Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia ni kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019: Kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani" Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia ni kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019: Kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani" 

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Maendeleo fungamani

Kanisa linataka kutangaza na kumshuhudia Kristo kuwa ni kiini cha maisha na wokovu wa walimwengu sanjari na kukabiliana na changamoto ya ekolojia fungamani. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele. Kiini cha maadhimisho ya Sinodi Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019: Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kujikita katika masuala ya haki, amani na mshikamano; utume na huduma ya upendo, ili kuhakikisha kwamba, Injili ya Kristo inatamadunishwa katika uhalisia wa maisha ya wananchi wa Amazonia, ili Kanisa liweze kupata sura mpya ya watu wa Amazonia kwa kuwa na: wakleri, watawa na waamini walei waliofundwa wakafundika barabara katika tunu msingi za Kiinjili! Hii ni changamoto inayohitaji ari, ujasiri na moyo wa kuthubutu, kwani kila jambo linawezekana mbele ya Mwenyezi Mungu. Kuna uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote na ukoloni mamboleo, unaofumbatwa katika nguvu ya kisiasa na kiuchumi inayotishia: ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Amazonia. Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia inapania pamoja na mambo mengine; kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji na kitume kwenye Ukanda wa Amazonia.

Kwa kukabiliana kwa dhati kabisa na uhaba mkubwa wa mihimili ya uinjilishaji wa kina, hali inayowafanya waamini wa Amazonia kukosa huduma makini na fungamani za kichungaji, kiasi hata cha kujisikia kwamba, wametelekezwa na Mama Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, utamadunisho ni mchakato unaolitajirisha Kanisa na kwamba, Kanisa linataka kuwajengea watu uwezo wa kupambana na hali pamoja na changamoto za maisha, ili siku moja Kanisa liweze kuwa na sura ya Amazonia inayofumbatwa na uwepo wa watu mahalia. Kanisa linataka kumtangaza Kristo Yesu kuwa ni kiini cha maisha na wokovu wa walimwengu sanjari na kukabiliana na changamoto ya ekolojia fungamani. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.

Hiki ndicho kiini cha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, Kardinali Claudio Hummes, Mwezeshaji mkuu wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia  ambaye pia Rais wa Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini, (Pan-Amazon Ecclesial Network of the Latin American Church, REPAM); pamoja na Askofu Fabio Fabene, Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu, Alhamisi, tarehe 3 Oktoba 2019 walipata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari ili kuwajuza mambo msingi katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wataendelea kuimarisha mafungamano ya kijamii, kimaumbile na mang’amuzi ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kanisa linapenda kukazia Injili ya upendo na mshikamano unaowashirikisha wananchi mahalia katika maamuzi na utekelezaji wa sera na mikakati yake. Kanisa linataka kutoa kipaumbele cha pekee katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ili kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kujikita katika sera na mikakati inayozingatia: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa linataka kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha na matumaini; kwa kujielekeza zaidi katika mchakato mzima wa uinjilishaji unaoifunda mihimili mikuu ya uinjilishaji na utamadunisho ili kweli Injili iweze kugusa, kuganga na kutakasa maisha ya watu mahalia, ili nao pia waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya: uhai, matumaini na huruma ya Mungu kwa waja wake!

Kardinali Lorenzo Baldisseri anafafanua kwamba, Sinodi hii ni maalum kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia ina wajumbe 184. Hawa ni wajumbe kutoka Tume ya Mawasiliano, Tume ya Utata, REPAM, Wawakilishi wa Majimbo Makuu ya Nchi za Ukanda wa Amazonia, Viongozi wakuu wa Mabaraza ya Kipapa. Katika orodha hii, kuna wajumbe walioteuliwa moja kwa moja na Baba Mtakatifu. Kuna wawakilishi kutoka Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Kuna wajumbe walioteuliwa kwa ajili ya maandalizi ya Sinodi; washiriki maalum, yaani wataalam. Baba Mtakatifu pia amewateua baadhi ya wakleri, watawa na waamini walei kuwa ni wasikilizaji. Kuna Makatibu wakuu wa Sinodi za Maaskofu, Wajumbe wa dini na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo pamoja na wageni maalum na kati yao kuna Dr. Ban Moon, Katibu mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa.

Kardinali Lorenzo Baldisseri anakaza kusema, tema iliyochaguliwa inaonesha umuhimu wa pekee wa Ukanda wa Amazonia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Kanisa linataka kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili zinazofumbatwa katika mchakato mzima wa utamadunisho sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Maadhimisho ya Sinodi hii yanapania pamoja na mambo mengine, kupunguza gharama za uendeshaji kwa kutumia bidhaa ambazo ni rafiki kwa mazingira na ekolojia fungamani mintarafu: mazingira, binadamu na jamii katika ujumla wake. Kwa upande wake, Kardinali Claudio Hummes, Mwezeshaji mkuu wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia katika hotuba yake amekazia kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kama mbinu mkakati wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na umaskini.

Sinodi inataka kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini, mambo ambayo ni sawa na chanda na pete. Ni wakati wa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, mambo msingi katika uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Uinjilishaji, utunzaji bora wa mazingira; Umuhimu wa Kanisa kujizatiti katika Injili ya uhai na matumaini; wongofu wa kiekolojia kwa kutambua, kuthamini na kuendeleza kazi ya uumbaji, ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu kuitunza. Wakati huo huo, Askofu Fabio Fabene, Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu amefafanua kanuni, taratibu na sheria mpya zilizopitishwa hivi karibuni katika Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanayowawezesha Maaskofu na waamini walei kutembea kwa pamoja katika imani, matumaini na mapendo. Maadhimisho haya yameboreshwa zaidi na Katiba ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko “Episcopalis Communio” yaani “kuhusu Sinodi za Maaskofu” iliyochapishwa mwezi Septemba 2018.

Ikumbukwe kwamba, Sinodi ni chombo cha uinjilishaji kinachofumbatwa katika ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza, kuadhimisha na kutenda kwa umoja. Hatua zote muhimu zimetekelezwa ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ushiriki mkamilifu wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazoni. Huu ni muda muafaka wa kusali, kutafakari na kushirikishana: uzoefu, mang’amuzi, vipaumbele na changamoto katika maisha na utume wa Kanisa Ukanda wa Amazonia. Sinodi itazinduliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu, itakayoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 6 Oktoba 2019 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katibu mkuu wa Sinodi atatoa hotuba elekezi katika maadhimisho ya Sinodi, Mwezeshaji mkuu atabainisha tema msingi zitakazojadiliwa na Mababa wa Sinodi; mchango binafsi wa Mababa wa Sinodi. Kutakuwepo pia kipindi cha majadiliano katika vikundi.

Makatibu wakuu maalum watashirikiana ili kuandaa Muswada wa Hati ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, utakaojadiliwa, kuboreshwa na hatimaye kupigiwa kura. Ujumbe wa Mababa wa Sinodi kwa ajili ya watu wa Mungu ni dhamana itakayotekelezwa na Baraza la Kipapa la Mawasiliano, ambalo kila siku litakuwa linatoa mrejesho wa maadhimisho ya Sinodi. Ili ujumbe uweze kuwafikia watu wengi zaidi, vyombo na mitandao mbali mbali ya kijamii itatumika , lakini Vatican News kutokana na uzoefu na historia yake, imepewa dhamana kubwa. Unaweza kutumia #sinodoAmazonico kwa lugha mbali mbali ili kupata kwa muhtasari yale yanayojiri katika Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Ili kuokoa matumizi ya karatasi, hotuba zote zitatolewa rasmi kwa njia ya mtandao.

Sinodi Amazonia
04 October 2019, 15:32