Hati ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia 2019: Amazonia: Njia Mpya ya Kanisa na kwa Ajili ya Ekolojia Fungamani Hati ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia 2019: Amazonia: Njia Mpya ya Kanisa na kwa Ajili ya Ekolojia Fungamani 

Hati ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia 2019

Hati hii inabainisha hija ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Baada ya kusikiliza kwa makini, sasa ni wakati wa kujikita katika wongofu wa kiekolojia, shughuli za kichungaji, kitamaduni pamoja na wongofu wa Kisinodi. Kanisa limeangalia pia njia mpya za wongofu Ukanda wa Amazonia pamoja na kutoa hitimisho la Hati ya Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6 - 27 Oktoba, 2019 yameongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Mababa wa Sinodi wamepitia, wakajadili na hatimaye wakapigia kura vipengele vyote na kupitisha Hati ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwa Mwaka 2019. Hati hii inaongozwa na kauli mbiu “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani”. Hati hii ina kurasa 30 zenye sura tano pamoja na utanguzi unaobainisha hija ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Baada ya kusikiliza kwa makini, sasa ni wakati wa kujikita katika wongofu wa kiekolojia, shughuli za kichungaji, kitamaduni pamoja na wongofu wa kiekolojia. Kanisa limeangalia pia njia mpya za wongofu Ukanda wa Amazonia pamoja na kutoa hitimisho la Hati ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.

Utangulizi: Hati hii inabainisha hija ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia ambao una umuhimu katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu. Uchafuzi na uharibifu wa mazingira Ukanda wa Amazonia unaweza kugeuka kuwa ni maafa makubwa ulimwenguni. Sinodi imekazia umuhimu wa kusikiliza, kuamua na kutenda kadiri ya nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu anayeliongoza Kanisa katika njia mpya. Uwepo wa Kanisa Ukanda wa Amazonia mintarafu mchakato wa uinjilishaji unapaswa kujikita katika majadiliano na utamadunisho ili hatimaye, kuziinjilisha tamaduni sanjari na kuitamadunisha Injili; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea, kudumisha utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kama sehemu ya ekolojia fungamani.

Sura ya kwanza: Amazonia: Kutoka Kusikiliza na Kuelekea kwenye Wongofu fungamani. Mababa wa Sinodi wamesikiliza sauti na wimbo wa Amazonia kama ujumbe wa zawadi ya uhai inayopaswa kulindwa, kudumishwa na kuendelezwa. Umefika wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha maskini wanaotishiwa na uchafuzi na uharibifu wa mazingira. Matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Ukanda wa Amazonia ni ufunuo wa Uso wa Kristo ambaye ni maskini, mwenye njaa na mgeni asiyekuwa na makazi maalum. Hawa ni watu wanaonyanyaswa na kudhulumiwa utu, heshima na haki zao msingi kutokana na athari za utumwa mamboleo, biashara ya binadamu na viungo vyake; mambo yanayohitaji sera makini za shughuli za kichungaji. Kanisa Ukanda wa Amazonia katika mchakato wa uinjilishaji wa kina limekuwa mstari wa mbele kusikiliza kilio cha maskini na hata baadhi ya wamisionari wake waliyamimina maisha kwa kulinda utu wa watu mahalia. Lakini Kanisa kwa upande mwingine, lilishirikiana na wakoloni, hali ambayo ilitia doa katika maisha ya jumuiya za Wakristo. Sasa ni wakati wa kuondokana na ukoloni wa kiitikadi, kwa kujikita katika majadiliano ya kitamaduni. Kwa hakika wamisionari wengi wameandika ukura wa utukufu wa Kanisa Ukanda wa Amazonia kwa njia ya damu yao! Huu ni wakati wa wongofu fungamani unaowataka watu wa Mungu kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kukazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa na hatimaye, kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika maisha ya watu.

Sura ya Pili: Njia Mpya za Wongofu wa Kichungaji. Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia wanakazia njia ya umisionari kwa kutambua kwamba, Kanisa linapaswa kuwa ni kielelezo cha Msamaria mwema, chemchemi ya huruma na mshikamano wa dhati. Kanisa liendelee kujielekeza zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa linapaswa kuwasindikiza watu wa Mungu katika hija ya kimisionari kwa kutambua na kuheshimu utu wa wazalendo na kwamba, Kanisa linapambwa pia kwa nyuso za wahamiaji pamoja na vijana wa kizazi kipya. Hii ni changamoto kwa Kanisa kujiekeleza zaidi katika shughuli za uinjilishaji mijini kwa kukazia demokrasia shirikishi, maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na haki jamii. Huu ni wakati wa kukuza na kudumisha tasaufi ya kusikiliza na kutangaza, kwa kuendelea kujikita katika wongofu wa shughuli za kichungaji.

Sura ya Tatu: Njia Mpya ya Wongofu wa Kitamaduni. Kanisa Ukanda wa Amazonia linawajibika kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili; kwa kusimama kidete katika wongofu wa kitamaduni unaothamini tamaduni, mila na desturi njema za watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Mama Kanisa hana budi kushikamana na kuungana na watu wa Ukanda wa Amazonia, kwa kulinda: utu, heshima na haki zao msingi. Utamadunisho ni sehemu ya mchakato wa umwilisho wa tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya watu. Watu mahalia wakisindikizwa na viongozi wao wa Kanisa ndio wahusika wakuu katika mchakato wa utamadunisho unaopaswa kushuhudiwa katika Ibada na kwa njia ya Katekesi makini; huku waamini walei wakishiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa ili kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda makini. Mafumbo yanayoadhimishwa na Mama Kanisa hayana budi kutamadunishwa kwa kuzingatia taalimungu; kwa kulinda na kuheshimu haki msingi za binadamu sanjari na kuendeleza majadiliano ya kitamaduni katika ulimwengu mamboleo.

Changamoto za huduma bora za afya, elimu na mawasiliano hazina budi kuvaliwa njuga na kuimarishwa zaidi ili kuwajengea watu utamaduni wa kukutana, kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ili kuweza kufikia lengo hili, kuna haja ya kuwekeza zaidi katika elimu ya mawasiliano kwa wazawa ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari na wongofu wa kiekolojia. Wanafunzi wafundishwe lugha mbali mbali ili kusaidia mwingiliano wa tamaduni, dhamana inayoweza kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa na Taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu vilivyoko kwenye Ukanda wa Amazonia.

Sura ya Nne: Njia Mpya za Wongofu wa Kiekolojia, ili kuwawezesha watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia kupata utimilifu wa maisha. Sura hii inatajirishwa kwa kiasi kikubwa na tafakari kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Inagungumzia athari zinazotishia Ukanda wa Amazonia na watu wake; changamoto za mitindo mipya ya maisha; mshikamano na umuhimu wa kujikita katika sera na mikakati ya maendeleo fungamani yanayokidhi mahitaji muhimu ya watu wa Ukanda wa Amazonia. Kanisa halina budi kusimama kidete; kulinda na kutetea mazingira nyumba ya wote kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika masuala ya kijamii na mazingira; kwa kukazia kanuni na tunu msingi za maadili na utu wema, ili kweli maendeleo yaweze kuwa ni shirikishi kwa wote.

Kanisa halina budi kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kuhakikisha kwamba, haki ya watu kupata maji safi na salama inatekelezeka. Kanisa halina budi kujitambulisha kuwa ni maskini kwa ajili ya maskini pamoja na maskini kwani hawa ni amana na utajiri wake. Kimsingi Kanisa katika mchakato wa wongofu fungamani linapaswa kuwa ni sauti ya kinabii na chemchemi ya Injili ya matumaini na mshikamano kati ya watu wa Mungu. Sera na mipango ya shughuli za kichungaji Ukanda wa Amazonia zinapaswa kusimamiwa na kuratibiwa na: Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, “Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini”, (Pan-Amazon Ecclesial Network of the Latin American Church, REPAM, Shirika la Misaada ya Kanisa Katoliki, Caritas, CLAR, Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kitaifa, Taasisi za Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu pamoja na kuhakikisha kwamba, Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu linakuwa na kitengo maalum kwa ajili ya maendeleo Ukanda wa Amazonia, ili kuharakisha maendeleo.

Sura ya Tano: Njia Mpya za Wongofu wa Kisinodi, ili wote waweze kuwa wamoja kwa kujikita katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu mchakato wa shughuli za kimisionari kwa ajili ya watu wa Mungu chini ya uongozi na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu. Watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia wanapaswa kuonesha na kushuhudia umoja wao kama ilivyokuwa kwa Mtaguso wa Yerusalemu. Mfumo na mtindo wa maisha na utume wa Kanisa unapaswa kujielekeza zaidi kama sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Wahudumu wa Kanisa na Mihimili Mipya ya uinjilishaji ni changamoto kwa Kanisa Ukanda wa Amazonia, ili kusoma alama za nyakati. Kuna watawa wanaoendelea kujisadaka katika huduma mbali mbali Ukanda wa Amazonia, changamoto na mwaliko ni kuhakikisha kwamba, Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume yahamasisha zaidi miito ya kipadre na kitawa miongoni mwa watu mahalia. Wanawake wanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa, vinginevyo Kanisa litakuwa tasa! Ili kukuza na kudumisha huduma kwa ajili ya Jumuiya mbali mbali za Kikristo Ukanda wa Amazonia kuna haja ya kukazia uwepo wa Mashemasi wa Kudumu. Hawa waandaliwe kiasi kwamba, wanaweza kusaidia mchakato wa ekolojia na maendeleo fungamani ya binadamu; huduma za kijamii kwa kuendelea kufunua Uso wa Kanisa linalojikita katika huduma kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema. Utambulisho wa Kanisa hauna budi kujikita katika Huduma makini! Dhamana na wito huu unahitaji majiundo na malezi endelevu yanayofumbatwa katika mchakato mzima wa utamadunisho!

Mababa wa Sinodi wanasema Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha umoja Kisinodi. Ni kielelezo cha umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa; ni chemchemi na hitimisho la uinjilishaji na kwamba, Kanisa linaishi na kumudu kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Waamini wanapaswa kurutubisha maisha yao kwa kujichotea nguvu, neema na baraka kutoka katika maadhimisho ya Ekaristi Takatifu. Maadhimisho haya ni kiini pia cha ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, kujipatanisha, kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu; ni mahali panapoiwezesha jumuiya kukua na kustawi. Kanisa linatambua na kuthamini sana zawadi ya Useja, unaowawezesha wakleri na watawa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Useja ni sehemu ya nidhamu ya Daraja Takatifu na wala si asili yake. Tofauti katika maisha ya Useja ndani ya Kanisa hauna madhara kwa umoja wa Kanisa.

Mababa wa Sinodi wanasema katika muktadha wa jukumu la kutakatifuza, Maaskofu kwa njia ya sala na kazi kwa ajili ya watu, wana mimina ukamilifu wa utakatifu wa Kristo kwa namna mbali mbali na kwa wingi. Kwa huduma ya Neno wanawashirikisha waamini uweza wa Mungu uletao wokovu na kwa njia ya Sakramenti wanawatakatifuza waamini. Ni katika mwanga wa Hati ya Fumbo la Kanisa, LG. Namba 26 Mababa wa Sinodi wanaomba wanaume walioshuhudia ufanisi katika Ushemasi wa kudumu wapewe Daraja Takatifu ya Upadre baada ya kukamilisha malezi na majiundo ya Daraja Takatifu ya Upadre. Lengo ni kusaidia kuenzi maisha ya jumuiya za Kikristo kwa kutangaza, kushuhudia na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa katika maeneo ya mbali vijijini. Mababa wa Sinodi wanasema, wongofu wa Kisinodi unahitaji pia uwepo wa miundo mbinu kwa kuanzisha Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ukanda wa Amazonia kitakachojikita katika mchakato wa: Uinjilishaji na utamadunisho; Malezi na majiundo ya Kipadre; tafiti na masomo ya kitamaduni. CELAM na REPAM ziwe ni vielelezo vya dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa Ukanda wa Amazonia. Mababa wa Sinodi wanashauri iwepo Ibada kwa ajili ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia.

HITIMISHO: Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, wanahitimisha Ujumbe wao kwa kuuwela chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Amazonia, anayeheshimiwa na waamini wa Ukanda huu kwa majina mbali mbali. Kwa maombi na sala zake, asaidie maadhimisho ya Sinodi hii kuwa ni alama hai ya dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, ili watu kwa njia ya Kristo Yesu, waweze kupata utimilifu wa maisha. Bikira Maria aendelee kusindikiza safari ya Amazonia, na Mtakatifu Yosefu, Baba na Mlinzi wa Familia Takatifu waendelee kubariki uwepo wa Kanisa Ukanda wa Amazonia, kwa kuliwezesha Kanisa kuwa na sura ya watu wa Amazonia kama sehemu ya safari yake ya kimisionari!

Hati ya Sinodi Amazonia 2019

 

27 October 2019, 13:02