Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 13 Novemba 2019 amekutana na kuzungumza na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 13 Novemba 2019 amekutana na kuzungumza na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani.  (ANSA)

Askofu mkuu Justin Welby akutana na Papa Francisko: Sudan ya Kusini

Askofu mkuu Justin Welby kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani akiwa ameandamana na Askofu mkuu Ian Ernest, Mkurugenzi wa Kituo cha Kianglikan Roma na Mwakilishi wa Kanisa Anglikan mjini Vatican amekutana na Papa Francisko. Viongozi hawa wawili wamejadili kuhusu mustakabali wa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, migogoro ya kimataifa na hali tete nchini Sudan ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 13 Novemba 2019 alikutana na kuzungumza na Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani aliyekuwa ameandamana na Askofu mkuu Ian Ernest, Mkurugenzi wa Kituo cha Kianglikan Roma na Mwakilishi wa Kanisa Anglikan mjini Vatican. Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wawili wamejadili kuhusu mustakabali wa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, migogoro ya kimataifa na kwa namna ya pekee, hali tete ya kisiasa na kijamii inayoendelea kujitokeza nchini Sudan ya Kusini.

Kwa sasa Serikali ya Sudan ya Kusini, imetoa siku 100 ili kuanza kutekeleza Makubaliano ya Amani yaliyotiwa saini mjini Entebe, Uganda kama sehemu ya mchakato wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Baba Mtakatifu Francisko na Askofu mkuu Justin Welby wameonesha nia ya kutembelea Sudan ya Kusini kwa pamoja, Mwenyezi Mungu akiweka mkono wake, mwaka 2020, ingawa tarehe rasmi haijapangwa. Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Sudan ya Kusini, ilipaswa kuundwa tarehe 12 Novemba 2019, kadiri ya makubaliano yaliyofikiwa mwezi Septemba 2019, baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo na shinikizo kutoka Umoja wa Mataifa, Marekani na nchi za kikanda.

Askofu Mkuu Welby
14 November 2019, 09:47