Tafuta

Mababa wa Sinodi wanasema, kiundwe kikosi kazi kwa ajili ya dhamana na utume wa kuinjilishaji na kutamadunisha Injili. Mababa wa Sinodi wanasema, kiundwe kikosi kazi kwa ajili ya dhamana na utume wa kuinjilishaji na kutamadunisha Injili. 

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Kikosi kazi cha uinjilishaji

Mababa wa Sinodi wametakiwa kuwa na imani thabiti kwa Roho Mtakatifu na kamwe wasitawaliwe na woga wa kukosea katika maamuzi yao. Kanisa Ukanda wa Amazonia linaitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Bado kuna umati mkubwa wa watu wasiomfahamu Kristo Yesu, kumbe uinjilishaji ni dhamana endelevu kabisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019 yanaongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Hii ni Sinodi inayoadhimishwa kwa kuzingatia mambo makuu manne: Shughuli za Kichungaji, Kitamaduni, Kisiasa na Kiekolojia; mambo yanayo ambatana na kukamilishana kwa sababu ni sehemu ya vinasaba vya ekolojia fungamani. Hadi sasa Mababa wa Sinodi wamepembua kwa kina na mapana kuhusu: Utumwa mamboleo na changamoto ya toba na wongofu wa kiekolojia; Dhamana ya uinjilishaji na utamadunisho; Dhana ya Sinodi, ari na mwamko wa kimisionari katika maisha na utume wa Kanisa. Mababa wa Sinodi wamegusia changamoto za maisha, wito na utume wa Kipadre; njia mpya ya “Viri probati” kama wazo la kuwashirikisha watu wa ndoa katika Daraja Takatifu ya Upadre, ili kusaidia mchakato wa maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.

Mababa wa Sinodi wamekazia zaidi umuhimu wa Kanisa kuendelea kuhamasisha Ibada mbali mbali kama chemchemi ya maboresho ya maisha ya kiroho na kiutu miongoni mwa watu wa Mungu. Mababa wa Sinodi wanasema, umefika wakati kwa watu wa Mungu kujifunza kwa makini taalimungu ya Kazi ya Uuumbaji ili kujikita katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mababa wa Sinodi bado wanaendelea kukazia umuhimu wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa; Majadiliano ya kidini na kiekumene ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Ukanda wa Amazonia ni amana na utajiri wa watu wote wa Mungu na wala si mali ya mtu binafsi anayeweza kuibinafsisha kama anavyotaka mwenyewe! Mababa wa Sinodi katika kikao chake cha nane, Jumamosi jioni tarehe 12 Oktoba 2019, wamehitimisha juma la kwanza la: Majadiliano, tafakari, mang’amuzi na vipaumbele vya Mama Kanisa katika maisha na utume wake Ukanda wa Amazonia.

Mababa wa Sinodi wametakiwa kuwa na imani thabiti kwa Roho Mtakatifu na kamwe wasitawaliwe na woga wa kukosea katika maamuzi yao. Kanisa Ukanda wa Amazonia linaitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kiini cha Habari Njema ya Wokovu! Inasikitisha kuona kwamba, bado kuna umati mkubwa wa watu wasiomfahamu Kristo Yesu, kumbe, dhamana na utume wa Kanisa ni kuendelea kutangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka sehemu mbali mbali za dunia. Ili kutekeleza dhamana hii, kuna haja ya kuunda kikosi kazi kitakachowezeshwa kuwa nyenzo msingi ili kuweza kukabiliana mubashara na changamoto mamboleo zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa, ili hatimaye, kushuhudia furaha ya uinjilishaji mpya inayokita mizizi yake katika uhalisia wa maisha ya watu. Njia mpya ya “Viri probati” kama wazo la kuwashirikisha watu wa ndoa katika Daraja Takatifu ya Upadre ni tema ambayo imejitokeza tena na tena. Mababa wa Sinodi wamekumbusha kwamba, uhaba wa miito ni changamoto fungamani ya Kanisa zima na wala hakuna sababu msingi ya kufanya upendeleo wa pekee kwa Ukanda wa Amazonia kwa kuambata njia mpya ya “Viri probati”.

Kama changamoto hii inaonekana kwa Kanisa kuwa ni mtambuka, basi kuna haja ya kushauri maadhimisho ya Sinodi itakayojikita zaidi katika uhaba wa miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Kila tamaduni zinatambua maana na kuambata useja pamoja changamoto zake. Inasikitisha kuona kwamba, walimwengu wengi wanadhani kwamba, useja wa maisha kipadre na kitawa ni ngome inayopaswa kuvunjiliwa mbali, kwani watu wanadhani kwamba, maisha ya binadamu ni kula na kunywa tu pasi na sadaka wala majitoleo. Baadhi ya Mababa wa Sinodi wamesikika wakisema kwamba, “njia mpya ya Viri probati” si njia mbadala na badala yake, Kanisa lijenge utamaduni wa wongofu wa kichungaji, kwa kushirikishana wahudumu wa Injili. “Viri probati” ni mtazamo unaoweza kuleta mpasuko mkubwa katika maisha na wito wa kipadre, kwa kushindwa kuona na kutambua sadaka ya maisha ya useja ndani ya Kanisa. Utambulisho wa Kanisa Ukanda wa Amazonia utoe upendeleo wa pekee kwa wazalendo, ingawa baadhi ya Mababa wa Sinodi wanasema, kuna haja kwa Kanisa kujizatiti katika imani kwa uwepo na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu badala ya kugubikwa na wasi wasi wa kukosea katika maamuzi kuhusu utambulisho wa Kanisa Ukanda wa Amazonia.

Wanawake ni mihimili ya ujenzi wa Kanisa na Jamii katika Ukanda wa Amazonia na Amerika ya Kusini katika ujumla wake. Injili ya Kristo iwe ni mwongozo rejea katika majadiliano ya kuwajengea uwezo wanawake kwani, Kristo Yesu aliwajali na kuwathamini sana wanawake, akawapatia uhuru wa kushiriki katika maisha na utume wake, kiasi hata cha kuwa ni mashuhuda wa Fumbo la Ufufuko, kiini cha imani na maisha ya Kanisa. Alijali na kuthamini utu na heshima yao kama binadamu. Baadhi ya Mababa wa Sinodi wameelezea uwezekano wa Kanisa Ukanda wa Amazonia kuibua na kudumisha pia Mashemasi wanawake, ili washiriki katika huduma kwa watu wa Mungu, pengine, dhana hii itaweza kusaidia kupambana na mfumo dume uliokomaa ndani ya Kanisa. Wanawake wajengewe uwezo wa kushiriki katika vikao mbali mbali vya maamuzi na utekelezaji wa sera na mikakati ya maisha na utume wa Kanisa mahalia. Wanawake wameendelea kujipambanua kuwa ni vyombo na mashuhuda wa: mshikamano, upatanisho, haki na amani sehemu mbali mbali za dunia. Inaonekana kana kwamba, mfumo dume ndani ya Kanisa ni chanzo cha kudumaza huduma za Kiinjili, udugu wa kibinadamu na mshikamano wa dhati.

Roho Mtakatifu ndiye anayewafundisha waamini kumwita Kristo Yesu kuwa ni Bwana, mwaliko ni kumsikiliza kwa makini, ili hatimaye, kumtangaza na kumtolea Yesu ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Waamini wanapaswa kumfungulia Roho Mtakatifu malango ya akili na nyoyo zao, ili kusikiliza wosia ambao Yesu mwenyewe aliwaachia Mitume wake alipowaambia kwamba, kamwe hata waacha yatima, atawapelekea Roho wa kweli, Msaidizi ambaye ni Roho Mtakatifu Mfariji na mtetezi wao mbele ya Mwenyezi Mungu. Huu ni wosia ambao Yesu mwenyewe aliwapatia wafuasi wake wakati wa Karamu ya mwisho. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, iwe ni fursa ya kumsikiliza Roho Mtakatifu, kwa kufanya toba na wongofu wa kiekolojia, kimisionari na katika shughuli za kichungaji. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Ukanda wa Amazonia unakuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kuliko ilivyo kwa wakati huu. Uchafuzi na uharibu wa mazingira Ukanda wa Amazonia ni hatari kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa familia kubwa ya binadamu.

Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha utandawazi wa upendo na mshikamano; utandawazi unaojali utu, heshima na haki msingi za binadamu dhidi ya ubinafsi, uchoyo na watu kutaka kumezwa na malimwengu. Ni ubinafsi wa kutaka faida kubwa na kwa haraka kwa hasara ya maisha ya wazalendo Ukanda wa Amazonia. Wongofu wa kielojia, maisha yasiyokuwa na makuu; sera na mikakati ya uchumi fungamani ni muhimu kwa Ukanda wa Amazonia. Watawa wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume wakumbuke kwamba, wanasukumwa na imani thabiti, na mapendo kwa Mungu na kwa jirani, na upendo kwa Msalaba, na matumaini katika utukufu ujao, kueneza popote duniani Habari Njema ya Wokovu, kusudi ushuhuda wao uonekane mbele ya watu wote na Baba yao aliye mbinguni apate kutukuzwa. Umefika wakati kwa Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume kuwa na sura ya watawa kutoka Ukanda wa Amazonia.

Ni wakati wa kugundua mbegu ya Neno la Mungu iliyofichika katika maisha, tamaduni, mila na desturi njema za watu wa Ukanda wa Amazonia. Watambue uwepo wa Kristo Mfufuka kati yao na kwamba, anataka kuwashirikisha ile furaha ya Injili. Sura ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia ndani ya Kanisa mintarafu maisha ya kitawa inapaswa kujikita katika uinjilishaji, utamadunisho na mwingiliano wa tamaduni katika mazingira ya Kimisionari na Kikanisa. Ni kwa njia hii, Kanisa litaweza kuwa na utambulisho wake kadiri ya muktadha wa Ukanda wa Amazonia. Lakini, ikumbukwe kwamba, kumekuwepo na watawa wa mashirika mbali mbali wanaoendelea kujizatiti katika kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za wananchi wa Ukanda wa Amazonia. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kujikita katika malezi na majiundo makini, ili tamaduni, mila na desturi njema ya watu wa Ukanda wa Amazonia ziweze kukita mizizi yake katika tasaufi ya Kikristo na hivyo kuendeleza ekolojia fungamani kwa ajili ya ulinzi wa binadamu na utunzaji bora wa mazingira.

Sinodi Kikao cha 8
14 October 2019, 10:27