Papa Francisko tarehe 13 Desemba 2019 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipooewa Daraja Takatifu ya Upadre. Amepokea salam na matashi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Papa Francisko tarehe 13 Desemba 2019 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipooewa Daraja Takatifu ya Upadre. Amepokea salam na matashi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia. 

Papa Francisko: Miaka 50 ya Daraja Takatifu: Salam na matashi mema!

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake amejipambanua kwa kusimama kidete katika mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho; utunzaji bora wa mazingira na mapambano dhidi ya umaskini ili kulinda na kudumisha misingi ya: utu, heshima, haki, amani na maridhiano; mambo yanayokita mizizi yake katika ukweli na uwazi, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, linapenda kuungana na watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa ajili ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, shukrani na masifu, kwa ajili ya Baba Mtakatifu Francisko anayeadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 13 Desemba 1969. Baba Mtakatifu Francisko alizaliwa tarehe 17 Desemba 1936 huko Flores, Buenos Aires, nchini Argentina. Mwaka 2019 anatimiza miaka 83 tangu alipozaliwa. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 13 Desemba 1969 akapewa Daraja Takatifu  ya Upadre. Kunako mwaka 1992 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu hapo tarehe 27 Juni 1992. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali tarehe 21 Februari 2001.

Tarehe 13 Machi 2013 akaanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ndiyo siri ya zawadi na fumbo la Daraja Takatifu ya Upadre linalomwezesha Baba Mtakatifu kuwa ni Kristo mwingine, “Alter Christus” kwa njia ya Daraja Takatifu ya Upadre. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amejipambanua kwa kusimama kidete katika mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na mapambano dhidi ya umaskini ili kulinda na kudumisha misingi ya: utu, heshima, haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa mambo yanayokita mizizi yake katika ukweli na uwazi, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi.

CELAM inasema, Baba Mtakatifu kwa hakika amekuwa ni shuhuda wa Injili ya matumaini kwa wale waliokata tamaa kwa kuwakumbusha kwamba, watu wote wanaweza kuonja na kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. CELAM inapenda kumsindikiza Baba Mtakatifu kwa sala na sadaka yake, ili kweli Nyota ya Mtoto Yesu iendelee kung’ara kati ya watu wa Mataifa na kufukuzia mbali giza la vita, kinzani na utengano kati ya watu ili hatimaye, kujenga utamaduni na madaraka yanayowakutanisha watu ili kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu! CELAM inataka kuhakikishia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, inaendelea kufuatilia kwa karibu sana mafundisho yake kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, haki na amani pamoja na kuendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Kwa upandce wake, Kardinali Gualtiero Bassetti, kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, anapenda kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko, anayeendelea kuwakumbusha watu wa Mungu, kuishi utume wao kama sehemu ya mchakato wa huduma kwa Mungu pamoja na watu wake kama kielelezo cha upendo na unyenyekevu, bila kukata tamaa hata kama kuna mafuriko ya changamoto na shida mbali mbali za maisha. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, kama sehemu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linamshukuru Baba Mtakatifu kwa kuendelea kuwa ni shuhuda wa Injili ya huruma, matumaini na furaha; daima amekuwa tayari kutafakari pamoja na kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Kwa hakika, Baba Mtakatifu anaendelea kuwa ni mfano wa Msamaria mwema anayeendelea kuwaganga watu wa Mungu kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini.

CELAM na CEI

 

 

13 December 2019, 16:31