Tafuta

Vatican News
Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia inaendelea kurindima mjini Vatican kwa kupembua changamoto, matatizo na fursa mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia inaendelea kurindima mjini Vatican kwa kupembua changamoto, matatizo na fursa mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa.  (Vatican Media)

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Vijana & Dawa za Kulevya!

Tema zilizojadiliwa: Utumwa mamboleo na changamoto ya toba na wongofu wa kiekolojia; Dhamana ya uinjilishaji na utamadunisho; Dhana ya Sinodi, ari na mwamko wa kimisionari; changamoto za maisha, wito na utume wa Kipadre; njia mpya ya “Viri probati”. Umuhimu wa Kanisa kuhamasisha Ibada mbali mbali; majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kwa ajili ya mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019 yanaongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Hii ni Sinodi inayoadhimishwa kwa kuzingatia mambo makuu manne: Shughuli za Kichungaji, Kitamaduni, Kisiasa na Kiekolojia; mambo yanayo ambatana na kukamilishana kwa sababu ni sehemu muhimu ya ekolojia fungamani. Mababa wa Sinodi wameendelea kuchangia hoja mbali mbali kama zilivyobainishwa kwenye Hati ya Kutendea Kazi, “Instrumentum Laboris”. Siku ya Jumanne, tarehe 8 Oktoba 2019, mada zilizojadiliwa ni pamoja na: Umaskini wa hali na kipato unavyopekenya hata maisha ya kiroho. Dhambi za kiekolojia na madhara yake katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Changamoto ya utakatifu wa maisha na wito wa kipadre; Uwajibikaji wa pamoja; haki msingi za binadamu; Mashemasi wa kudumu Ukanda wa Amazonia pamoja na umuhimu wa kuwahamasisha vijana kuwa watakatifu hata katika ujana wao.

Siku ya Jumatano, tarehe 9 Oktoba 2019, kwa uwepo na ushiriki mkalimifu wa Baba Mtakatifu Francisko, Mababa wa Sinodi wamepembua kwa kina mapana kuhusu: Utumwa mamboleo na changamoto ya toba na wongofu wa kiekolojia; Dhamana ya uinjilishaji na utamadunisho; Dhana ya Sinodi, ari na mwamko wa kimisionari; changamoto za maisha, wito na utume wa Kipadre; njia mpya ya “Viri probati”. Umuhimu wa Kanisa kuhamasisha Ibada mbali mbali kama chemchemi ya maboresho ya maisha ya kiroho. Umefika wakati kwa watu wa Mungu kujifunza kwa makini taalimungu ya Kazi ya Uuumbaji ili kujikita katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mababa wa Sinodi bado wanaendelea kukazia umuhimu wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa; Majadiliano ya kidini na kiekumene ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Ukanda wa Amazonia ni amana na utajiri wa watu wote wa Mungu na wala si mali ya mtu binafsi. Baba Mtakatifu Francisko pia amechangia maoni yake!

Uzalishaji, usambazaji, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni janga kubwa Ukanda wa Amazonia, changamoto ya kupambana fika na janga hili kwa kujikita katika ujenzi wa misingi ya haki; kwa kuwaelimisha vijana maana na tunu msingi za maisha ya pamoja, sanjari na kuendelea kuwasaidia walioathirika na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Huduma hii ifanywe kwa upendo wa Kristo, kwa kujifunza kuwakumbatia wenye shida na mahangaiko, kwa kuwaonesha ukaribu, huruma na upendo. Mababa wa Sinodi anawahimiza waamini na watu wenye mapenzi mema, kuwasaidia kwa hali na mali wale waliotumbukia katika matumizi haramu ya dawa za kulevya, ili waweze kuwa na ujasiri wa kusimama tena, wakionesha nia na utashi wa kufanya hivyo. Kila mtu anawajibika katika maisha yake, jambo la msingi ni kuwa na ujasiri wa kutenda na hapo mtu anaweza kupata msaada. Vijana katika hali kama hii, kamwe wasijisikie pweke, kwani Kanisa na watu wenye mapenzi mema, wanaendelea kufanya hija pamoja nao katika shida na mahangaiko yao ya ndani; wao wanapaswa kuwa ni watu wenye matumaini na kamwe, wasiache tumaini hili kuporwa na wajanja wachache.

Kila mwamini awe ni chombo cha matumaini kwa jirani yake. Mikakati na sera za mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya hazina budi kuzingatia maisha ya mwanadamu ambayo kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, mwanadamu: roho na mwili anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Vijana ni rasilimali watu inayohitajika kwa ajili ya maendeleo fungamani kwa sasa na kesho iliyo bora zaidi. Matumizi haramu ya dawa za kulevya yana madhara makubwa katika medani mbali mbali za maisha ya watu, jambo la msingi ni kujikita katika wongofu wa kiekolojia. Mchakato huu, uende sambamba pia na utunzaji bora wa mazingira kwa kuhakikisha kwamba, uvunaji mkubwa wa misitu na majanga ya moto yanadhibitiwa. Kwa njia ya utamadunisho, Injili ya Kristo inaendelea kung'ara katika maisha na tamaduni za watu. Imani katika Kristo Yesu ni kielelezo cha ukweli wa Kiinjili, unaomwezesha mwamini kutambua jambo jema la kufuata kwa ajili ya maisha yake ya kijamii.

Kanisa Ukanda wa Amazonia linataka kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha na matumaini; kwa kujielekeza zaidi katika mchakato mzima wa uinjilishaji unaoifunda mihimili mikuu ya uinjilishaji na utamadunisho ili kweli Injili iweze kugusa, kuganga na kutakasa maisha ya watu mahalia, ili nao pia waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya: uhai, matumaini na huruma ya Mungu kwa waja wake! Ni changamoto kwa watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia kutolea ushuhuda wa imani yao katika misingi ya kikristo inayopata chimbuko lake katika mafundisho ya Kanisa. Waamini wanapaswa kulinda uhusiano uliopo kati ya Injili na utambulisho wa tamaduni zao, ili kutolea ushuhuda wa imani yao katika Yesu Kristo, kiini cha wokovu wa ulimwengu. Mababa wa Sinodi wanasema, kuna haja ya kuweka uwiano mzuri kati ya mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho Ukanda wa Amazonia. Mababa wa Sinodi wanasema, dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inafumbatwa katika ushitiki mkamilifu wa watu wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa.

Hapa mkazo unawekwa kwenye ukuhani wa waamini wote; unaowataka waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa pamoja na kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene. Kuamsha ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko Kumbe, Ukanda wa Amazonia unaweza kuwa ni mahali pa kumwilisha dhana ya Sinodi ya Kimisionari katika maisha na utume wa Kanisa zima. Kumbe, hapa kuna mwingiliano mkubwa wa tamaduni, mila na desturi za watu wa Mungu na kwa njia, kuna uwezekano mkubwa wa kujenga mshikamano kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Wito na maisha ya Kipadre ni kama bustani, ambayo inaweza kutunzwa vyema lakini wakati mwingine inaweza kusahaulika. Kuna uhusiano mkubwa katika maisha na utume wa Kipadre unaofumbatwa katika huduma ya Kiinjili kwa ajili ya Familia ya Mungu.

Pale ambapo Padre anakosa mambo msingi katika ukuaji na ustawi wa maisha yake ya kiroho, hapo cheche za kuanza kumezwa na malimwengu zinaanza kujitokeza. Huu ndio mwanzo wa kukauka na hatimaye kunyauka kiroho kwa kutamani malimwengu ambayo kimsingi anapaswa kuyapatia kisogo. Huu ni mwanzo wa kupatwa na msongo wa mawazo na upweke hasi na matokeo yake ni kuchanganyikiwa na kujutia maamuzi ya kujiunga na wito, maisha na utume wa kipadre. Pale ambapo Padre anashindwa kusali, kutafakari na kuadhimisha barabara Mafumbo ya Kanisa, huo ni mwanzo wa kunyauka kwa maisha na utume wa Kipadre. Ukanda wa Amazonia una uhaba mkubwa wa Mapadre na Watawa. Lakini ikumbukwe kwamba, Mapadre ni mali ya Kanisa zima, kumbe, hapa kuna uwezekano wa kujenga umoja na mshikamano katika huduma za kichungaji. Baadhi ya Mababa wa Sinodi wamekazia umuhimu wa Wahudumu wa imani, unaohitaji malezi, makuzi na majiundo ya awali, endelevu na makini, ili kukuza na kudumisha uwajibikaji bora zaidi kwa uwepo na ushiriki wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa.

Dhana ya “Viri Probati” bado inaendelea kuchambuliwa na Mababa wa Sinodi. Mababa wa Sinodi wameelezea umuhimu wa Kanisa kuendeleza Ibada mbali mbali kama chemchemi ya neema na baraka kwa watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Lakini, Ibada hizi zinapaswa kuratibiwa ili ziweze kuadhimishwa kadiri ya taratibu, sheria na kanuni za Kanisa Katoliki. Taalimungu ya Kazi ya Uumbaji imesisitiziwa sana na Mababa wa Sinodi. Hapa kuna umuhimu wa kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi kati ya taalimungu na sayansi mbali mbali, Mwenyezi Mungu ambaye ni asili na hatima ya yote akipewa kipaumbele cha kwanza. Utu, heshima na haki msingi za binadamu Ukanda wa Amazonia zinapaswa kuendelezwa. Vijana wazalendo kutoka Ukanda wa Amazonia wapewe majiundo makini na endelevu. Mababa wa Sinodi wameendelea kupembua kuhusu umuhimu wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa Ukanda wa Amazonia.

Wanawake wajengewe uwezo ili kushiriki katika ngazi mbali mbali za uongozi. Wanawake kimsingi ni mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kanisa linawahitaji wainjilishaji makini watakaokuwa vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini na mapendo kwa watu wa Mungu. Mababa wa Sinodi wanasema, wanawake ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, kumbe, watiwe shime kukuza na kushirikisha karama hizi katika maisha na utume wa Kanisa. Mababa wa Sinodi wanasema, majadiliano ya kidini na kiekumene kati ya waamini wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo ni nyenzo msingi ya kupambana na tabia ya ubinafsi, misimamo mikali ya kidini na kiimani, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo, mshikamano na maridhiano kati ya watu, kila mtu akipewa nafasi ya kushuhudia imani yake! Kwa upande wa Ukanda wa Amazonia, utu, heshima na haki msingi ya wazawa zinapaswa pia kuangaliwa kwa jicho la pekee kabisa.

Lengo ni kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu; kwa kushirikishana huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Waamini wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo kwa pamoja na wanaweza kusimama kidete kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kimsingi, Ukanda wa Amazonia ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia nzima ya binadamu. Hii inatokana na ukweli kwamba, uchungu na fadhaa ya watu wa Ukanda wa Amazonia ni furaha na matumaini; uchungu na fadhaa ya Kanisa zima kama wanavyosema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Maisha ya wananchi wa Ukanda wa Amazonia ni matakatifu yanapaswa kuheshimiwa, kulindwa na kuendelezwa.

Sinodi: Dawa za Kulevya
10 October 2019, 15:47