Tafuta

Familia ya Mungu Ukanda wa Amazonia una kiu ya kutaka kushiriki katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa! Familia ya Mungu Ukanda wa Amazonia una kiu ya kutaka kushiriki katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa!  Tahariri

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Mafumbo ya Kanisa!

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia isaidie kutoa majibu yatakatokata kiu ya maisha ya kiroho kwa Watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Kwa sasa kuna wazo la “Dhana ya “Viri Probati”, yaani, Kanisa litoe kibali cha kufanya majaribio kwa wazee wanaume wenye ndoa na familia zao, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre ili wasaidie mchakato wa maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019 yanaongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake kuhusu Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia anasema, tangu Sinodi hii ilipozinduliwa rasmi, kumekuwepo na kilio kutoka kwa Mababa wa Sinodi, ili kuhakikisha kwamba, wazalendo kutoka Ukanda wa Amazonia, wanaheshimiwa, wanathaminiwa na kusikilizwa. Kuna umuhimu wa kusikiliza pia kilio cha Dunia Mama na maskini kutoka Ukanda wa Amazonia, tayari kuibua mbinu mkakati utakaosaidia mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Waamini wa Ukanda wa Amazonia, wanacho kilio kingine cha ukosefu wa huduma msingi za maisha ya kiroho kutokana na uhaba wa mihimili ya uinjilishaji yaani: wakleri, watawa na makatekista.

Kuna idadi ndogo sana ya Mapadre wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu walio enea sehemu mbali mbali za Ukanda wa Amazonia, huku kukiwa na vikwazo vya kuhama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kutokana na ukosefu wa miundo mbinu. Hii imekuwa ni changamoto kubwa kwa Mama Kanisa Ukanda wa Amazonia. Matokeo yake ni kwamba, kuna Jumuiya nyingi za waamini ambazo hazipati huduma ya Ibada ya Misa Takatifu pamoja na Neno la Mungu. Wanakosa Mapadre wakuwagawia Mafumbo ya Kanisa, kiasi kwamba, wengi wao wanaitupa mkono dunia wakiwa majumbani mwao bila msaada wa huduma za kiroho. Dr. Andrea Tornielli anasema, mchango wa mawazo, tafakari na mang’amuzi kutoka kwa Mababa wa Sinodi, yanapaswa kimsingi kutoa jibu makini litakalozima kiu ya maisha ya kiroho kwa watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia.

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia isaidie kutoa majibu yatakatokata kiu ya maisha ya kiroho kwa Watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Kwa sasa kuna wazo la “Dhana ya “Viri Probati”, yaani, Kanisa litoe kibali cha kufanya majaribio kwa wazee wanaume wenye ndoa na familia zao, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre ili wasaidie mchakato wa maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Ikumbukwe kwamba, hapa si kwamba, Kanisa linafyekelea mbali nadhiri ya useja au kutoa mwanya kwa wale Mapadre wanaotaka kuoa, kuanza “kuchakarika mapema iwezekanvyo”! La hasha! Lakini hii si njia peke yake! Kwa bahati mbaya iliyoje anasema Dr. Andrea Tornielli kwamba, ndio mkazo unaotolewa kwenye vyombo na mitandao ya kijamii. Wamesahau kwamba, ndani ya Kanisa Katoliki pia kuna Mashemasi wa kudumu, dhana ambayo ingepaswa kuimarishwa zaidi, kwa kuwapatia malezi na majiundo makini katika maisha na wito huu.

Majiundo makini ni wajibu kwa wakleri, watawa pamoja na waamini walei. Utume wa waamini walei ni jambo jingine linalopaswa kupewa kipaumbele cha pekee, kwani kimsingi, waamini walei wanapaswa kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu ili kuyatakatifuza malimwengu. Kuna watawa hata katika uchache wao, wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma za maisha ya kiroho na kiutu kwa familia ya Mungu Ukanda wa Amazonia. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu inalijenga na kuliimarisha Kanisa. Pale ambapo kuna uhaba wa Mapadre kwa maadhimisho haya? Hapa ni mahali muafaka pa kusoma alama za nyakati, kwa kumwachia Roho Mtakatifu, ili aweze kulielekeza Kanisa kutambua njia mpya zitakazowasaidia watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.

Njia mpya za Kanisa zinapaswa kwanza kabisa kuwashirikisha wazalendo kama wadau wakuu na mihimili ya uinjilishaji miongoni mwa ndugu zao katika Kristo Yesu. Wasimame imara kutangaza hna kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; wao wenyewe wawe ni Mashemasi wa kudumu, ili kuweza kuadhimisha Sakramenti kadiri ya Kanuni, Sheria na Taratibu za Kanisa. Huu ni wakati wa kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu, kwa kutambua kwamba, Sinodi ni safari ya watu wa Mungu katika umoja wao!

Taharirir: Sinodi

 

 

11 October 2019, 15:57