Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya III ya Maskini Duniani 2019: Kauli Mbiu: "Matumaini ya wanyonge hayatapotea kamwe". Maadhimisho ya Siku ya III ya Maskini Duniani 2019: Kauli Mbiu: "Matumaini ya wanyonge hayatapotea kamwe". 

Siku ya III ya Maskini Duniani 2019: Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele

Siku ya III ya Maskini Duniani 2019 inaongozwa na kauli mbiu: "Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele”. Papa anatarajiwa kuhitimisha maadhimisho haya, Jumapili tarehe tarehe 17 Novemba 2019 kwa Ibada ya Misa Takatifu. Mara tu baada ya Misa takatifu, Baba Mtakatifu Francisko atajiunga na maskini 1, 500 kwa ajili ya kupata chakula cha mchana pamoja! Je, ninyi mhaisherekea ki vipi?

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa linapaswa kuwa ni kielelezo cha utandawazi wa mshikamano wa maisha ya kiroho dhidi ya sera na mikakati ya kiuchumi inayotenga, nyanyasa na kuwabagua maskini. Kwa sasa tofauti msingi kati ya watu kimekuwa ni chanzo cha kinzani, migogoro na uhasama. Lakini, ikumbukwe kwamba, dunia inahitaji wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, kwa kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, kwa kuthamini, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwa na Uso wa huruma kama ulivyofunuliwa na Kristo Yesu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wawe ni wajenzi na vyombo vya amani duniani; manabii wa huruma na wasamaria wema, wanaothubutu kuwahudumia maskini kwa: unyenyekevu, ari na moyo mkuu, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu, umoja na mshikamano wa binadamu.

Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, na kwa mara ya kwanza imeadhimishwa kunako mwaka 2017. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni kumbu kumbu endelevu ya huruma ya Mungu inayopaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa waamini katika ujumla wao. Siku hii ni fursa ya kushikamana kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, kama alama ya: urafiki, umoja na udugu wa kibinadamu unaovunjilia mbali kuta za utengano kwa sababu mbali mbali. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa daima limekuwa likisikiliza na kujibu kilio cha maskini na wahitaji kama inavyoshuhudiwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume, kwa kuwachagua Mashemasi saba walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho na hekima, ili waweze kutoa huduma kwa maskini.  

Hii ni alama ya kwanza ya huduma kwa maskini kutokana na utambuzi kwamba, maisha ya Kikristo yanafumbatwa katika udugu na mshikamano. Yesu mwenyewe aliwapatia maskini kipaumbele cha kwanza katika Heri za Mlimani kwa kusema, “Heri maskini, maana hao watairithi nchi”. Jumuiya ya kwanza ya Wakristo iliuza mali na vitu vyake na kuwagawia watu kadiri ya mahitaji yao! Maadhimisho ya Siku ya III ya Maskini Duniani kwa mwaka 2019 yanaongozwa na kauli mbiu "Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele”. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuhitimisha maadhimisho haya, Jumapili tarehe tarehe 17 Novemba 2019 kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baada ya Misa takatifu, Baba Mtakatifu Francisko atajiunga na maskini 1, 500 kwa ajili ya kupata chakula cha mchana pamoja, kwa ajili ya heshima ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kama kawaida, baada ya chakula, wale wote watakaohudhuria watapewa zawadi kama kumbu kumbu ya tukio hili. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, jitihada mbali mbali kwa ajili ya kuwaenzi na kuwahudumia maskini zitafanyika kwenye Makanisa mahalia sehemu mbali mbali za dunia. Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya anasema, kuanzia Jumapili tarehe 10 hadi  Jumapili ya 33 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, yaani tarehe 17 Novemba 2019, hata mwaka huu, maskini, wahamiaji na wakimbizi wanaweza kupata huduma ya kupima na kuchunguza afya zao; wanaweza kupata tiba na matibabu ya magonjwa mbali mbali yanayowaandama pamoja na kupata chanjo dhidi ya mafua ambayo kwa wakati huu ni ugonjwa unaowanyemelea watu wengi! Huduma hizi ni kielelezo cha mshikamano wa Injili ya upendo na huduma kutoka kwa wadau mbali mbali wa sekta ya afya.

Tujikumbushane tena sababu zinazopelekea umaskini kuendelea kushamiri duniani, licha ya sera na mikakati mbali mbali inayowekwa na Jumuiya ya Kimataifa: Kuna mambo mengi yanayochangia kuenea kwa umaskini duniani unaoendelea kujionesha katika nyuso za watu mbali mbali wanaoteseka na kunyanyaswa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, vita, ghasia na machafuko ya kijamii; kuna watu wanaofungwa na kutupwa magerezani bila kuhukumiwa na wengine wanapotea katika mazingira ya kutatanisha! Maskini ni watu wanaonyimwa uhuru na utu wao kusiginwa kama “soli ya kiatu”. Ni watu wanaoteseka kwa ujinga, magonjwa, ukosefu wa fursa za ajira, mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo na biashara ya binadamu na viungo vyake.  Wanalazimika kukimbilia nchi zao ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi kwa ajili yao binafsi pamoja na familia zao.

Siku ya Maskini 2019
12 November 2019, 16:41