Kardinali Pietro Parolin, tarehe 17 Desemba 2019 ametembelea Gereza la Milano-Opera lenye ulinzi mkali kama ushuhuda wa upendo na mshikamano kutoka kwa Papa Francisko. Kardinali Pietro Parolin, tarehe 17 Desemba 2019 ametembelea Gereza la Milano-Opera lenye ulinzi mkali kama ushuhuda wa upendo na mshikamano kutoka kwa Papa Francisko. 

Sherehe ya Noeli: Mshikamano na wafungwa magerezani: utu wao!

Kanisa linasherehekea Noeli ya Kristo Yesu, ambaye amependa kuwa kati pamoja na waja wake, ili kupyaisha matumaini. Fumbo la Noeli ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu. Kardinali Parolin amezindua kwenye Gereza la Milano-Opera kitengo cha kutengeneza Hostia kwa ajili ya mahitaji ya Kanisa ndani na nje ya Italia. Huu ni mradi wa kwanza kuwahi kutekelezwa nchini Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Gereza ni mahali pa mahangaiko ya ndani ya binadamu. Askari magereza wanatumia muda mrefu kuwa magerezani, ili kulinda na kudumisha ulinzi na usalama, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa barabara. Askari magereza wawe ni walinzi wa ndugu zao wafungwa, wawe ni madaraja kati ya magereza na jamii katika ujumla wake, kwa kuonesha upendo unaowawajibisha, ili kuondoa wasi wasi na kashfa ya kutowajali wengine. Baba Mtakatifu Francisko anawataka askari magereza kutambua uzito wa kazi na wajibu wao kwa wafungwa pamoja na familia zao wenyewe. Kumbe, inawapaswa kusaidiana na kushikamana ili kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa zinazopatikana kutokana na kazi yao. Ni katika muktadha huu wa upendo na mshikamano wa dhati kwa wafungwa na askari magereza, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumanne, tarehe 17 Desemba 2019 ametembelea Gereza la Milano-Opera, lenye ulinzi mkali sana nchini Italia, linalotoa hifadhi kwa wafungwa 1, 400.

Akiwa ameandamana na viongozi wakuu wa gereza hili, Kardinali Parolin, ametembelea gereza hilo na kuzungumza na baadhi ya wafungwa kama kielelezo cha upendo na mshikamano wa Baba Mtakatifu Francisko katika maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2019. Kardinali Parolin, ametembelea vitengo mbali mbali vya uzalishaji gerezani hapo na kwa namna ya pekee, kwenye kitengo kinachotengeneza Hostia kwa ajili ya matumizi ya Parokia mbali mbali ndani na nje ya Italia. Kitengo hili kilianza uzalishaji wake kunako mwaka 2016. Kwa kazi ya mikono yao, wanawawezesha waamini kushiriki vyema Fumbo la Ekaristi Takatifu na kwa wafungwa wenyewe ni fursa ya kuendeleza mchakato wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza upya hija ya maisha yao wakiwa ni watu wapya zaidi kuliko walivyoingia gerezani. Utengenezaji wa Hostia imekuwa ni kazi maalum kwa wafungwa wa zamani, wanawake waliokombolewa kutoka katika mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo pamoja na vijana wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.

Kardinali Parolin, amepata nafasi ya kusali pamoja na wafungwa na askari magereza kwa kukazia kwamba, Noeli ni muda muafaka wa kupyaisha tena imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Kardinali Parolin amewatakia heri na baraka katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2019 na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko daima anawakumbuka na kuwaombea katika sala na sadaka yake, ili kwamba, wanapotoka magerezani waweze kuwa ni watu wapya zaidi. Kanisa linasherehekea Noeli ya Kristo Yesu, ambaye amependa kuwa kati pamoja na waja wake, ili kupyaisha matumaini. Fumbo la Noeli ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Kardinali amezindua kwenye Gereza la Milano-Opera kitengo cha kutengeneza Hostia kwa ajili ya mahitaji ya Kanisa ndani na nje ya Italia. Huu ni mradi wa kwanza kuwahi kutekelezwa na magereza ya Italia. Mradi utasimamiwa na wanawake wakimbizi na wahamiaji wanaotoka katika maeneo ya vita, ghasia na dhuluma.

Kumbe, mradi huu ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja na mafungamano ya kijamii; kwa kuwasaidia wanawake kupyaisha matumaini yao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Hiki ni kielelezo makini cha kusikiliza na kujibu kilio cha maskini kwa njia ya mshikamano wa upendo. Baba Mtakatifu Francisko kuhusu magereza anapenda kukazia kwa namna ya pekee kabisa: Umuhimu wa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wafungwa magerezani,  kwa kutambua kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa Injili sanjari na kuwa na ujasiri wanapotekeleza dhamana na utume wao miongoni mwa wafungwa. Baba Mtakatifu anawapongeza Askari magereza kila wakati wanapotekeleza dhamana na utume wao kwa ajili ya ulinzi na usalama kwa maskini na wanyonge zaidi katika jamii, yaani wafungwa, ili kuhakikisha kwamba, haki, amani, ulinzi na usalama vinatawala ndani ya jamii. Hii ni dhamana inayowataka Askari magereza siku kwa siku kuwa ni wajenzi wa haki na wajumbe wa amani kwa kuwakumbuka wafungwa hao waliofungwa kana kwamba, wamefungwa pamoja nao na kama wanadhulumiwa, basi hata wao wahisi haya madhulumu mwilini wao.

Kufurika kwa wafungwa magerezani nchini Italia ni kati ya changamoto changamani kwa wakati huu, hali ambayo inachangia pia kudhohofisha maisha ya Askari magereza, kiasi hata cha kukosa imani. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, wafanyakazi na wafungwa wanaishi maisha yenye hadhi na utu wa kibinadamu, vinginevyo, magereza yatageuka kuwa nyumba za chuki na uhasama badala ya kuwa ni mahali pa kurekebisha tabia na mwenendo wa wafungwa. Baba Mtakatifu Francisko anawataka wadau wa huduma mbali mbali magerezani kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili, tayari kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza. Wanapokumbana na umaskini wa wafungwa magerezani, watambue kwamba, hawa ni watu wanaohitaji kwanza kabisa msamaha na huruma ya Mungu. Wawe na ujasiri wa kusamehe kama mashuhuda waaminifu wa msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu; wawe ni watu wa faraja na kamwe wasimwache mtu hata mmoja kutumbukia katika upweke hasi, unaoweza kusababisha watu kumezwa na utamaduni wa kifo.

Magereza

 

 

19 December 2019, 11:13