Siku ya Wavuvi Kimataifa inaadhimishwa tarehe 21 Novemba 2019 Siku ya Wavuvi Kimataifa inaadhimishwa tarehe 21 Novemba 2019 

Siku ya Wavuvi Duniani kwa Mwaka 2019: Ujumbe kutoka Vatican

Takwimu zinaonesha kuwa sekta ya uvuvi ni hatari kwa maisha ya binadamu. Kila mwaka zaidi ya wavuvi 32, 000 wanapoteza maisha. Wavuvi wengi wanafanyishwa kazi katika mazingira magumu na hatarishi; wanadhulumiwa na kunyonywa, wanatumbukiwa katika biashara ya binadamu na viungo vyake, kielelezo cha utumwa mamboleo nawanaofanyishwa kazi za suluba katika uvuvi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Wavuvi Duniani kwa Mwaka 2019 inaadhimishwa tarehe 21 Novemba 2019, kwa kujikita katika uwajibikaji wa kijamii katika sekta ya uvuvi, kwa kujielekeza zaidi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Sekta ya uvuvi ina mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Jumuiya ya Kimataifa na kwamba, wahusika wanapaswa kuwajibika kikamilifu katika masuala ya kijamii, utunzaji bora wa mazingira, uimarishaji wa uchumi pamoja na kuzingatia utawala wa sheria katika ulimwengu wa utandawazi. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu katika ujumbe wake kwa Siku ya Wavuvi Duniani kwa Mwaka 2019 anasema, siku hii inaongozwa na kauli mbiu “Uwajibikaji wa kijamii katika Mfumo wa Tunu za Sekta ya Uvuvi” kwa ajili ya mchakato wa maendeleo fungamani. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanabainisha wazi umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuzingatia kanuni maadili na utu wema katika masuala ya kiuchumi si tu kwa wamiliki bali pia wanapaswa kuwangalia wadau wengine wanaochangia katika ukuaji wa biashara.

Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna uhusiano wa karibu kati ya wamiliki wa shughuli za kiuchumi, maeneo wanamotekelezea shughuli zao za uzalishaji na kwamba, tafiti nyingi zinakazia uwajibikaji wa shughuli za kiuchumi kwa ajili ya jamii husika. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anasikitika kusema kwamba, dhana ya uwajibikaji wa kijamii katika sekta ya uvuvi haijapewa umuhimu unaostahili kutokana na ukubwa wa eneo, hali ya kutojali na uhuru usi ona mipaka kutoka kwa wahusika wakuu. Takwimu zinaonesha kwamba, sekta ya uvuvi ni hatari sana kwa maisha ya binadamu na kwamba, kila mwaka zaidi ya wavuvi 32, 000 wanapoteza maisha. Wavuvi wengi wanafanyishwa kazi katika mazingira magumu na hatarishi; wanadhulumiwa na kunyonywa, wanatumbukiwa katika biashara ya binadamu na viungo vyake, kielelezo cha utumwa mamboleo. Kuna wakimbizi na wahamiaji wanaofanyishwa kazi za suluba katika sekta ya uvuvi.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anapenda kuzihamasisha Serikali, Mashirika ya Kimataifa na Taasisi mbali mbali kuhakikisha kwamba, zinatekeleza kikamilifu wajibu wa kijamii, kwa kuzingatia mikataba na itifaki za kimataifa kwa ajili ya kuwalinda wavuvi pamoja na kuwapatia haki zao msingi. Huu ni mwaliko wa kuondokana na tabia ya kuwanyanyasa na kuwadhulumu wavuvi; kupuuzia haki zao msingi pamoja na kuchafua mazingira. Kuna haja ya kutunza ekolojia kwa kujielekeza zaidi katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu Ifikapo mwaka 2030, kwa kuhakikisha kwamba, tabia kama hizi zinatokomezwa. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume: “Caritas in veritate” yaani “Upendo katika ukweli” anakazia umuhimu wa kuthamini na kupenda kile kilicho kweli, ili kuweza kuweza kuwa na mwamko wa uwajibikaji kijamii na kwa ajili ya ujenzi wa mafungamano ya kijamii badala ya mwelekeo wa sasa wa kutaka kuwadaidisha wamiliki wa makampuni ya kiuchumi.

Ikumbukwe kwamba, tunu msingi za maisha ya kiroho zinaweza kusaidia kuboresha na hatimaye, kuchangia maisha ya watu wengi duniani, yaani upendo kwa Mungu na jirani. Kwa njia hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kujizatiti zaidi katika kulinda haki msingi za binadamu, ili watu wengi zaidi waweze kupata furaha ya kweli katika maisha sanjari na kuchangia katika Pato Ghafi la Taifa. Kanuni auni na uwajibikaji wa kijamii visaidie kuchangia usalama wa wavuvi na mafunzo kazini; maboresho ya vifaa vya uvuvi pamoja na kuhakikisha kwamba, wavuvi wanapata mshahara unaokidhi mahitaji yao, wanapata huduma za tiba, wanasaidiwa kukua kiroho pamoja na kupata msaada wa kisheria pale inapobidi, ili kuwawezesha wavuvi pamoja na familia zao kuwa ni watu wa furaha pia. Umefika wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha wavuvi. Watu waendelee kuhamasishwa kutambua na kuthamini haki msingi za wavuvi na mchango wao katika mchakato wa ukuaji wa maendeleo. Changamoto zote hizi zinapaswa kushughulikiwa na Jumuiya ya Kimataifa pamoja na kuhakikisha kwamba, wadau wote wanatekeleza vyema dhamana na wajibu wao kwa ajili ya maboresho ya maisha ya wavuvi na sekta ya uvuvi katika ujumla wake.

Siku ya Wavuvi Duniani 2019

 

 

 

23 November 2019, 17:29