Tafuta

Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za wafungwa wa kivita kimataifa! Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za wafungwa wa kivita kimataifa! 

Kanisa litaendelea kutetea haki za wafungwa wa kivita duniani!

Wahudumu Wakatoliki wa Maisha ya Kiroho kwenye Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na Maaskofu wa Majimbo ya Kijeshi, ni vyombo na mashuhuda wanaotafuta kujenga na kuimarisha mchakato wa majadiliano ya haki na amani, hasa katika ulimwengu mamboleo ambao umegubikwa na Vita ya Tatu ya Dunia inayopiganwa vipande vipande, sehemu mbali mbali za dunia. Utu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wahudumu Wakatoliki wa Maisha ya Kiroho kwenye Vikosi vya Ulinzi na Usalama, 130 kutoka katika nchi 70 pamoja na Maaskofu wa Majimbo ya Kijeshi, kuanzia tarehe 29-31 Oktoba 2019 wamehudhuria kozi ya awamu ya tano kuhusu haki za kimataifa. Kozi hii iliandaliwa na: Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu pamoja na Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki. Kozi ya mwaka huu imejikita zaidi katika: Ukosefu wa uhuru wakati wa vita sanjari na Dhamana na utume wa wahudumu wa maisha ya kiroho kwenye vikosi vya ulinzi na usalama. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu katika hotuba yake ya utangulizi walipokutana na Baba Mtakatifu Francisko na kusema kwamba, Wahudumu Wakatoliki wa Maisha ya Kiroho kwenye Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na Maaskofu wa Majimbo ya Kijeshi, ni vyombo na mashuhuda wanaotafuta kujenga na kuimarisha mchakato wa majadiliano ya haki na amani, hasa katika ulimwengu mamboleo ambao umegubikwa na Vita ya Tatu ya Dunia inayopiganwa vipande vipande, sehemu mbali mbali za dunia.

Kozi hii pamoja na mambo mengine, imeasaidia kuamsha tena dhamiri nyofu kuhusu matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za wafungwa wa vita. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anasema, Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki ya wafungwa kimataifa, kwa kutambua kwamba, wahudumu wa maisha ya kiroho kwenye vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na Maaskofu wa Majimbo ya Kijeshi ni mashuhuda wa upendo wenye huruma unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika hali na maisha ya wafungwa wa vita ambao mara nyingi utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa sana. Hawa ni mashuhuda wanaotekeleza dhamana na utume wao si tu kwa maneno, bali kwa njia ya sadaka ya maisha yenye mvuto na mashiko. Wafungwa wa vita mara nyingi ni watu ambao wanadhulumiwa na kunyanyasika sana na mifumo mipya ya uhalifu wa kimataifa.

Kwa upande wake, Padre Giulio Cerchietti, Mratibu wa Ofisi ya Kimataifa ya Majimbo ya Kijeshi katika Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu  anasema, ni kutokana na muktadha huu, kuna haja ya kuwaandaa wakleri maalum watakaosadaka maisha yao kwa ajili ya kusimamia kanuni, sheria na taratibu zinazopewa kipaumbele cha kwanza na Kanisa katika utekelezaji wa haki ya wafungwa wa kivita kimataifa. Kozi Awamu ya 5 kwa Mwaka 2019 ni sehemu ya kumbu kumbu  ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa Kimataifa wa Geneva wa mwaka 1949. Mkataba huu ni chombo cha sheria kimataifa, kinachodhibiti  matumizi ya nguvu wakati wa vita, kwa kukazia umuhimu wa kuwalinda raia na wafungwa wakati wa vita. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, kumekuwepo na mkanganyiko mkubwa wa jinsi ya utekelezaji wa haki za binadamu kimataifa. Leo hii maktaba nyingi zinafurika vitabu na nyaraka zinazokazia haki binafsi, ili kukidhi vionjo na matarajio ya watu katika kipindi mpito na kusahau haki msingi za binadamu na matokeo yake, haki inakosekana na watu wanaanza “kujimwambafai kwa ajili ya mafao binafsi”.

Waathirika wakuu ni wafungwa wa kivita. Hata katika hali tete ya vita na kinzani za kijamii, utu, heshima na haki msingi za wafungwa zinapaswa kuheshimiwa na kudumishwa na wote. Dhamana na utume huu, kimsingi unapaswa kutekelezwa na Wahudumu Wakatoliki wa Maisha ya Kiroho kwenye Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na Maaskofu wa Majimbo ya Kijeshi. Katika mazingira na changamoto kama hizi, kuna haja kwa Majimbo ya Kijeshi kuwafunda watu wake watakaokuwa na nguvu, ari na jeuri ya kukemea pale haki za wafungwa wa vita kimataifa zinaposiginwa. Kuna hatari pia ya wafungwa wa kijeshi kesi zao kusikilizwa na kutolewa hukumu kwa kuchelewa sana, hali ambayo inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu kama inavyojitokeza huko nchini Argentina. Licha ya kinzani na hali tete ya kisiasa na kijamii, lakini Venezuela inajitahidi kutekeleza haki za wafungwa wa vita kimataifa. Hivi karibuni, Waziri wa Ulinzi nchini Venezuela aliandaa kozi maalum kwa ajili ya vikosi vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha kwamba, vinatekeleza na kuzingatia haki za wafungwa kimataifa.

Wafungwa wa Kivita
13 November 2019, 15:14