Tafuta

Vatican News
Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano wa 31 wa IMO unakazia: Wajibu wa kimaadili, ekolojia fungamani, masuala ya kijamii, elimu na umuhimu wa majadiliano na ushirikiano. Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano wa 31 wa IMO unakazia: Wajibu wa kimaadili, ekolojia fungamani, masuala ya kijamii, elimu na umuhimu wa majadiliano na ushirikiano.  (ANSA)

Kardinali Turkson: Utunzaji wa bahari kwa maendeleo fungamani!

Ujumbe wa Vatican unakazia: Wajibu wa kimaadili katika mchakato wa ulinzi na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote; pili ni ekolojia fungamani ya maendeleo ya binadamu katika medani mbali mbali za maisha. Tatu ni suluhu ya changamoto mamboleo mintarafu mazingira kupembuliwa pia kwa kutumia “miwani ya kijamii”, umuhimu wa elimu ya ekolojia, majadiliano na ushirikiano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Kimataifa la Bahari la Umoja wa Mataifa ‘International Maritime Organization" (IMO), linajihusisha na hatua za kuboresha usalama wa usafirishaji wa kimataifa na kuzuia uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote kutoka melini. Ni Shirika linalojihusisha na masuala ya kisheria, ikiwa ni pamoja na masuala ya dhima na fidia, na pia linasaidia usafiri wa kimataifa wa baharini.  Ilikuwa ni tarehe 6 Machi 1948  huko Geneva nchini Uswiss katika mkutano ulioitishwa na Umoja wa Mataifa ulipopitisha Mkataba wa Kimataifa wa kuanzisha Shirika la Kimataifa la Bahari. Na tarehe 17 Machi 1958, lilianza kutekeleza dhamana na wajibu wake. Shirika hili limekuwa likijelekeza zaidi kwa mambo yafuatayo: Kutoa utaratibu wa ushirikiano katika nyanja ya udhibiti wa vitendo vya kiharamia; Ushirikiano wa masuala ya kiufundi yanayoathiri usafiri wa kibiashara wa kimataifa. Kuhimiza na kuhamasisaha kiwango cha juu katika usalama baharini, utunzaji wa mazingira na ufanisi katika usafiri wa majini. Kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazohusiana na malengo ya kuanzishwa kwa Shirika hili. 

Mkutano mkuu wa Shirika ni jukwaa linalowakutanisha wanachama ili kujadili na kupembua masuala mbali mbali ya kisheria, kiufundi sanjari na ulinzi na usalama wa mazingira nyumba ya wote! Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, ameongoza ujumbe wa Vatican kwenye mkutano wa thelathini na moja wa Shirika la Kimataifa la Bahari la Umoja wa Mataifa kwa kukazia mambo makuu matano: wajibu wa kimaadili katika mchakato wa ulinzi na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote; pili ni ekolojia fungamani ya maendeleo ya binadamu katika medani mbali mbali za maisha. Tatu ni suluhu ya changamoto mamboleo mintarafu mazingira kupembuliwa pia kwa kutumia “miwani ya kijamii”, umuhimu wa elimu ya ekolojia na mwishoni ni majadiliano na ushirikiano katika kupanga, kuamua na kutekeleza sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Kardinali Turkson amewasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa wajumbe wanaoshiriki katika mkutano huu unaopania pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inatumia kwa busara rasilimali za dunia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Juhudi hizi zinakwenda sanjari na upunguzaji wa uzalishaji wa hewa ya ukaa ambayo imesababisha madhara makubwa katika mazingira, usalama na maisha ya watu katika ujumla wake. Uchafuzi wa vyanzo vya maji, bahari na maziwa umepelekea athari kubwa katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Ujumbe wa Vatican katika mkutano huu unapenda kukazia wajibu wa kimaadili kama kanuni msingi ya ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii inatokana na ukweli kwamba, hii ni sehemu ya utekelezaji wa haki jamii kama inavyofafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika nyaraka zake mbali mbali.

Jumuiya ya Kimataifa ina haki na wajibu wa kutumia na kutunza bahari, maziwa na vyanzo mbali mbali vya maji kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu. Kanuni ya pili ni ekolojia fungamani ya maendeleo ya binadamu inayogusa medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu kama vile: masuala ya kiuchumi, ekolojia ya kijamii, ekolojia ya kitamaduni na  ekolojia ya maisha ya kila siku inayoongozwa na kanuni ya ustawi, mafao ya wengi na haki kati ya vizazi mbali mbali. Kumbe, uchafuzi wa mazingira una athari kubwa katika maisha ya binadamu na maendeleo yake. Haki jamii ni kati ya masuala tete yanayopaswa kuingizwa katika majadiliano ya juu ya utunzaji bora wa mazingira ili kuweza kusikiliza kilio cha Dunia Mama pamoja na kilio cha maskini duniani. Sera na mikakati hii ilenge pia kuboresha hali ya maisha ya wavuvi baharini pamoja na familia zao, sanjari na kuboresha mazingira ya kazi na haki zao msingi.

Changamoto na matatizo mbali mbali yanayojitokeza katika uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote yanapaswa kushughulikiwa kwa pamoja kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema; katika umoja na mshikamano kwa kuwaambata na kuwakumbatia watu wote. Kanuni ya nne ni elimu ya utunzaji bora wa mazingira inayopaswa kumwilishwa katika malezi na makuzi ya watoto hadi watu wazima. Elimu ya utunzaji bora wa mazingira ni muhimu sana kwa vijana wa kizazi kipya. Kanuni ya tano inakita ujumbe wake kwa kuwataka watu wa Mungu kuhakikisha kwamba, wanajadiliana na kushirikisha mamuzi na utekelezaji wake katika ngazi mbali mbali. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na tafuiti makini ili ziweze kufanyiwa kazi. Kuhusu utunzaji bora wa mazingira, jambo la msingi ni ushirikiano na wala hakuna sababu za malumbano yasiyokuwa na tija wala mvuto, kwa sababu athari za mabadiliko ya tabianchi hazibagui wala hazichagui, wote wanaathirika, lakini maskini wanaathirika zaidi.

kardinali Turkson
28 November 2019, 18:07