Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anatembelea Barani Asia akiwa amebeba Injili ya Maisha na Injili ya Amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anatembelea Barani Asia akiwa amebeba Injili ya Maisha na Injili ya Amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.   (ANSA)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Asia: Injili ya uhai na amani!

Papa Francisko anakwenda Barani Asia akiwa na Injili ya maisha na amani mikononi mwake. Matumizi ya silaha za kinyuklia ni kinyume kabisa cha kanuni maadili. Familia ya Mungu nchini Japan inatambua fika umuhimu wa utamaduni wa majadiliano na udugu miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; ili kujenga umoja na mshikamano sanjari na kulinda utu na haki msingi za binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Jumatano, tarehe 19-26 Novemba 2019 Barani Asia kwa kutembelea: Thailand na Japan ni sehemu ya mchakato wa Kanisa wa kutaka kudumisha majadiliano ya kidini na kitamaduni ili kulinda: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo, mafao ya wengi, haki na amani duniani na kwa namna ya pekee Barani Asia. Baba Mtakatifu anakwenda Barani Asia akiwa na Injili ya maisha na amani mikononi mwake. Matumizi ya silaha za kinyuklia ni kinyume kabisa cha kanuni maadili. Familia ya Mungu nchini Japan inatambua fika umuhimu wa utamaduni wa majadiliano na udugu miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; ili kujenga umoja na mshikamano sanjari na kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu, tayari kujielekeza zaidi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, hiki ni kiini cha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya thelathini na mbili kimataifa Barani Asia.

Hija hii inachapa ya kimisionari kwa kufuata nyayo za Mtakatifu Yohane Paulo II, kunako mwaka 1981 alipotembelea, Tokyo, Japan na Mwaka 1984 alipotembelea Bankok nchini Thailand. Hizi ni nchi ambazo zina idadi ndogo sana ya waamini wa Kanisa Katoliki, lakini Baba Mtakatifu anataka kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo. Baba Mtakatifu anatembelea nchi hizi wakati ulimwengu wautandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano vimepamba moto. Baba Mtakatifu anataka kushuhudia kwa macho yake mwenyewe na kukutana na watu wa Mungu katika nchi hizi mbili, ili kuwatia shime, wasonge mbele kama mashuhuda na vyombo vya tunu msingi za maisha ya Kikristo. Anawataka kwa pamoja waweze kutafuta na hatimaye, kujipatia majibu muafaka ili kukubaliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Makanisa mahalia.

Habari Njema ya Wokovu haina budi kutangazwa na kushuhudiwa kwa ari na moyo mkuu, kwa njia ya ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo kama kielelezo cha imani tendaji! Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 19-23 Novemba 2019 anafanya hija ya kitume nchini Thailand inayoongozwa na kauli mbiu: “Mitume wa Kristo, Wamisionari Mitume”. Hija hii ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa utume wa Vikarieti ya Siam kunako mwaka 1669. Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, Baba Mtakatifu anafuata nyayo za wale wamisionari wa kwanza, waliosadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Wakapandikiza mbegu ya imani nchini Thailand, utume uliotekelezwa na Wafranciskani pamoja na Wadominican, leo hii kuna Majimbo kumi na moja nchini Thailand. Baba Mtakatifu anawataka Wakristo nchini Thailand kuwa kweli ni wafuasi amini wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Wamisionari Mitume, vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, watu ambao wako tayari kujisadaka kwa ajili ya uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia ambayo yameongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu ni amri kutoka kwa Kristo Yesu kwa wafuasi wake na kwamba, utume wa kimisionari ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Bila kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, Kanisa litabaki kuwa kama “Chama cha Maisha ya kiroho” kinachoshindwa kutoa nafasi kwa Kristo Yesu ili kuendelea kukutana na waja wake, katika hija ya maisha yao ya ndani. Kwa njia ya nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, Kanisa linahamasishwa kutoka na kuwaendea watu wake kwani Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu wa mchakato wa uinjilishaji kama ilivyokuwa hata katika Kanisa la Mwanzo mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume.

Huu ni mchakato wa uinjilishaji unaokita vipaumbele vyake katika ushuhuda anasema Kardinali Pietro Parolin. Ari na mwamko wa kimisionari ni changamoto endelevu kwa kila mwamini mbatizwa! Kauli mbiu iliyochaguliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Japan kwa ajili ya hija ya Baba Mtakatifu nchini Japan kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019 ni “Linda Maisha Yote”. Huu ni ujumbe unaowataka watu wa Mungu nchini Japan kusimama kidete kulinda: utu na heshima ya binadamu dhidi ya vitisho vinavyohatarisha misingi ya amani na utulivu na hasa zaidi mapambano ya silaha. Japan inatambua fika madhara ya vita na matumizi ya silaha za atomiki; maafa makubwa ya tetemeko kubwa la ardhi na tsunami iliofuatia vilisababisha vifo vya watu 20,000 nchini Japan. Uharibifu uliosababishwa kwenye mtambo wa nyuklia wa Fukushima Daichi ukapelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linasema kuna haja ya kusimama kidete “Kulinda maisha yote”.

Kardinali Parolin anasikitika kusema kwamba, Japan ni nchi ambayo imeathirika sana na mashambulizi ya silaha za atomiki huko Hiroshima na Nagasaki. Licha ya “patashika nguo kuchanika wakati wa vita” Japan, ikaibuka kidedea na kuanza kuchapa mwendo katika ukuaji wa uchumi, ustawi na maendeleo ya watu wake. Changamoto ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; anahimiza umuhimu wa kutafuta na kudumisha amani duniani bila ya vitisho vya mashambulizi na maangamizi ya silaha za kinyuklia. Ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anaunga mkono jitihada za kupiga marufuku utengenezaji, usambazaji na ulimbikizaji wa silaha za nyuklia. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anahitimisha mahojiano maalum na Vatican News kwa kusema kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Asia ni kielelezo cha mchungaji mwema anayetaka kuwashirikisha watu wa Mungu furaha ya Injili, matumaini na mapendo.

Kama mchungaji mwema, anaguswa na mahangaiko pamoja na matarajio ya watu wake. Ujumbe wa kimisionari unaotolewa na Baba Mtakatifu unaligusa Kanisa zima, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, umuhimu wa kukuza na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu, amani, ustawi na maendeleo ya wengi! Haya ni mambo yanayoligusa Kanisa katika ujumla wake.

Kard. Parolin: Asia
19 November 2019, 15:35