Chama cha Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo na mshikamano kwa maskini! Chama cha Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo na mshikamano kwa maskini! 

Chama cha Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki: Mashuhuda wa Injili

Chama cha Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia, RnS. kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 3 Novemba 2019 vinakutana huko mjini Rimini, Italia, ili kuadhimisha mkutano wao wa 43 unaosindikizwa na kauli mbiu “Watu wote watawatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yoh. 13:35): Kuinjilisha na kupendana”. Mashuhuda wa Injili ya Upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia, RnS., ni chombo madhubuti cha majadiliano ya kiekumene, yanayoliwezesha Kanisa Katoliki, kutembea bega kwa bega na waamini wa Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo; katika mchakato wa utekelezaji wa uekumene wa sala na huduma makini kwa maskini, na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kazi ya Roho Mtakatifu ni kuwafundisha na kuwaongoza waamini katika umoja unaofumbatwa kwenye utofauti. Roho Mtakatifu ni chemchemi ya uekumene wa sala, huduma, maisha ya kiroho sanjari na uekumene wa damu! Karama na utume wa Kanisa vinamwilishwa kwa namna ya pekee, katika maisha ya kijumuiya, kwa njia ya huduma makini kwa maskini ambao kimsingi ni amana, utajiri na walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu.

Ni kutokana na muktadha huu, vikundi na jumuiya za Chama cha Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia, RnS., kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 3 Novemba 2019 vinakutana huko mjini Rimini, Italia, ili kuadhimisha mkutano wao wa 43 unaosindikizwa na kauli mbiu “Watu wote watawatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yoh. 13:35): Kuinjilisha na kupendana”. Vikundi na jumuiya hizi zinapaswa kujizatiti zaidi katika toba na wongofu wa ndani, uponyaji wa mahangaiko wa watu, ili waweze kuwekwa huru kwa kuwapatia msaada wanaohitaji.  Vijielekeze zaidi katika ujenzi wa udugu, umoja, upendo na mshikamano ili kuanza kuchakarika katika hija ya maisha mapya!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam na matashi mema kwa wanachama wa Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia RnS., akionesha uwepo wake wa karibu kiroho. Kipindi hiki cha sala na tafakari, iwe ni fursa ya kujinyenyekesha kwa Roho Mtakatifu, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo, mwanga angavu unaong’aa na moto unaoangaza na kupasha joto; chumvi inayotoa ladha ya maisha na uzima wa milele; kielelezo makini cha nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu ulimwenguni. Baba Mtakatifu Francisko anawatakia heri na baraka kutoka kwa Roho Mtakatifu wanachama wote sanjari na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Anawaalika wao pia kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa njia ya sala na sadaka zao.

Parolin: Uamsho wa Kikatoliki
01 November 2019, 14:17