Tafuta

Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia wameanza kuchangia hoja mbali mbali kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi hii. Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia wameanza kuchangia hoja mbali mbali kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi hii. 

Mababa wa Sinodi ya Amazonia waanza kuchangia hoja!

Majira ya jioni, vijana walipewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya ekolojia fungamani; umuhimu wa kulinda na kutunza vyanzo vya maji kama sehemu ya haki msingi za binadamu; athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na ongezeko la gesi ya ukaa; mchakato wa utamadunisho na hatimaye changamoto ya “Viri probati” yaani “wanaume waliooa kupewa Daraja Takatifu ya Upadre".

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019 yanaongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Baba Mtakatifu Francisko anasema, wazawa wa Ukanda wa Amazonia ndio wadau wakuu wanaopaswa kuandika historia ya wito na maisha yao. Mama Kanisa anataka kujizatiti zaidi katika mchakato wa haki unaofumbatwa katika huduma makini inayozingatia na kuheshimu ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, binadamu na mahitaji yake msingi akipewa kipaumbele cha kwanza! Kanisa linataka kujielekeza katika huduma inayokita mizizi yake katika utu na heshima ya wazawa wa Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu anasema hii ni Sinodi kwa ajili ya uinjilishaji na ekolojia fungamani; hija ya watu wa Mungu wanaotembea kwa pamoja ili kuweza kusimama kidete dhidi ya athari za ukoloni wa kiitikadi.

Mababa wa Sinodi wanasema, huu ni muda muafaka wa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama pamoja na kilio cha maskini Ukanda wa Amazonia kwa kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Sinodi hii inapania pamoja na mambo mengine kusoma alama za nyakati kwa kutambua hali halisi inayowakabili wananchi wa Ukanda wa Amazonia kukazia: uinjilishaji, utamadunisho na mwingiliano wa tamaduni katika mazingira ya Kimisionari na Kikanisa. Utume wa Kanisa unaotekelezwa na: Wakleri pamoja na nafasi ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni wakati wa kuibua sera na mbinu mkakati wa ekolojia fungamani mintarafu mazingira, uchumi, masuala ya kijamii na kitamaduni. Kanisa Ukanda wa Amazonia halina budi kusoma alama za nyakati tayari kuinjilisha mazingira ya mijini bila kusahau changamoto ya maji safi na salama kama sehemu ya haki msingi za binadamu.

Baada ya Sinodi kufunguliwa rasmi Jumapili tarehe 6 Oktoba kwa Ibada ya Misa Takatifu, Jumatatu 7 Oktoba kwa Maandamano kutoka Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican; wajumbe wamesikiliza hotuba elekezi pamoja na muhtasari “Instrumentum Laboris” yaani hati ya kutendea kazi. Majira ya jioni, vijana walipewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya ekolojia fungamani; umuhimu wa kulinda na kutunza vyanzo vya maji kama sehemu ya haki msingi za binadamu; athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na ongezeko la gesi ya ukaa; mchakato wa utamadunisho na hatimaye changamoto ya “Viri probati” yaani “wanaume waliooa kupewa Daraja Takatifu ya Upadre” ili kuongoza maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa.  Mababa wa Sinodi wamewachagua wajumbe wanne watakaohusika na mchakato wa kuandaa Hati ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.

Wajumbe wengine watatu, watateuliwa moja kwa moja na Baba Mtakatifu Francisko, ili kukamilisha Sekretarieti kuu ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia inayoundwa na Kardinali Lorenzo Baldisseri, Kardinali Claudio Hummes, Askofu Mario Grech pamoja na Kardinali Michael Czerny na Askofu David Martinez de Agguirre Guinea, Makatibu wakuu maalum wa Sinodi. Mababa wa Sinodi wamewachagua pia wajumbe wa Tume ya Mawasiliano wanaokamilisha Tume inayoongozwa na Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano. Mababa wa Sinodi wameendeleza changamoto iliyotolewa na vijana wakati wa Maadhimisho ya Sinodi ya Vijana kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya vijana wanaoendelea kujipambanua katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama ilivyo kwa kijana Greta Thunberg.

Kuna umuhimu kwa Jumuiya ya Kimataifa kujadiliana na vijana wa kizazi kipya kuhusu sera na mikakati ya utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Vijana wa kizazi kipya ni sehemu ya vinasaba vya Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini wanaoteseka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Majadiliano yasaidie kutoa mwelekeo sahihi katika maisha ya vijana, ili changamoto ya mazingira isiwe tu ni uragibishaji bali sehemu muhimu sana ya maisha yao halisi. Mababa wa Sinodi wamekazia umuhimu wa kulinda na kutunza vyanzo vya maji kama sehemu ya haki msingi za binadamu. Kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji unaofanywa na Makampuni makubwa, kiasi cha kutishia maisha ya wananchi mahalia kukosa maji safi na salama, hali inayoweza kusababisha kuibuka kwa magonjwa kwa siku za usoni.

Kumbe, kuna haja ya kulinda mila, desturi na tamaduni za watu sanjari na kujielekeza katika njia mpya za uinjilishaji. Katika muktadha kama huu, haki msingi za binadamu, utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi ni mambo ambayo yanapaswa pia kuvaliwa njuga, ili kuendeleza ekolojia fungamani, inayoweka uwiano sawia kati ya binadamu na mazingira yake. Mababa wa Sinodi wanasema, utunzaji bora wa mazingira ni dhamana ya wote, kwa sababu mazingira bora ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Umefika wakati wa kuachana na teknolojia inayozalisha hewa ya ukaa, hasa kwenye Nchi zilizoendelea zaidi, na hivyo kuanza mchakato wa kuelekea katika matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira. Ukoloni mamboleo hauna tena nafasi tena, watu waheshimiwe na kuthaminiwa.

Kanisa linataka kujielekeza zaidi katika mchakato wa kuheshimiana, kuthaminiana na kukamilishana, kama sehemu ya mchakato wa utamadunisho na uinjilishaji, kama inavyojionesha katika maisha ya wakleri na watawa. Kristo Yesu ni kiini cha utamadunisho na Roho Mtakatifu ni mhusika mkuu wa mchakato wa utamadunisho kumbe, Kanisa linawajibika kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili; kwa kusimama kidete ili kukazia ekolojia fungamani. Mama Kanisa anaweza kuanza kufanya majaribio ya tamaduni, mila na desturi njema kutoka kwa watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia, kwa kuzingatia mang’amuzi sahihi ya kitaalimungu, kiliturujia na katika shughuli za kichungaji. Ibada ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia, utawasaidia waamini hao kumwilisha kikamilifu imani yao katika uhalisia wa maisha.

Changamoto ya “Viri probati” yaani “wanaume waliooa kupewa Daraja Takatifu ya Upadre” ili kuongoza maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa ni kati ya changamoto kubwa zinazowakabili Mababa wa Sinodi kwa wakati huu. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna baadhi ya watu kwa makusudi mazima, wanataka kupotosha mchakato wa majadiliano haya, kwa kuwaaminisha watu kwamba, Kanisa tayari limekwisha kutoa maamuzi ya “kuachana na useja”. Mababa wa Sinodi wanasema kwamba, Kanisa linaendeleza Mapokeo yake na wala hakuna sababu msingi ya kubadilisha asili ya Sakramenti ya Daraja Takatifu na uhusiano pamoja na mafungamano yake na Useja kama unavyobainishwa kwenye Madhehebu ya Kilatini. Wazo lililopo kwa sasa ni kuwahamasisha vijana wazawa kutoka Ukanda wa Amazonia, kuweza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji na pale inapowezekana wasadake maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake, ili kusiwepo Makundi ya waamini wa Kanisa Katoliki, “Kundi A” waliobahatika kupata Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na wale wa “Kundi B” ambao wataendelea kukosa Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. 

Sinodi Amazonia
08 October 2019, 15:38