboresha maisha yao. Sura ya tano inaonesha mapito ya ujana katika makuzi na ukomavu; vijana wanaojisadaka na kujitosa kwa ajili ya huduma kwa jirani zao. Vijana wanakumbushwa kwamba, wanaitwa na kutumwa kama wamisionari jasiri, ili kutangaza na kushuhudia Injili kwa njia ya maisha yao katika ukweli, hii ni changamoto kwa vijana wote!

Sura ya sita, inawaonesha vijana waliokita mizizi yao katika mambo msingi ya maisha. Hawa ni wale vijana wenye uwezo wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na wazee; ili kumwilisha ndoto na maono, ili kwa pamoja, wazee na vijana waweze kuonesha uthubutu wao katika maisha. Sura ya saba ni kuhusu utume wa Kanisa kwa vijana, kwa kuwasindikiza na kuwaongoza, wao wenyewe wakionesha kipaji cha ubunifu. Mkazo katika utume kwa vijana: tafiti na ukuaji! Kanisa linapaswa kujenga mazingira yatakayosaidia kumwilisha vipaumbele hivi. Kanisa pia linapaswa kuwekeza zaidi katika utume wa vijana kwenye taasisi za elimu na vyuo vikuu; kwa kuendesha pia utume wa vijana katika “vijiwe vya vijana” ili kuwatafuta na kuwaendea huko huko waliko, daima kwa kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu. Daima vijana wakumbuke kwamba, wao ni wamisionari, kumbe, utume kwa vijana unapaswa kujikita katika umisionari, huku vijana hawa wakiwa wanasindikizwa na watu wazima na wakomavu, ili kujitambua na kwamba, wanapaswa kutembea bega kwa bega, huku wakiheshimu na kuthamini uhuru wao!

Fra Alois, Mkuu wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè anasema kwamba, Siku ya 42 ya Vijana wa Kiekumene Barani Ulaya inazinduliwa rasmi tarehe 28 Desemba 2019 hadi tarehe Mosi, Januari 2020 huko mjini Wroclaw, nchini Poland. Na hii itakuwa ni mara ya tatu kwa mji wa Wrocław, baada ya maadhimisho yaliyofanyika kunako mwaka 1989 na 1995. Lakini hii ni safari ya tano kwa Poland kuwa mwenyeji wa Siku ya Vijana wa Kiekumene Barani Ulaya. Hizi ni nyakati muhimu sana za maisha na utume wa Kanisa kwa vijana, zinazofumbatwa katika maisha ya sala, tafakari, katekesi, ibada pamoja na ujenzi wa madaraja ya vijana kukutana, ili kuaminiana na kuthaminiana katika maisha yao, licha ya tofauti zao msingi. Ni tukio linalowawezesha vijana kukutana na mashuhuda wa imani kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya.

Ni katika mukadha huu wa utume wa Kanisa kwa vijana, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anapenda kuwatakia heri na baraka vijana wote wanaoshiriki katika maadhimisho haya ambayo kwa mara ya tano yanaadhimishwa nchini Poland, mahali alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II, muasisi wa Maadhimisho ya Siku za Vijana Ulimwenguni. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia uwepo wake kwa njia ya sala na sadaka yake, ili kweli vijana “waendelee kujikita katika njia ya imani na kamwe wasing’olewe huko”, kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya huko nchini Poland. Waamini nchini Poland wamekumbana na changamoto mbali mbali katika maisha ya imani, lakini wakathubutu kusimama kidete na kujikita katika matumaini hata pale ambapo matumaini yalionekana kana kwamba yanatoweka.

Vijana wanayo mengi ya kujifunza kutoka kwa waamini ambao licha ya patashika nguo kuchanika, wameendelea kusimama imara katika imani, wakiwa na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi. Imani thabiti iwasaidie vijana kukutana na vijana wenzao, wakiwa tayari kupambana na changamoto mamboleo, hususan juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Bado kuna mizizi ya imani inayopaswa kumwilishwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko hata katika ulimwengu mamboleo, kama njia ya kujibu kikamilifu changamoto mamboleo. Kwa kukutana na vijana wenzao, watagundua umuhimu wa kutoka na kwenda kushiriki katika tukio hili kama ilivyokuwa kwa Ibrahim, Baba wa imani. Vijana wanapaswa kuwa tayari daima ili kuandika kurasa mpya za maisha yao kwa njia ya ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili, kwa kuwa na mvuto kwa wale wote wanaowazunguka. Kwa hakika, vijana wanapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha na matumaini kwa watu waliokata tamaa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Vijana wanapaswa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa “Leo ya Mungu katika maisha yao” kwa kutumia vyema nguvu na kipaji chao cha ubunifu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa vijana wote wanaoshiriki katika mkutano huu pamoja na familia zote ambazo zimekubali kuwapokea na kuwaonjesha ukarimu. Anawaweka wote hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, aliyeondoka kwa haraka, ili aendelee kuwatia shime katika kuenzi imani kwa Kristo Yesu!

Vijana: Poland
27 December 2019, 15:36