Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza hija yake ya 32 ya Kitume Barani Asia kwa kutembelea Thailand na Japan amejikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Afrya ya Warumi. Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza hija yake ya 32 ya Kitume Barani Asia kwa kutembelea Thailand na Japan amejikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Afrya ya Warumi. 

Papa Francisko ajikabidhi chini ya Bikira Maria Afya ya Warumi!

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 19 Novemba 2019 alikwenda kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” iliyoko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu Jimbo kuu la Roma kabla ya kuanza hija yake ya kitume ya 32 huko Thailand na Japan, kuanzia tarehe 19-26 Novemba 2019. Baba Mtakatifu anakwenda kuwatembelea rafiki zake walioko Thailand na Japan.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kama sehemu ya desturi na utamaduni wake, Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, asubuhi tarehe 19 Novemba 2019 alikwenda kutembelea na kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” iliyoko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, lililoko Jimbo kuu la Roma, kabla ya kuanza hija yake ya kitume ya 32 huko Thailand na Japan, kuanzia tarehe 19-26 Novemba 2019. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema kwamba, Jumatano tarehe 19 Novemba 2019 anaanza hija ya kuwatembelea rafiki zake walioko nchini Thailand na Japan. Anatarajia kukutana na kusali nao. Ni matumaini yake kwamba, siku hizi zitasheheni utajiri wa neema na furaha. Wachunguzi wa mambo wanasema, Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko Jimbo kuu la Roma ni kati ya Makanisa ambayo Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ameyatembelea mara nyingi zaidi kwa ajili ya sala ya binafsi: kuomba na kushukuru kila wakati anapoadhimisha matukio makuu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, ili aweze kuwasaidia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, kielelezo cha imani tendaji! Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha imani, matumaini na mapendo, kwani amediriki kuwa ni mfuasi wa kwanza wa Kristo Yesu na chombo cha huduma makini kwa jirani zake; mtindo na mfumo wa maisha unaopaswa kutekelezwa na Mapadre kama sehemu ya majiundo yao ya awali na endelevu katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, ikiwa kweli waamini wanataka kuwa wafuasi wamisionari wa Kristo Yesu na Kanisa lake; ili kuguswa na kuponywa na huruma pamoja na upendo wa Mungu, wanapaswa kuzingatia mambo makuu yafuatayo: Fumbo la Msalaba, Ekaristi Takatifu na Ibada ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Bikira Maria ni Mama wa Mungu na Kanisa, kwani ndani ya Moyo wake safi usiokuwa na doa, watu wote wanapata utambulisho wao, kwa kupenda na kupendwa, hali inayoonesha uwepo wa Mungu kati ya watu wake.

Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mama wa Mlango wa Mbinguni, ametangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni “Bikira Maria Mama wa huruma na matumaini”. Ni Mama ambaye daima ameonesha ulinzi na tunza kwa watu wanaomkimbilia katika shida na mahangaiko yao; upendo ambao umeendelezwa hadi nyakati hizi. Bikira Maria ni dira na kielelezo cha njia ya kwenda mbinguni; Njia ambayo kamwe haiwezi kumpotezesha mtu mwelekeo wa maisha! Njia hii, ni Kristo ambaye pia ni ukweli na uzima. Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anasema, kunako mwaka 2015, Kanisa liliadhimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu; mwaka ambao umewawezesha waamini wengi kuvuka Lango la Huruma ya Mungu, ili kuonja upendo unaofariji, unaosamehe na kutoa matumaini.

Hii ndiyo hamu inayopaswa kushuhudiwa na watu wote kwa kuwaonjesha jirani zao wema na huruma ya Mungu katika maisha yao. Bikira Maria Mama wa huruma na matumaini, asaidie watu kusambaza na kueneza wema na huruma ya Mungu kama njia ya kuganga na kuponya madonda yanayomwandama mwanadamu, tayari kusimama na kupiga moyo konde, ili kusonga mbele kwa neema na baraka ya Mungu. Baba Mtakatifu anawataka waamini  kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amejishusha ili kuwaokoa, mwaliko kwao pia ni kujishusha na kuwainamia jirani zao wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali, kwa kuwa na jicho la huduma kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, ili kuwaonjesha watu wanaoteseka, ile “divai ya furaha”, kama ilivyotokea kwenye Arusi ya Kana. Bikira Maria awe ni mfano na kielelezo cha wanawawake wote ambao wamekuwa kweli ni tabernakulo ya Injili ya uhai, ili kuwaheshimu na kutambua dhamana, wito na utume wao kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Hata katika ukimya wao, wanawake ni nguvu ya matumaini.

Papa: B.Maria
19 November 2019, 13:54