Tafuta

Vatican News
Papa Francisko, tarehe 26 Novemba 2019 ametembelea na kuzungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Sophia, Jijini Tokyo, nchini Japan. Papa Francisko, tarehe 26 Novemba 2019 ametembelea na kuzungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Sophia, Jijini Tokyo, nchini Japan.  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko Japan: Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sophia, Tokyo, Japan!

Baada ya Miaka 38 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea chuoni hapo, tarehe 26 Novemba 2019, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sophia kikatembelewa na Papa Francisko. Chuo kina vyuo vikuu vishiriki 300 kutoka katika nchi 59 duniani. Kina idara 29 na vitivo tisa. Kuna jumla ya wanafunzi 13, 000 na kuna Maprofesa 1, 400 wanaotoka katika nchi 21 duniani. Elimu bora kwa wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa Katoliki nchini Japan, mwaka 2019 linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 470 tangu alipowasili nchini humo, Mtakatifu Francisko Xavier pamoja na wenzake na huo ukawa ni mwanzo wa kuenea kwa Ukristo nchini Japan. Kunako mwaka 1614 madhulumu dhidi ya Wakristo yakafumuka na kupamba moto kwa takribani miaka 260 na waamini wengi wakauwawa kikatili kwa ajili ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika kipindi cha madhulumu, Wakristo waliokuwa wanaishi kwenye Mkoa wa Nagasaki waliendelea kupyaisha imani yao na kufanikiwa kuwarithisha wengine amana na utajiri huu kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji, sala na katekesi ya kina. Pamoja na hayo yote, mwaka 2019 Japan inaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Balozi wa kwanza wa Vatican alipotumwa rasmi nchini Japan. Maaskofu Katoliki Japan wanamwomba Mwenyezi Mungu ili awasaidie watu wa Mungu nchini Japan kuthamini Ukristo na Kanisa Katoliki, ili mahusiano na mafungamano baina ya pande hizi mbili, yasaidie kuchochea mchakato wa maendeleo fungamani kwa ajili ya Jumuiya ya Kimataifa.

Kauli mbiu iliyochaguliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Japan kwa ajili ya hija ya 32 ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Japan ni “Linda Maisha Yote”. Baba Mtakatifu, Jumanne tarehe 26 Novemba 2019 amepata nafasi ya kutembelea na kuzungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sophia kilicho mjini Tokyo, nchini Japan. Chuo Kikuu hiki ilikuwa ni ndoto ya awali kabisa ya  Mtakatifu Francisko Xavier, yapata Miaka 470 tangu alipowasili nchini humo yaani kunako mwaka 1549, lakini ndoto hii ikawa ukweli kunako mwaka 1913, chini ya uongozi wa Papa Pio wa X. Mwaka 2013, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sophia kikaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Baada ya Miaka 38 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea chuoni hapo, tarehe 26 Novemba 2019, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sophia kikashuhudia uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko. Chuo hiki kina vyuo vikuu vishiriki 300 kutoka katika nchi 59 duniani. Kina idara 29 na vitivo tisa. Kuna jumla ya wanafunzi 13, 000 na kati yao kuna wanafunzi wa kimataifa takribani 150, 000. Kuna Maprofesa 1, 400 wanaotoka katika nchi 21 duniani.

Padre Tsutomu Sakuma SJ, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sophia katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na wanajumuiya wa Chuo Kikuu cha Sophia amelishukuru Kanisa Katoliki kwa kuwekeza sana katika sekta ya elimu kwa ajili ya malezi na majiundo ya kina kwa vijana wa kizazi kipya. Chuo hiki kimekuwa pia ni chachu ya kukoleza miito mitakatifu, ikizingatiwa kwamba, kuna “ukame wa miito ya kipadre na kitawa nchini Japan”. Sera na mikakati ya elimu Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sophia ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Wayesuit katika Kipindi cha Miaka kumi yaani kuanzia mwaka 2019-2029. Wayesuit katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa, wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mambo makuu yafuatayo: Kuendeleza mchakato wa mang’amuzi na mafungo ya kiroho; Kushikamana na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; Kuwasindikiza vijana katika safari ya maisha yao; Mwishoni ni kutunza mazingira nyumba ya wote. Haya ni mambo ambayo yanabainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika barua aliyomwandikia Padre Arturo Sosa, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit kama sehemu ya mpango mkakati wa maisha na utume wao katika kipindi cha miaka kumi yaani kuanzia mwaka 2019-2029.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hivi pia ndivyo vipaumbele vya Kanisa la Kiulimwengu kwa wakati huu! Mambo ambayo yanapaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Sinodi za Maaskofu na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia. Kwa ufupi, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sophia kinataka kuwashirikisha wanafunzi katika mchakato mzima wa elimu, maarifa na ujuzi, kwa kukazia tafiti maalum na makini pamoja na kuwaandaa wanafunzi ili waweze kuingia kwa urahisi katika soko la ajira. Pamoja na mambo mengine, Chuo kinatoa upendeleo wa pekee kwa wanafunzi wanatoka katika familia zenye kipato duni, pamoja na kujielekeza zaidi katika sera za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ili watu wa Mungu waweze kuishi kwa amani na utulivu.

Chuo Kikuu cha Sophia

 

 

26 November 2019, 15:15