Vatican News
Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana kilichoko mjini Roma, tarehe 7 Novemba 2019 kinaadhimisha Siku ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana kilichoko mjini Roma, tarehe 7 Novemba 2019 kinaadhimisha Siku ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.  (AFP or licensors)

Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana: Siku ya Mwl. Julius K. Nyerere!

Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, Roma, Alhamisi tarehe 7 Novemba 2019 ni siku maalum iliyotengwa kwa ajili ya kumtafakari Mwl. J. K. Nyerere, miaka ishirini tangu alipofariki dunia yaani kuanzia mwaka 1922 hadi mwaka 1999. Wawezeshaji ni pamoja na Mheshimiwa George Kahema Madafa, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Juvernalis Paul Baitu Rwelamila, kutoka SAUT.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, muasisi wa taifa la Tanzania ataendelea kukumbukwa na wengi ndani na nje ya Tanzania, kwa kusimamia misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu bila ubaguzi. Hata Tanzania ya wakati huu, na Afrika katika ujumla wake, ina kiu kubwa ya viongozi kama hawa wanaoweza kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya mafao ya wengi, badala ya kujikita katika uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka na kwamba uongozi unapaswa kutambuliwa kuwa ni dhamana na huduma kwa watu wa Mungu. Mwalimu Nyerere ni kiongozi aliyejipambanua kwa kujenga, kuimarisha na kutetea umoja wa taifa na muungano wa watanzania. Mwalimu Nyerere alisimamia harakati za mapambano ya kisiasa na ukombozi ndani ya Tanzania na kusini mwa Bara la Afrika. Alijitahidi kuimarisha mahusiano na mafungamano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi jirani, kwa kuzingatia misingi ya: haki, amani, utu na heshima ya binadamu.

Mwalimu Nyerere ni kiongozi aliyekazia maendeleo fungamani ya binadamu yanayozingatia mahitaji yake msingi: kiroho na kiutu; kwa kujikita zaidi katika: haki msingi za binadamu, utu na heshima yake na wala si maendeleo ya vitu, bali watu wenyewe wapewe kipaumbele cha kwanza! Huu ndio msingi wa maendeleo fungamani ya binadamu! Askofu mstaafu Paride Taban wa Jimbo Katoliki la Torit, Sudan ya Kusini anawachangamotisha viongozi wa Serikali na vyama vyama vya kisiasa nchini humo kuondokana na ukabila, ubinafsi, uchu wa mali na madaraka na badala yake, wajitoe bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Sudan ya Kusini, bila upendeleo wala ubaguzi. Askofu mstaafu Taban anasema, ukabila na udini ni sumu ya amani, maendeleo na ustawi wa wananchi wengi. Viongozi wa Serikali Sudan ya Kusini, wajitahidi kufuata mfano wa Mwalimu Julius Kambare Nyerere, Muasisi wa Tanzania aliyesimama kidete kulinda na kutetea umoja, upendo na mshikamano wa watu wake, kiasi kwamba, Tanzania ikajulikana kuwa ni "Kisiwa cha Amani". Kwake, ukabila na udini haukuwa na nafasi, mambo ambayo leo hii yanaendelea kusababisha maafa makubwa huko Sudan ya Kusini na sehemu mbali mbali za Bara la Afrika.

Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilichoko mjini Roma, Alhamisi tarehe 7 Novemba 2019 ni siku maalum iliyotengwa kwa ajili ya kumtafakari Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, miaka ishirini tangu alipofariki dunia yaani kuanzia mwaka 1922 hadi mwaka 1999. Kati ya wageni maarufu watakatoa mada ni pamoja na Mheshimiwa George Kahema Madafa, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Juvernalis Paul Baitu Rwelamila, kutoka SAUT, Tanzania anayepembua dhamana ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mkatoliki katika masuala ya kisiasa. Profesa Antoine de Padou Pooda amepewa fursa ya kumzungumzia Mwalimu Nyerere katika mchakato wa ujenzi wa nchi ya Tanzania. Profesa Angelo Romano anatarajiwa kudadavua kuhusu mchango wa Mwalimu Nyerere tangu wakati wa uhuru sanjari na mchakato wa ujenzi wa Umoja wa Afrika.

Askofu mkuu mstaafu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican, anawaalika watanzania kumuenzi Mwalimu kwa kuzingatia misingi ya haki, amani, umoja, mshikamano, utu, heshima na mafao ya wengi. Askofu mkuu Lebulu anasema, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ni kiongozi aliyejipambanua kwa moyo wa uzalendo, akasimamia haki, amani na mshikamano wa kitaifa. Ni kiongozi aliyewajali watu wake kiasi hata cha kuyasadaka maisha yake kwa ajili ya ustawi wa Watanzania na Afrika katika ujumla wake. Kwa Mwalimu uongozi kilikuwa ni kielelezo cha huduma. Askofu mkuu Lebulu anawataka watanzania kujibidisha zaidi katika kushughulikia masuala nyeti na tete yanayowagusa watanzania katika ujumla wao, kwa kutambua kwamba, kila mtu anawajibika mbele ya Mungu, kwa jinsi gani anavyojitoa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wengi, kwa kuweka misingi thabiti ya mustakabali wa taifa katika masuala ya haki na amani; umoja na mshikamano wa kitaifa, ili kujenga taifa linalojipambanua katika Jamii ya kimataifa kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Askofu mkuu Lebulu anakiri wazi kwamba, katika mchakato wa kutunga Katiba Mpya ya Tanzania, nchi imetikiswa katika msingi wake wa umoja na mshikamano wa kitaifa. Lakini watanzania wanapaswa kutambua kwamba, kipaumbele cha kwanza hakina budi kutolewa kwa ajili ya utu na heshima ya binadamu, mafao na maendeleo ya watanzania wote. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere awe ni mfano wa kuigwa katika kusimamia misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Kwa upande wake, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki la Iringa anasema kwamba, licha ya shida na mahangaiko yao, lakini wanafarijika kuona kwamba, Kanisa Katoliki nchini Tanzania linaendeleza mchakato wa kutaka Mtumishi wa Mungu Mwalimu Nyerere aweze kutangazwa na Mama Kanisa kuwa ni kati ya wenyeheri, kama kiongozi na mfano kwa wanasiasa na waamini walei, kutokana na upendo wake kwa Kristo na Kanisa lake, mambo msingi yaliyomwezesha kuishi na kutenda kama mwanasisa na akawa kweli ni mfano bora wa kuigwa na mataifa mengine!

Mchakato wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwamini mlei kutoka Jimbo Katoliki la Musoma, kuwa Mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu ulianzishwa na hayati Askofu Justin Samba, ukaboreshwa na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma na sasa umefikishwa Jimbo kuu la Dar Es Salaam, Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania! Mchakato unaendelea! Padre Alfred Stanslaus Kwene wa Jimbo Katoliki Musoma katika kumbukizi la miaka 20 tangu alipofariki dunia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema, “Kwa upande wa Mwl. J.K. Nyerere tunaamini na kutumaini kuwa yeye kama mkristo alitamani kufikia utakatifu na bidii yake yote kwa yale mazuri aliyoyafanya katika maisha yake ilikuwa ni kufikia azma hiyo – hivi kwamba ushuhuda juu ya maisha yake uliotakiwa kutolewa kama sharti msingi la kuruhusu mchakato kuanza uliweza kuleta ushawishi na Vatican kuridhia.

Kanisa bado halijamtangaza rasmi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa ni mtakatifu. Tunachoalikwa kufanya kwa ajili yake ni kusali ili utakatifu wake uweze kudhihirika wazi na hatimaye Kanisa siku moja liweze kumtangaza rasmi kuwa Mtakatifu.” Ikumbukwe kwamba, wito wa utakatifu wa maisha ni mwaliko kwa kila mwamini na kwamba, maisha ni zawadi na mali ya Mwenyezi Mungu na kwamba, binadamu amepewa dhamana ya kutunza tunu hii kubwa!  Chuo Cha Kumbu Kumbu ya Mwalimu Nyerere kilichoko nchini Tanzania,  tarehe 8 Oktoba 2019 kilifanya kongamano na kujadili kuhusu: urithi wa Mwalimu Julius Kambarege Nyerere katika uongozi, maadili, umoj, amani na ujenzi wa Taifa la Tanzania.

Mwl. J.K. Nyerere 2019

 

06 November 2019, 16:10