Tafuta

Vatican News
Shirika la Wamisionari wa Consolata, tarehe 22 Desemba 2019 limepata Mashemasi watano wa mpito! Shirika la Wamisionari wa Consolata, tarehe 22 Desemba 2019 limepata Mashemasi watano wa mpito! 

Shirika la Wamisionari wa Consolata lapata Mashemasi wapya watano! Huduma!

Ushemasi ni ngazi ya kwanza ya Sakramenti ya Daraja Takatifu ambayo kwayo Mama Kanisa Mtakatifu anajipatia wahudumu wa Liturujia, Neno la Mungu na huduma ya upendo kwa watu hasa maskini na wanyonge. Mashemasi wanaitwa kutolea maisha yao kuwa chachu ya utakatifu katika ushuhuda na mfano thabiti wa sala, kujitoa katika utii na kujitolea kwa upendo kwa taifa la Mungu.

Karoli Joseph Amani, - Vatican.

Shirika la Wamisionari wa Consolata, linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya maisha, uwepo na utume wake nchini Tanzania na kilele chake kilikuwa ni hapo tarehe 14 Oktoba 2019, Kanisa nchini Tanzania lilipomwimbia Mwenyezi Mungu, utenzi wa sifa na shukrani, kwa kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Waconsolata wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Faraja kwa watu wa Mungu nchini Tanzania. Mwenyeheri Joseph Allamano katika maisha yake, alibahatika kuwa ni: mwalimu, mtume na kiongozi wa maisha ya kiroho. Katika shughuli za kitume, alikazia kwa namna ya pekee mambo makuu mawili: Mosi, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, yaani: Kuhubiri, ili watu waweze kumfahamu Mwenyezi Mungu aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu na hivyo kuwa ni faraja ya watu wa Mungu.

Pili, ilikuwa ni muhimu sana kusoma alama za nyakati, kwa kuangalia maisha ya watu, ili kujizatiti katika mchakato wa kuinua: utu na heshima yao kwa kuwapatia huduma yenye kutukuka. Lengo ni kuinua hali ya maisha ya watu wanaowahudumia, ili hatimaye, waweze kupata utimilifu wa maisha. Ni katika muktadha huu, Wamisionari wa Consolata katika kipindi cha miaka 100 iliyopita, katika maisha na utume wao, wamejielekeza zaidi katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni Shirika ambalo limejikita katika mchakato wa malezi na majiundo ya kimisionari, ili kuwaandaa wamisionari watakaoendeleza utume huu sehemu mbali mbali za dunia kama mashuhuda na watangazaji wa Injili. Ushemasi ni ngazi ya kwanza ya Sakramenti ya Daraja Takatifu ambayo kwayo Mama Kanisa Mtakatifu anajipatia wahudumu wa Liturujia, Neno la Mungu na huduma ya upendo kwa watu hasa maskini na wanyonge.

Mashemasi wanaitwa kutolea maisha yao kuwa chachu ya utakatifu katika ushuhuda na mfano thabiti wa sala, kujitoa katika utii na kujitolea kwa upendo kwa taifa la Mungu hususan kwa wanyonge na wasio na watetezi. Kwa kuwekewa mikono na sala ya kuwekwa wakfu, mashemasi wanafanywa kuwa watumishi katika Kanisa wakipewa dhamana ya kufanya shughuli za kuwatangazia watu Neno la Mungu hususan kuhubiri katika maadhimisho ya liturujia, kuadhimisha Sakramenti za ubatizo na ndoa, kutunza na kuwapatia wakristo Ekaristi takatifu, kuwapelekea wagongwa komunyo Takatifu na kuwazika wafu (Lumen Gentium 29). Jumapili tarehe 22 Desemba 2019 Kardinali Giuseppe Bertello Rais wa mji wa Vatican ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Parokia ya Mtakatifu Julio, Jimbo kuu la Roma na kutoa Daraja ya Ushemasi kwa majandokasisi watano wa Shirika la Wamisionari wa Consolata, ambao ni Eugenio Teresa (Msumbiji), Mathew Gaithan Kilamlya (Tanzania),  John Kinyua Nkinga (Kenya), Patrick Mandondo Fwakongo (Jamhuri ya Kimekrasia Congo) na Felix Mutinda Mulwa (Msumbiji).

Katika mahubiri yake Kardinali Bertello alitilia mkazo suala la wito akisema kwamba, tangu Agano la Kale Mwenyezi Mungu anawachagua wale anaowataka, akawateuwa kuwa wajumbe wake. Katika Injili ya Domenika ya Nne ya Majilio, Mtakatifu Yosefu mtu wa haki aliteuliwa kuwa mjumbe wa Mungu katika mpango wa Ukombozi. Mtakatifu Paulo, Mwalimu na mtume wa Mataifa anatambua wazi kwamba, ameitwa na Mungu. Kumbe wito ni  kwa wote lakini kwa namna ya pekee, ushemasi ni zawadi ya Mungu kwa ajili ya huduma. Akidadavua kuhusu Liturujia ya Daraja ya Ushemasi, Kardinali Bertello amewakumbusha wateule kwamba tendo la Kuwakabidhi Kitabu cha Injili ambayo wao wanafanyika watangazaji wa Neno la Mungu, liwabidiishe kuifanya Injili kuwa sera na mkakati wa maisha yao yote. Aidha, Kitendo cha kulala kifudifudi huku wengine wote wakiungana kuwaombea kwa Litania ya watakatifu; ni ishara ya kujitoa bila kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake, katika utii na unyenyekevu wa moyo kwa ajili ya huduma ya Kanisa. Walioitwa na Mungu katika umisionari wanapaswa kuwa tayari kutolea yote, hata ikipasa uhai wao kwa ajili ya kulitangaza Neno la Mungu.

Kardinali Bertello alikazia kwamba, Mashemasi wanaapa kuchukua wajibu wa kusali Sala ya Kanisa. Kwa kiapo hicho wanakabidhiwa wajibu ambao ndani yake Mungu anawapa upendeleo wa kuwa waombezi wa Kanisa na taifa lake lote ili wamtolee sifa na utukufu. Hivyo, wanapaswa kujizoesha kukua katika mapendo na Mungu wakijuvia katika sala. Aliwaasa mashemasi wapya kufuasa mfano wa mwanzilishi wao Mwenyeheri Yosefu Alamano, kuishi wito wao wa kimisionari wakijikabidhi daima katika tunza ya mama Bikira Maria Mlinzi na mwombezi wa Shirika la Wamisionari wakonsolata.  Ndugu, jamaa na marafiki wa mashemasi wapya, waliungana na familia ya wamisionari Waconsolata kumshukuru Mungu, kuwapongeza, kuwaombea na kuwaunga mkono wamisionari hawa jasiri, ili wajae shime na ari ya kimisionari kuendelea kuumbiza mwenge wa uinjilishaji kokote watakapokuwa.

Mashemasi

 

24 December 2019, 15:41