Tafuta

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 ni kipindi cha neema na baraka; ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa zima! Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 ni kipindi cha neema na baraka; ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa zima! 

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Ni Kipindi cha Neema!

Sinodi hii ni amana, utajiri na zawadi kubwa ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa Ukanda wa Amazonia. Inajikita katika wongofu wa shughuli za kichungaji, kimisionari, lakini pia ni Sinodi ambayo imejikita katika mchakato wa utunzaji wa mazingira nyumba ya wote, tema inayohitaji pia wongofu wa kiekolojia. Majadiliano ya kidini na kiekuemene ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019 yanaongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Hii ni Sinodi inayotoa kipaumbele cha pekee kwa mambo makuu manne: Shughuli za Kichungaji, Kitamaduni, Kisiasa na Kiekolojia; mambo yanayo ambatana na kukamilishana. Mababa wa Sinodi wanapaswa kupembua changamoto hizi kwa kutumia jicho ya Mitume wa Yesu. Sinodi hii ni amana, utajiri na zawadi kubwa ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa Ukanda wa Amazonia. Licha ya kujikita katika wongofu wa shughuli za kichungaji na kimisionari, lakini pia ni Sinodi ambayo imejikita kwa kiasi kikubwa na mchakato wa utunzaji wa mazingira nyumba ya wote, tema inayohitaji pia wongofu wa kiekolojia. Majadiliano ya kidini na kiekuemene ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Sinodi maana yake ni mchakato wa Kanisa kutembea kwa pamoja, “Kairos”, ili kujipatanisha na Ukanda wa Amazonia kwa kuendelea kujikita katika mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili; kwa kusimama kidete ili kukazia ekolojia fungamani.

Lengo la Sinodi hii ni kubainisha njia mpya za uinjilishaji Ukanda wa Amazonia, kwa kusikiliza na kujibu kwa ufasaha kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini; kwa kupembua matatizo, changamoto na fursa zilizopo ili kutoa mapendekezo yatakayofanyiwa kazi na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa muhtasari haya ndiyo mawazo makuu yaliyowasilishwa na Mababa wa Sinodi katika tafakari, majadiliano na mang’amuzi yaliyoibuliwa kwenye majadiliano ya vikundi vidogo vidogo, “Circoli Minori” vipatavyo 12 na kuwasilishwa kwenye Kikao cha 12 mbele ya uwepo na ushiriki wa Baba wa Mtakatifu Francisko. Mababa wa Sinodi wameonesha matumaini makubwa katika mchakato wa maendeleo fungamani Ukanda wa Amazonia kwa kuzingatia njia mpya ya Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu huko Amazonia. Nguzo msingi ya matumaini haya ni ari na mwamko mpya wa kimisionari unaolitaka Kanisa kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili, ili kuwajengea watu wa Mungu mazingira bora zaidi ya kuishi.

Hiki ni kipindi cha neema na baraka zitakazosaidia kumwilisha “Heri za Mlimani” muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu katika maisha ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Mwanga wa Neno la Mungu uwawezeshe watu wa Amazonia kupata utimilifu wa maisha. Mababa wa Sinodi katika taarifa za vikundi vyao, wametoa mapendekezo maalum yanayopaswa kufanyiwa kazi na Mama Kanisa katika ujumla wake. Hii inatokana na ukweli kwamba, changamoto msingi zinazoukabili Ukanda wa Amazonia zinafanana na zile zinazoyakabili Makanisa mengine, sehemu mbali mbali za dunia. Baada ya Mababa wa Sinodi kusoma na kukabidhi muhtasari wa taarifa za vikundi, “Circoli minori”, sasa maadhimisho ya Sinodi yanaanza kuingia katika kile kipindi cha “lala salama”. Hiki ni kipindi ambacho Sekretarieti kuu ya Sinodi inahariri na kupanga mapendekezo ya Mababa wa Sinodi yatakayopigiwa kura na hatimaye, kuwasilishwa kwa Baba Mtakatifu kwa ajili ya kufanyiwa tafakari na hatimaye, utekelezaji wake.

Mababa wa Sinodi wanajiandaa pia kutoa ujumbe wa Sinodi kwa Watu wa Mungu na hatimaye, kufunga Sinodi kwa Ibada ya Misa Takatifu. Huo utakuwa ni mwisho na mwanzo wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, kwani kilele cha maadhimisho haya ni Wosia wa Kitume kutoka kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mababa wa Sinodi wamekazia kuhusu maadhimisho ya: Ibada mbali mbali, Liturujia na Sakramenti za Kanisa zinazowasaidia waamini kukua na kukomaa katika imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake na hivyo kuwa tayari kujisadaka bila ya kujibakiza. Kuna uwezekano wa kuboresha shughuli za kichungaji kwa kuwatumia Mashemasi wa kudumu kama wanavyoelekeza Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na kuamsha ari na mwamko wa shughuli za kimisionari Ukanda wa Amazonia. Ikumbukwe kwamba, useja ni zawadi kubwa kwa Kanisa, changamoto inayohitaji malezi na majiundo makini kwa ajili ya wakleri pamoja na watawa.

Mababa wa Kanisa wanakumbusha kwamba, ndani ya Kanisa Katoliki kuna uwezekano wa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa kutumia madhehebu 23, kielelezo cha mchakato wa utamadunisho wa imani ya watu mahalia, kumbe, kuna uwezekano wa kuwa na Madhehebu ya Watu wa Ukanda wa Amazonia, ili kuliwezesha Kanisa kuthamini utamaduni, mila na desturi njema za watu wa Ukanda wa Amazonia. Hii ni sehemu muhimu sana ya uinjilishaji, utamadunisho na majadiliano ya kitamaduni. Kanisa halina budi kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu Ukanda wa Amazonia pamoja na kuendeleza mchakato wa kutunza mazingira nyumba ya wote. Kuna haja ya kukuza sera na mikakati inayozingatia uchumi shirikishi na fungamani unaokita mizizi yake katika kanuni ya auni, umoja na mshikamano. Mchakato huu utasaidia kuondokana na dhambi na madeni ya kiekolojia yanayopelekea wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; utumwa mamboleo unaonyanyasa utu na heshima ya binadamu pamoja na utamaduni wa kifo.

Elimu makini itakayowasaidia watu kupambana na hali pamoja na mazingira yao ni muhimu sana kwa vijana wa kizazi kipya. Kanisa halina budi kuendelea kuwekeza katika utume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Dhana ya Sinodi ndani ya Kanisa Katoliki kama ilivyoasisiwa na Mtakatifu Paulo VI ni kati ya viupaumbele vya Kanisa kwa wakati huu. Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia wanalitaka Kanisa kuanza kumwilisha dhana hii katika maisha ya Makanisa mahalia; Mabaraza ya Maaskofu; Mashirikisho ya Kanda hadi kufikia Kanisa la Kiulimwengu.  Kanisa linaendelea kupyaisha dhana ya Sinodi kwa kuwa na mbinu mpya iliyowashirikisha Mababa wengi wa Sinodi kwa kutoa nafasi zaidi kwa makundi madogo madogo, yajulikanayo kitaalamu kama “Circuli minori”. Mababa wa Sinodi wanaendelea kukazia siasa safi kama msingi wa maendeleo endelevu na fungamani Ukanda wa Amazonia. Demokrasia shirikishi na uongozi bora unaojikita katika hoja zenye mashiko na huduma kwa wananchi. Siasa safi inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi yanayowashirikisha wadau mbali mbali mbali katika jamii; marika pamoja na tamaduni, daima wakijitahidi kujenga imani kati yao kama sehemu ya kukuza na kudumisha amani. 

Baba Mtakatifu Francisko anasema, wazawa wanapaswa kuwa ndio wadau wakuu katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuwa karibu na familia ya Mungu Ukanda wa Amazonia, unaonyemelewa kwa kiasi kikubwa na ukoloni wa kiitikadi unaotaka kupekenya: utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi sanjari na kuharibu mazingira nyumba ya wote! Ukoloni wa kiitikadi unajikita katika sera na mikakati ya maendeleo isiyozingatia wala kuthamini: historia, utamaduni, utu na heshima yao. Ndiyo maana mapendekezo ya Mababa wa Sinodi yamezingatia: Shughuli za kichungaji, Kitamaduni, Kijamii, Kiekolojia na katika Maisha ya kiroho kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia.

Sinodi Kipindi cha Neema
21 October 2019, 09:54