Mahibiri ya Kipindi cha Majilio 2019: Kauli mbiu: Wakamwona Mtoto Pamoja na Mariamu Mamaye! Bikira Maria ni mfano wa imani, matumaini na mapendo! Mahibiri ya Kipindi cha Majilio 2019: Kauli mbiu: Wakamwona Mtoto Pamoja na Mariamu Mamaye! Bikira Maria ni mfano wa imani, matumaini na mapendo! 

Mahubiri ya Kipindi cha Majilio 2019: Bikira Maria Mama wa Mungu

Padre Raniero Cantalamessa, anapenda kuwaandaa waamini kuadhimisha Sherehe ya Noeli, wakiwa wanasindikizwa na Bikira Maria, Mama wa Mungu. Tarehe 6 Desemba 2019, tafakari ya kwanza: “Malaika Gabrieli anampasha habari Maria kuwa atakuwa Mama wa Mungu. Tema ya pili ni: Maria Mtakatifu anakwenda kumtembelea Elizabeti. Tema ya tatu ni: Yesu anazaliwa Bethlehemu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Mwaka wa Liturujia, Kanisa linaadhimisha Fumbo lote la Kristo Yesu, tangu Umwilisho hadi kurudi kwake kwa utukufu ili kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Kipindi cha Majilio ni nafasi kwa waamini kulitafakari kwa namna ya pekee, Fumbo la Umwilisho, Yesu alipozaliwa kwa mara ya kwanza katika historia na maisha ya mwanadamu. Hiki ni kipindi cha subira, imani na matumaini yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini. Majilio ni kipindi kinachomwandaa mwamini kuadhimisha vyema Fumbo la Umwilisho. Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu ni chemchemi ya matumaini, imani na furaha; tema muhimu sana wakati wa Kipindi cha Majilio na waamini wanaongozwa kwa namna ya pekee na tafakari kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, matumaini yameingia ulimwenguni kama Nabii Isaya anavyosema, tazama Bikira atachukua mimba na kumzaa mtoto atakayeitwa Emmanueli.

Mwenyezi Mungu ametekeleza ahadi yake kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili na kukaa kati ya watu wake, ili kuwaonesha mshikamano na wala hakuona kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kung’angania sana, kielelezo makini cha unyenyekevu na uaminifu unaofungua Ufalme wa mbinguni na kuwakirimia wanadamu matumaini mapya: yaani maisha ya uzima wa milele! Wakristo wakiangazwa na Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, wanaweza kuwaandaa walimwengu kwa ajili ya ujio wa Mkombozi. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kujiandaa kwa sala, tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa ajili ya ujio wa Kristo Yesu, Mkombozi na Masiha. Wahusika wakuu katika kipindi cha Majilio ni: Nabii Isaya, Yohane Mbatizaji, Zakaria na mkewe Elizabeth Wengine wanaopamba kipindi hiki ni: wachungaji wa kondeni, Mamajusi, watu wa kawaida lakini kwa namna ya pekee, Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu. Hawa wawe ni mifano bora ya kuigwa katika kipindi hiki cha Majilio! Hawa ni wale walioguswa kwa namna ya pekee na maandalizi ya ujio wa Masiha.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “ADMIRABILE SIGNUM” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli”, anasema Pango la Noeli ni mahali pa kusimama, kutafakari na kusali katika ukimya. Kunahitajika kimya kikuu ili kuutafakari uzuri wa Uso wa Mtoto Yesu ambaye amelazwa kwenye hori ya kulishia wanyama. Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai akazaliwa katika hali ya umaskini wa kutupwa. Sala mbele ya Pango la Noeli ni kielelezo cha moyo wa shukrani na mshangao mkubwa mbele ya zawadi kubwa ya upendo ambayo Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake. Katika Pango la Noeli, Ishara ya kushangaza, waamini wamejenga na kudumisha Ibada ambayo wameirithisha kwa kizazi baada ya kizazi. Ibada hii inakita mizizi yake katika: imani, matumaini na mapendo katika Fumbo la Umwilisho, ambalo ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa binadamu na kwa binadamu na maisha yake.

Mwenyezi Mungu katika busara na hekima yake ya Kibaba, ameamua kutembea bega kwa bega na watoto wake kwa njia ya uwepo wake, usionekana kwa macho makavu, lakini unaonekana kwa imani, katika nyakati za furaha au nyakati za mateso na machungu ya maisha. Yeye ni Emmanueli yaani Mungu pamoja nasi! Kama ilivyokuwa kwa wachungaji kule kondeni mjini Bethelehemu, hata katika ulimwengu mamboleo, waamini wanahimizwa kuupokea wito na mwaliko wa kwenda mjini Bethelehemu kuona na kutambua “Signum” yaani “Ishara” ambayo wamepewa na Mwenyezi Mungu. Ni katika muktadha huu anasema Baba Mtakatifu Francisko kwamba, nyoyo za waamini zitaweza kusheheni furaha na hata kuweza kuipeleka mahali ambapo kuna majonzi;  kwani hapo patajazwa matumaini pamoja na kushirikiana na wale ambao wamepokonywa fadhila ya matumaini katika maisha yao.

Kipindi cha Majilio, kiwe ni msaada kwa waamini kujivika utu mpya kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, Neno la Mungu na Matendo ya huruma kwa jirani. Waamini wajiandae kikamilifu wasijikute wanafikiwa na Kristo Yesu huku wakiwa bado wamemezwa na malimwengu. Waamini waandae mioyo na familia zao, ili Kristo Yesu aweze kuzaliwa katika mazingira ya: Imani, Mapendo na Matumaini; Amani na mshikamano wa dhati kwa maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii: kiroho na kimwili. “Wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye” Mt. 2:11. Hii ndiyo kauli mbiu inayoongoza tafakari za Kipindi cha Majilio zinazotolea na Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri wa nyumba ya Kipapa. Mahubiri haya yanahudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko, viongozi wakuu wa Sekretarieti ya Vatican pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kwenye Kikanisa cha “Mama wa Mkombozi” “Redemptoris Mater” kilichoko mjini Vatican.

Katika kipindi cha Majilio anasema Padre Raniero Cantalamessa, anapenda kuwaandaa waamini kuadhimisha Sherehe ya Noeli, wakiwa wanasindikizwa na Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa mintarafu matendo ya furaha kama yanavyotafakariwa kwenye Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya ukombozi. Tarehe 6 Desemba 2019, tafakari ya kwanza inaongozwa na tema: “Malaika Gabrieli anampasha habari Maria kuwa atakuwa Mama wa Mungu. Tumwombe Mungu atujalie unyenyekevu.”. Ijumaa tarehe 13 Desemba 2019, tema ya pili ni: Maria Mtakatifu anakwenda kumtembelea Elizabeti. Tumwombe Mungu atujalie mapendo ya jirani. Ijumaa tarehe 20 Desemba 2019, tema ya tatu ni: Yesu anazaliwa Bethlehemu. Tumwombe Mungu atujalie moyo wa ufukara. Bikira Maria anapewa nafasi ya pekee katika Fumbo la Umwilisho kutokana na utayari wa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake.

Padre Raniero Cantalamessa anahitimisha kwa kusema kwamba, tafakari hizi zinaonesha jinsi ambavyo Mama Kanisa na kila mwamini katika hali na maisha yake anavyopaswa kumuiga Bikira Maria katika imani, kwa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani na wawe tayari kumshuhudia Kristo Yesu anayezaliwa katika maisha na mazingira yao, ili kupyaisha imani, matumaini, mapendo na mshikamano wa dhati miongoni mwa watu wa Mungu!

Kipindi cha Majilio
05 December 2019, 15:59