Tafuta

Mahubiri ya Kipindi cha Majilio Mwaka 2019: Utenzi wa Bikira Maria ni shule ya uinjilishaji, toba na wongofu wa ndani. Mahubiri ya Kipindi cha Majilio Mwaka 2019: Utenzi wa Bikira Maria ni shule ya uinjilishaji, toba na wongofu wa ndani. 

Utenzi wa Bikira Maria: Magnificat: Ni shule ya uinjilishaji, toba na wongofu wa ndani

Padre Raniero Cantalamessa katika mahubiri ya Pili ya Kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2019 amefafanua kwa kina na mapana maana ya Utenzi wa Utenzi wa Bikira Maria "Magnificat" kuwa ni mtazamo mpya kuhusu ulimwengu na historia. Ni shule ya uinjilishaji kama wanavyofafanua Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Ni shule ya toba na wongofu wa ndani! Magnificat!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya Kipapa katika kipindi cha Majilio anasema, anapenda kuwaandaa waamini kuadhimisha Sherehe ya Noeli kwa mwaka 2019, wakiwa wanasindikizwa na tafakari ya kina kuhusu Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa mintarafu matendo ya furaha kama yanavyotafakariwa kwenye Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya ukombozi. “Wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye” Mt. 2:11. Hii ndiyo kauli mbiu inayoongoza tafakari za Kipindi cha Majilio kwa Mwaka huu. Utenzi wa Bikira Maria, ni mtazamo mpya kuhusu Mwenyezi Mungu na ulimwengu. Ni utenzi wa toba na wongofu wa ndani unaowahimiza waamini kujenga na kudumisha utamaduni unaomwilisha huruma na upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha. Utenzi wa “Magnificat” una mwelekea Mwenyezi Mungu,  ambaye ni mkuu, mwingi wa huruma na mapendo, mtakatifu na enzi zote ni zake na kwamba, huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi.

Utenzi wa Bikira Maria ndiyo mada iliyoongoza tafakari ya Pili ya Kipindi cha Majilio, iliyotolewa na Padre Raniero Cantalamessa, Ijumaa tarehe 13 Desemba 2019, kilele cha Jubilei ya Miaka 50 tangu Baba Mtakatifu Francisko alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, hapo tarehe 13 Desemba 1969. Tafakari hii ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei hii ambayo inatajirishwa pia na Wimbo wa Zakaria “Benedictus:Canticum Zachariae” pamoja na utenzi wa shukrani kutoka kwa Mzee Simeoni “Nunc dimittis”. Matukio yote haya ni ushuhuda wa imani inayoadhimishwa na Mama Kanisa katika Liturujia kama sehemu ya matukio ya safari ya wokovu. Licha ya tafiti mbali mbali za Sayansi ya Maandiko Matakatifu kusigana kuhusu: watunzi, asili na muundo wake, lakini Mwinjili Luka alipenda kuweza tenzi hizi kama sehemu ya Injili, yaani Neno la Mungu kwa vile limeandikwa kwa uvuvio wa Roho wa Mungu.

Utenzi wa Bikira Maria, ni mtazamo mpya kuhusu Mwenyezi Mungu na ulimwengu katika ujumla wake. Hii ni shule ya uinjilishaji, toba na wongofu wa ndani unaowahimiza waamini kujenga na kudumisha utamaduni unaomwilisha huruma na upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha. Utenzi wa “Magnificat” unatoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu,  ambaye ni: Bwana na Mkuu: ni mwingi wa huruma na mapendo; ni mtakatifu na enzi zote ni zake na kwamba, huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi. Huruma yake ni sawa na mto unaoendelea “kurutubisha” historia ya mwanadamu. Ni Mungu ambaye ameutazama unyonge wa mjakazi wake, kiasi cha kumkirimia neema na baraka, mambo ambayo ameyapokea kwa moyo wa unyenyekevu. Ndiyo maana roho yake inamfurahia Mungu mwokozi wake kwa sababu amemuumba, akampenda na kumkomboa na kwa njia ya utenzi huu, anataka kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo, uzuri na umilele kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni kilele cha furaha yote ya mwanadamu.

Mtakatifu Bonaventure anasema, Bikira Maria alipopashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu, alisafishwa na kutakaswa zaidi na hiki ndicho kiini cha furaha yake iliyopelekea hata kumwimbia Mwenyezi Mungu “Magnificat”. Utenzi huu ni ushuhuda wa imani kutoka kwa Bikira Maria na unaweza pia kuonekana katika Jumuiya inayosherehekea na kuadhimisha matendo makuu ya Mungu katika maisha. Padre Raniero Cantalamessa anasema, utenzi wa Bikira Maria, ni mtazamo mpya kuhusu ulimwengu na historia katika ujumla wake kama kielelezo cha ufunuo wa Mungu na uwepo wake wa daima kwa sababu amefanya nguvu kwa mkono wake, amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao, amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi. Hawa ndio akina Mfalme Herode ambao walitisha na kutikisa dunia enzi zao, kiasi hata cha Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Mtakatifu Yosefu kulazimika kukimbilia Misri ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu. Lakini Mwenyezi Mungu akawakweza wanyonge. Huu ni utajiri unaopata chimbuko la kibali chake machoni pa Mungu pamoja kwa kuonesha pia ubora wa maisha ya ufukara.

Utenzi wa Bikira Maria ni shule ya uinjilishaji kama wanavyofafanua Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwamba, Bikira Maria na Mama, ni mfano mtimilifu wa Kanisa katika misingi ya imani, mapendo na umoja kamili na Kristo Yesu. Mtakatifu Ambrosi anasema kwa maana katika Fumbo la Kanisa ambalo pia laitwa kwa haki mama na bikira, Bikira Maria ametangulia kwa njia bora ya pekee kutoa mfano wa kuwa bikira na mama. Katika utenzi huu, Kanisa linakumbushwa kwamba, linaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Linapaswa kuwa ni sauti ya kinabii, chemchemi ya imani na kwamba, ni wajibu wake msingi wa kushughulikia haki, amani na masuala ya kijamii mintarafu Sheria ya Mungu na upendo kwa jirani. Utenzi wa Bikira Maria ni onyo kwa wenye mamlaka na matajiri, kutubu na kumwongokea Mungu kwa kutumia fursa zao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kanisa linapaswa kuunganisha nguvu zake na watu wenye mapenzi mema ili kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Kanisa linapaswa kuwa kweli ni sauti ya kinabii ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo. Linapaswa kutangaza na kusimamia ukweli, maadili na utu wema. Bikira Maria ni shuhuda wa utajiri unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kuwa kweli ni sauti ya kinabii. Kwa hakika, Bikira Maria ni nyota ya uinjilishaji. Padre Raniero Cantalamessa anaendelea kufafanua kwamba, utenzi wa Bikira Maria ni shule ya toba na wongofu wa ndani kwa sababu Mwenyezi Mungu amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao. Bikira Maria anakazia ukweli na haki na kwamba, vita, kinzani na mapigano yanayosikika sehemu mbali mbali za dunia ni matokeo ya uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka. Lakini wenye njaa wameshibishwa mema na wenye mali amewaondoa mikono mitupu!

Kanisa halina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utenzi wa Bikira Maria ni shule ya ajabu sana inayofumbata hekima ya Kiinjili, chachu ya toba na wongofu wa ndani. Kwa hakika, Bikira Maria ni kielelezo na mfano bora wa imani tendaji na anaendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kama ambayo Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 13 Desemba 2019 alivyomwimbia Mungu utenzi wa shukrani kwa kuadhimisha kilele cha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Cantalamessa
13 December 2019, 17:33