Tafuta

Vatican News
Familia ya Mungu nchini Tanzania inaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kadiri ya wito, mazingira na fursa zilizopo! Familia ya Mungu nchini Tanzania inaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kadiri ya wito, mazingira na fursa zilizopo!  (Vatican Media)

Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019: Kuzeni ari ya kimisionari

Kanisa nchini Tanzania linatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sanjari na linatakiwa kujikita zaidi na zaidi katika kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari miongoni mwa watu wa vijana wa kizazi kipya nchini Tanzania. Kila mwamini anapaswa kutambua kwamba amebatizwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili kadiri ya maisha, wito na mazingira yake! Umisionari!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza katika kufanikisha maadhimisho ya Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019. Hayo yamesemwa hivi karibuni na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, wakati alipokuwa akifungua mkutano Shirika la Kipapa la Umoja wa Wamisionari hivi karibuni. Amebainisha kwamba,  Mwezi Oktoba 2019 ulitengwa maalum na Mama Kanisa kwa ajili ya kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari sehemu mbali mbali za dunia, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa. Kanisa la Kristo katika utume”. Itakumbukwa kwamba, Mwaka 2019, Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume "Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari” akafungua rasmi ukurasa mpya wa maisha na utume wa Kanisa mintarafu shughuli za kimisionari, kwa kulitaka Kanisa kuanzisha mchakato wa majiundo na malezi kwa ajili ya kuyategemeza Makanisa mahalia kwa rasilimali watu, yaani mihimili ya uinjilishaji.

Hiki kimekuwa ni kipindi cha kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari. Imekuwa ni fursa muhimu kwa Kanisa kujikita zaidi katika utekelezaji wa mambo makuu manne: Mosi, waamini wamejitahidi kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Sala. Pili ni ushuhuda wa wamisionari watakatifu, wafiadini na waungama imani, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Tatu ni majiundo makini, endelevu na fungamani ya kimisionari kwa kujikita katika: Biblia, Katekesi, Tasaufi na Taalimungu. Nne ni huduma ya upendo kama kielelezo cha Injili ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, kama kielelezo makini cha imani tendaji! Huu umekuwa ni muda muafaka wa Injili kutangazwa, Sakramenti za Kanisa kuadhimishwa na Wakristo kutoa ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake pamoja na kuendelea kujikita katika Tafakari ya Neno la Mungu. Haya ni mambo yanayopaswa kuendelezwa katika sera, mikakati, maisha na utume kwa Makanisa mahalia.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, Katibu Mwambata, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, hivi karibuni ameshìriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuhitimisha Mwezi Maalum wa Kimisionari nchini Tanzania. Amelipongeza Kanisa la Tanzania kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sanjari na kulitaka kujikita zaidi na zaidi katika kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari miongoni mwa vijana wa kizazi kipya nchini Tanzania. Kila mwamini anapaswa kutambua kwamba amebatizwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili kadiri ya maisha, wito na mazingira yake. Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu litaendelea kusaidia mchakato wa kujenga na kuyaimarisha Makanisa katika nchi za kimisionari, ili hatimaye, siku moja yaweze kujitegemea.

Ushuhuda wa ari na mwamko wa kimisionari unapaswa kumwilishwa katika sera na mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji majimboni, kwenye parokia na hasa zaidi kwenye jumuiya ndogo ndogo za Kikristo. Askofu mkuu Giampietro Dal Toso amekazia umuhimu wa Kanisa nchini Tanzania kuwekeza zaidi katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kujenga familia ambazo zitakuwa kweli ni Kanisa dogo la nyumbani; Shule ya Sala, Neno la Mungu, Sakramenti na matendo ya huruma kama kielelezo cha imani tendaji. Familia zijenge na kudumisha umoja, upendo na mshikamano.

Kardinali Filoni
16 November 2019, 13:39