Tafuta

Tarehe 12 Desemba 2019 ni Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe: Kanisa linaelekeza jicho lake huko Amerika ya Kusini Tarehe 12 Desemba 2019 ni Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe: Kanisa linaelekeza jicho lake huko Amerika ya Kusini 

Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe: Jicho la Kanisa Amerika ya Kusini

Kwa mara ya kwanza kumbu kumbu hii iliadhimishwa mjini Vatican tarehe 12 Desemba 2011 na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kama kumbu kumbu ya Jubilei ya uhuru kwa nchi nyingi za Amerika ya Kusini. Kunako mwaka 2014, Baba Mtakatifu Francisko akaonesha nia njema ya kutaka kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 12 Desemba, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, Msimamizi wa Amerika ya Kusini. Kama ilivyo ada, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican ili kuomba ulinzi na tunza ya Mama Bikira Maria wa Guadalupe, hasa kwa ajili ya familia ya Mungu huko Amerika ya Kusini ambayo kwa sasa ina kabiliwa na changamoto nyingi. Tume ya Kipapa kwa Amerika ya Kusini inakumbusha kwamba, kwa mara ya kwanza kumbu kumbu hii iliadhimishwa mjini Vatican tarehe 12 Desemba 2011 na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kama kumbu kumbu ya Jubilei ya uhuru kwa nchi nyingi za Amerika ya Kusini. Kunako mwaka 2014, Baba Mtakatifu Francisko akaonesha nia njema ya kutaka kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe. Na kwa sasa huu umekuwa ni sehemu ya utamaduni wa utume wake. Tarehe 12 Desemba 2019, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu, Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe kuanzia majira ya 12:00 jioni kwa saa za Ulaya.

Ibada hii ya Misa Takatifu ni sehemu ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kufanikisha Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia iliyotimua vumbi kuanzia tarehe 6 - 27 Oktoba, 2019 kwa kuongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Baada ya kusikiliza kwa makini, sasa ni wakati wa kujikita katika wongofu wa kiekolojia, shughuli za kichungaji, kitamaduni pamoja na wongofu wa kisinodi. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, Jioni tarehe 26 Oktoba 2019 alitoa hotuba ya kufunga maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Katika hotuba hiyo, likazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, wongofu wa kitamaduni unaojikita katika mchakato wa utamadunisho; wongofu wa kiekolojia unaofumbatwa katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; wongofu wa kijamii kwa kuheshimu utu na utambulisho wa watu mahalia. Wongofu wa kichungaji, uwawezeshe wananchi wa Ukanda wa Amazonia kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kama wakleri na watawa!

Kanisa linapaswa kuendeleza utume wake miongoni mwa vijana wa kizazi kipya pamoja na kuendelea kuwahamasisha mapadre na wamisionari kujisadaka kama zawadi ya imani kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu amekazia pia dhamana na utume wa wanawake katika Kanisa Ukanda wa Amazonia. Pili  kuendelea kuombea mchakato wa uinjilishaji mpya miongoni mwa waamini wa Amerika ya Kusini; ili waweze kukua na kuimarika:kiimani na kiutu, daima wakijitahidi kujikita katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya: haki, amani, umoja na mshikamano wa dhati. Kwa namna ya pekee, maadhimisho haya ambayo ni moto wa kuotea mbali, yanafanyika nchini Mexico na maeneo ambayo Ibada kwa Mama Bikira Maria wa Guadalupe imeenea kwa kiasi kikubwa. Katika siku za hivi karibuni, nchi nyingi za Amerika ya Kusini zimekumbwa na machafuko ya kisiasa kiasi cha kupelekea hata kwa baadhi ya nyumba za Ibada kuchomwa moto! Huu ni mwaliko kwa waamini kuangalia mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kukazia umoja na mshikamano wa dhati, ili kutoa majibu muafaka ya changamoto, matatizo na fursa zilizopo kati ya watu. Upendo kwa Mungu na jirani ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

B. Maria wa Guadalupe

 

11 December 2019, 15:18