Tafuta

Majadiliano ya kidini na kiekumene ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo! Majadiliano ya kidini na kiekumene ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo! 

Majadiliano ya kidini na kiekumene ni sehemu ya Uinjilishaji!

Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo anapenda kujikita zaidi katika mchakato wa uinjilishaji unaokita mizizi yake katika majadiliano ya kidini na kiekumene ili kulinda, kudumisha na kuendeleza misingi ya haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Hii ni sehemu ya mchakato wa mshikamano katika huduma kwa maskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unajikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini ili kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu Injili, ni kwa kadiri ile ile wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia ni mambo yanayowaunganisha wote bila ubaguzi hata kidogo. Damu ya Wakristo, itaendelea kuwa ni mbegu ya Ukristo na mchakato wa umoja wa Wakristo. Wakristo wote wanateseka na kudhulumiwa kwa sababu ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; kumbe, uekumene wa damu una nguvu sana kama kielelezo cha ushuhuda wa imani yenye mvuto na mashiko! Takwimu zinaonesha kwamba, hata katika ulimwengu mamboleo, bado kuna Wakristo wanaoendelea kuteseka kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni katika muktadha huu, Mashuhuda wa uekumene wa damu, wanawataka Wakristo kubaki wakiwa wameungana, ili mbegu hii iweze kuzaa matunda ya umoja, upendo na mshikamano wa dhati. Leo hii kuna wafiadini wengi zaidi duniani, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo. Mashuhuda wa uekumene wa damu kutoka katika Makanisa mbali mbali kwa sasa wanaunganishwa na kifungo cha upendo huko mbinguni.

Mbegu waliyopandikiza duniani, itazaa matunda kwa wakati wake. Lengo kuu ni ushuhuda wenye mvuto kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Mama Kanisa anaendeleza juhudi za uinjilishaji unaofumbatwa pia katika mchakato wa majadiliano ya kidini. Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Hivi karibuni, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Antonianum, Kitivo cha Taalimungu cha Mtakatifu Bonaventura “Seraphicum”, kimeadhimisha kongamano ambalo pamoja na mambo mengine, limejadili kuhusu: kumbu kumbu ya miaka 800 iliyopita wakati Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokutana na kuzungumza na Sultan Al Malik al Kamil. Huo ukawa ni mwanzo wa ujenzi wa umoja, udugu na amani miongoni mwa Wakristo na waamini wa dini ya Kiislam. Changamoto mamboleo ni kwa waamini wa dini mbali mbali duniani kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Ukarimu kwa maskini na wahitaji zaidi; haki na amani; wema na upendo ni kati ya mambo ambayo yamejadiliwa kwa kina na mapana kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu. Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni katika hotuba yake amekazia umuhimu wa ujenzi wa jamii inayoheshimiana na kuthamiana ili kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu.

Kumbe, majadiliano ya kidini ndani ya Kanisa Katoliki ni changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mambo msingi: haki jamii, tunu msingi za kimaadili; amani, uhuru wa kuabudu pamoja na kuendeleza haki msingi za binadamu. Ikumbukwe kwamba, binadamu wote ni sawa kwa sababu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake, alijitahidi kuhakikisha kwamba, majadiliano ya kidini yanakuwa ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Leo hii kuna Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linaloendeleza jitihada hizi. Majadiliano ya kidini yanapaswa kwenda sanjari na majadiliano ya kitamaduni na pale inapowezekana kuwa na taalimungu ya kidini. Kanisa ni Sakramenti ya wokovu kwa wote. Kanisa linaheshimu na kuthamini tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili zinazopatikana miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali duniani.

Kanisa Katoliki halikatai yaliyo ya kweli na matakatifu katika dini hizi. Lakini, Kanisa litaendelea kutangaza na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu ndiye njia, ukweli na uzima, na ambaye ndani yake, wanadamu wanaona utimilifu wa maisha ya utauwa, na ambamo Mungu alivipatanisha vitu vyote na nafsi yake. Majadiliano ya kidini, yawawezeshe waamini wa dini mbali mbali kutoa ushuhuda wa imani yao, kwa kukuza mema ya kiroho na ya kimaadili; na tunu za kijamii na za kitamaduni ambazo zinapatikana katika dini hizi.

Kardinali Ravasi
06 November 2019, 15:47