Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Nicolas Lhernould kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Constantine nchini Algeria. Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Nicolas Lhernould kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Constantine nchini Algeria.  (AFP or licensors)

Padre Nicolas Lhernould ateuliwa kuwa Askofu Jimbo la Constantine

Askofu mteule Nicolas Lhernould alizaliwa mwaka 1975 huko Courbevoie nchini Ufaransa. Alihitimu masomo yake na kujipatia shahada ya uzamili katika masomo ya sayansi jamii kunako mwaka 1997. Baada ya kutafakari sana kuhusu hatima ya wito na maisha yake, kunako mwaka 1999 akaamua kujiunga na malezi pamoja na majiundo ya kipadre na hatimaye kupadrishwa 22 Mei 2004.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Nicolas Lhernould kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Constantine, nchini Algeria. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Nicolas Lhernould alikuwa ni Makamu Askofu wa Jimbo kuu la Tunis, nchini Algeria. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Nicolas Lhernould alizaliwa tarehe 23 Machi 1975 huko Courbevoie nchini Ufaransa. Alihitimu masomo yake na kujipatia shahada ya uzamili katika masomo ya sayansi jamii kunako mwaka 1997. Baada ya kutafakari sana kuhusu hatima ya wito na maisha yake, kunako mwaka 1999 akaamua kujiunga na malezi pamoja na majiundo ya kipadre na kutumwa kusoma falsafa na taalimungu kwenye Chuo cha Kipapa cha Gregoriani kilichoko mjini Roma.

Hatimaye, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 22 Mei 2004 huko Tunis. Alijiendeleza na kufanikiwa kupata shahada ya uzamili kuhusu Mababa wa Kanisa kutoka katika Taasisi ya Kipapa ya “Agostinianum” iliyoko mjini Roma. Baada ya kurejea Jimboni Tunis, alibahatika kutekeleza utume wake kama Paroko kwenye Parokia Sousse, Monastir pamoja na Mahdia kati ya Mwaka 2005 hadi mwaka 2012. Kuanzia mwaka 2012 akateuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Sainte-Jeanne d’Arc Jimbo kuu la Tunis pamoja na kuwa ni Makamu wa Askofu Jimbo kuu la Tunis. Historia inaonesha kwamba, kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2014 alikuwa ni Rais wa “Kituo cha Masomo cha Carthage, Καρχηδών.”

Algeria
09 December 2019, 14:42