Tafuta

Vatican News
Rais Joao Lourenco wa Angola amekutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican, tarehe 12 Novemba 2019. Rais Joao Lourenco wa Angola amekutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican, tarehe 12 Novemba 2019.  (ANSA)

Rais Joao Lorenzo wa Angola akutana na Papa Francisko: Maendeleo!

Viongozi hawa wawili, wameridhishwa na uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Angola sanjari na mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini humo. Wamegusia mkataba uliotiwa saini hapo tarehe 13 Septemba 2019 na kujadili kuhusu hali halisi nchini Angola, kwa kukazia umuhimu wa kuboresha maendeleo na haki jamii nchini Angola.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 12 Novemba 2019 amekutana na kuzungumza na Rais João Manuel Gonçalves Lourenço wa Angola pamoja na ujumbe wake, wakati alipomtembelea mjini Vatican. Wakati huo huo, Monsinyo Mirosław Stanisław Wachowski, Katibu mkuu msaidizi wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa amekutana na kuzungumza pia na Bwana Manuel Domingos Augusto, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Angola. Katika mazungumzo ya viongozi hawa wawili, wameridhishwa na uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Angola sanjari na mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Angola.  

Viongozi hawa baadaye, wamejielekeza zaidi katika mkataba uliotiwa saini hapo tarehe 13 Septemba 2019. Baadaye, wameendelea kujadili kuhusu hali halisi nchini Angola, kwa kukazia umuhimu wa kuongeza bidii na juhudi zitakazosaidia kuboresha mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na kudumisha haki jamii! Rais João Manuel Gonçalves Lourenço wa Angola na ujumbe wake, wamepata pia bahati ya kutembelea na kuhojiana na Radio Vatican.

Papa: Rais wa Angola
12 November 2019, 16:04