Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa watu! Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa watu!  Tahariri

Changamoto ya kutangaza na kushuhudia Injili Ulimwenguni kote!

Wongofu wa shughuli za kichungaji unapaswa kukita mizizi yake katika maisha ya Kikristo, kwa kubadili mitazamo, vipaumbele sanjari na kubaki kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake. Kuna wakati familia ilikuwa ni kitovu na mahali pa kurithishia imani na kwamba, tunu msingi za maisha ya Kikristo ndizo zilizokuwa zinatumika kama dira na mwongozo wa maisha. Mambo yamebadilika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake za Noeli na matashi mema alizotoa, Jumamosi, tarehe 21 Desemba 2019 kwa Sekretarieti kuu ya Vatican alikaza kusema, mchakato wa mageuzi unaoendelea mjini Vatican unafumbata na kuambata toba na wongofu wa ndani, ili kutoa huduma makini zaidi kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Matokeo ya mageuzi haya ni mwelekeo mpya wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kati ya watu wa Mataifa. Amezungumzia kuhusu asili ya baadhi ya Mabaraza ya Kipapa na mchakato wa mageuzi ambayo yamekwisha kutekelezwa hadi wakati huu. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu yalianzishwa kwa lengo la kuinjilisha watu wa Mataifa. Sasa kuna haja ya kuwa na wongofu wa kichungaji kwa kusoma alama za nyakati. Mageuzi yaliyofanywa kwenye Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya jamii yanapania kuboresha zaidi huduma inayotolewa na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican kwa kuzingatia changamoto zinazoendelea kuibuliwa na ulimwengu wa kidigitali.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, mageuzi  ya Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu ni kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii yaani: wakimbizi na wahamiaji; ambao kwa sasa ni sawa na kilio cha watu wa Mungu kutoka jangwani. Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake, anafanya rejea tena kwa hotuba ya Baba Mtakatifu kwa Sekretarieti kuu ya Vatican kwa kusema kwamba, lengo na mabadiliko mbali mbali kwenye Sekretarieti kuu ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa walimwengu wanaotaka kuisukumizia dini pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu. Mababa wa Kanisa waliotangulia hata kabla ya Mtaguso Mkuu wa Vatican waliliona hili na kusema kwamba, leo hii kuna makundi mbali mbali yanayoshiriki katika mchakato wa kutengeneza na kuunda tamaduni za watu. Leo hii kuna uhuru na watu wana imani mbali mbali hata Barani Ulaya na wala si ukristo peke yake.

Changamoto zote hizi zinahitaji wongofu wa shughuli za kichungaji, kwa sababu Kanisa si kiungo pekee kinachowakutanisha watu katika umoja na mshikamano kama ilivyokuwa kwa pengine kwa miaka kadhaa iliyopita. Wongofu wa shughuli za kichungaji anasema Baba Mtakatifu Francisko unapaswa kukita mizizi yake katika maisha ya Kikristo, kwa kubadili mitazamo, vipaumbele sanjari na kubaki kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kuna wakati familia ilikuwa ni kitovu na mahali pa kurithishia imani na kwamba, tunu msingi za maisha ya Kikristo ndizo zilizokuwa zinatumika kama dira na mwongozo wa maisha ya kijamii. Leo hii, utamaduni na mapokeo haya yamevunjiliwa mbali na jamii kutokana na sababu mbali mbali kati yake ni chuki dhidi ya Ukristo. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, ni katika muktadha huu, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na viongozi wakuu wa Kanisa waliofuatia baadaye, wakajielekeza zaidi kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sehemu mbali mbali za dunia.

Huu ni mchakato wa kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya Huruma ya Mungu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, ambaye ameonesha mshikamano wa dhati na binadamu katika Fumbo la Umwilisho, mateso na kifo na chake Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu ndiye Msamaria mwema, anayejishusha chini ili kuwaganga wale waliopondeka moyo kwa mafuta ya huruma ya Mungu na divai ya Sakramenti za Kanisa. Kanisa limeagizwa kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu inayopaswa kupenya katika medani mbali mbali ya maisha ya mwanadamu. Huruma ni daraja inayomkutanisha Mungu na waja wake, kiasi cha kuonja upendo wake usiokuwa na mipaka. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kupyaisha sera na mikakati yake ya shughuli zake za kichungaji. Kanisa linapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa furaha ya Injili, kwa njia ya mvuto wenye mashiko na wala si kwa kufanya wongofu wa shuruti.

Hii ndiyo changamoto inayopaswa kutekelezwa na wamisionari katika maisha na utume wao. Watu waguswe na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii ndiyo namna bora zaidi ya kudhihirisha kwa nje neema ya ndani kutoka kwa Roho Mtakatifu na kwamba, huruma ndiyo fadhila kubwa kushinda nyingine zote. Kwa hakika, bila ya Kristo Yesu, wafuasi wake, hawawezi kufua dafu! Kanisa linakua na kupanuka kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kimsingi wongofu wa shuruti unakinzana na ari na mwamko wa majadiliano ya kidini na kiekumene. Wongofu wa shuruti ni kitendo kinachowakosea haki wahusika kwa kuingilia uhuru na utashi wao. Baba Mtakatifu anaonya kwamba, hata leo hii, Kanisa lisipokuwa makini, linaweza kujikuta likitumbukia katika wongofu wa shuruti unaotekelezwa Parokiani, kwenye vyama vya kitume pamoja na kwenye Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume!

Habari Njema ya Wokovu inapaswa kutangazwa na kushuhudiwa kama cheche ya imani, matumaini na mapendo kwa watu wa Mungu, ili wote waweze kuokolewa. Huu ni mwaliko kwa viongozi wa Kanisa kuondoa vikwazo vinavyowazuia watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Watu wote wana uwezo wa kupokea na kukumbatia tunu msingi za Injili kama walivyoshuhudia hata Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kama chemchemi ya kuyatakatifuza malimwengu, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Heri hizi zinakwenda sanjari na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Wakristo. Hii ni sehemu ya Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu anakaza kusema kwamba, Kanisa linawajibika kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili; kwa kusimama kidete katika wongofu wa kitamaduni unaothamini tamaduni, mila na desturi njema za watu mahalia.

Kwa njia hii, Kanisa linapaswa pia kupambwa kwa tunu msingi kutoka katika tamaduni mbali mbali “Sposa ornata monilibus suis”. Kanisa katika dhamana na utume wake wa Kimisionari linatumwa kuhamasisha mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na wala halina Mamlaka ya kudhibiti na kuweka vikwazo vya kiimani. Ni matamanio ya Kristo Yesu, kuweza kuwakumbatia na kuwaambata watu wote, ili kuwaonjesha huruma na upendo wake wa daima. Kwa hakika, bila ya Kristo Yesu, wafuasi wake, hawawezi kufua dafu na wala si mali kitu!

Tahariri
24 December 2019, 16:15