Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia 2019: Kardinali Claudio Hummes: Muhtasari wa hati ya kutendea kazi! Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia 2019: Kardinali Claudio Hummes: Muhtasari wa hati ya kutendea kazi! 

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Hati ya kutendea kazi!

Mababa wa Sinodi wanapaswa kujikita zaidi katika: Sura ya watu wa Amazonia ndani ya Kanisa kwa kukazia uinjilishaji, utamadunisho na mwingiliano wa tamaduni katika mazingira ya Kimisionari na Kikanisa. Utume wa Kanisa unaotekelezwa na: Wakleri pamoja na nafasi ya wanawake; utunzaji bora wa mazingira kwa kusikiliza sauti ya Dunia Mama na sauti ya maskini na ekolojia fungamani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Cláudio Hummes, Mwezeshaji mkuu wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019 yanaongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani” amefafanua kwa kina na mapana “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya Kutendea Kazi” itakayokuwa ni mwongozo wakati wa maadhimisho ya Sinodi, sehemu ya mchakato wa watoto wa Kanisa kutembea kwa pamoja, ili kuwaendea na kuwatangazia watu wa Mungu furaha ya Injili. Hawa ni wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili waweze kumtambua Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu, chemchemi ya huruma, upendo na faraja ya Mungu kwa waja wake. Huu ni wakati wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kwa ajili ya maskini, wagonjwa, wakimbizi na wahamiaji bila kuwasahau watu mahalia. Kanisa halina budi kutembea katika uaminifu wa Mapokeo na imani yake kwa Kristo Yesu kwa kusoma alama za nyakati.

Hakuna sababu msingi za kuogopa njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, historia nzima ya wokovu ni ufunuo wa upyaisho wa Mungu na kwamba, Kristo Yesu ndiye ule upyaisho wa milele! Sinodi hii inataka kutafuta na kuambata njia mpya kadiri ya Roho Mtakatifu atakavyoliongoza Kanisa. Sinodi inapania kujikita katika malezi na majiundo yatakayolisaidia Kanisa Ukanda wa Amazonia kuwa ni mihimili yake ya shughuli za kichungaji. Huu ni wakati wa Mama Kanisa kujikita katika uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa linatambua na kukiri mapungufu yake kwamba, kuna wakati baadhi ya watoto na wamisionari wake, walisaidiana na wakoloni kuwanyonya watu mahalia, Ukanda wa Amazonia. Ni wakati wa kutambua na kuthamini mchango na ushuhuda wa imani unaotolewa na waamini mbali mbali kwenye Ukanda wa Amazonia, kiasi hata cha kuyasadaka na kuyamimina maisha yao kama mbegu ya Ukristo.

Kanisa linataka kuwekeza katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hususan katika sekta ya elimu makini, afya pamoja na mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato, pamoja na kuhakikisha kwamba, watu wanaweza pia kuadhimisha Mafumbo ya imani, kikolezo cha ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ekaristi Takatifu na maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali ni muhimu sana katika maboresho ya maisha ya kiroho. Njia mpya za Kanisa ziwe ni chachu ya maendeleo fungamani kwa ajili ya wananchi mahalia wa Ukanda wa Amazonia. Wawe ni wadau na wahusika wakuu katika sera na mikakati ya maendeleo yao. Utume wa Kanisa Ukanda wa Amazonia unapania kupembua hali halisi, vipaumbele, changamoto na fursa zilizopo kwenye Ukanda wa Amazonia, ili kuweza kushirikiana na Serikali, taasisi na watu wote wenye mapenzi mema kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia.

Huu ni mchakato wa kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; kwa kujielekeza zaidi katika upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa, ari na mwamko wa kimisionari; utamadunisho na uinjilishaji, ili kuwatangazia watu wa Mungu Injili ya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake. Mwingiliano wa tamaduni ni muhimu sana kuendelezwa, kwa kujielekeza zaidi pia katika maboresho ya njia za mawasiliano ya kijamii. Kanisa na ekolojia fungamani ni sawa na chanda na pete, ni mambo yanayokamilishana, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ukanda wa Amazonia kwa miaka mingi umeandika kurasa chungu za mauaji ya viongozi na watetezi wa maskini; kumekuwepo na ufisadi na ubadhirifu mkubwa wa mali ya umma; ukwapuaji mkubwa wa ardhi na maliasili kwa matumizi ya watu na makampuni binafsi. Kumekuwepo na miradi mikubwa ya kiuchumi na kijamii ambayo imeendelea kuwanufaisha watu wachache pamoja na kusababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira ambao umekuwa ni chanzo kikuu cha magonjwa Ukanda wa Amazonia.

Eneo hili ni linafahamika sana kwa uzalishaji, biashara na matumizi ya dawa za kulevya; utumwa mamboleo pamoja na biashara haramu ya binadamu. Wananchi wa Ukanda wa Amazonia wametumbukizwa katika umaskini mkubwa. Kumbe, sera na mikakati ya ekolojia fungamani inafumbatwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Ekolojia ya mazingira, kijamii na kitamaduni ni kati ya mada zinazochambuliwa na Mababa wa Sinodi, ili kweli wananchi wa Ukanda wa Amazonia waweze kuwa na utimilifu wa maisha kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto fungamani ambayo haina budi kuvaliwa njuga na Mama Kanisa kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote”.

Wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na maskini, wanapaswa kujengewa uwezo wa kupambana na hali pamoja na mazingira yao kwa njia ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu pamoja na Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa yanapaswa kuangaliwa kwa kuzingatia njia mpya za Kanisa. Ili kukabiliana na upungufu wa Mapadre, Kanisa linataka kuangalia uwezekano wa kuwapatia Daraja Takatifu ya Upadre wanaume waliooa pamoja na kuboresha huduma ya wanawake wanaojiweka wakfu kwa ajili ya huduma ya watu wa Mungu, Ukanda wa Amazonia. Kanisa linatambua kwamba, maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu na hii ni changamoto kubwa kwa watu wa Mungu, Ukanda wa Amazonia. Uhaba huu unatokana na uchafuzi mkubwa wa vyanzo vya maji katika Ukanda wa Amazonia.

Kardinali Cláudio Hummes, Mwezeshaji mkuu wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia anashauri Mababa wa Sinodi kujikita zaidi katika mchakato wa Mama Kanisa Ukanda wa Amazonia kuweza kuangalia njia mpya: Sura ya watu wa Amazonia ndani ya Kanisa kwa kukazia uinjilishaji, utamadunisho na mwingiliano wa tamaduni katika mazingira ya Kimisionari na Kikanisa. Utume wa Kanisa unaotekelezwa na: Wakleri pamoja na nafasi ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa. Kuna haja kwa Kanisa kujikita katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira kwa kusikiliza sauti ya Dunia Mama na sauti ya maskini. Huu ni wakati wa kuibua sera na mbinu mkakati wa ekolojia fungamani mintarafu mazingira, uchumi, masuala ya kijamii na kitamaduni. Kanisa Ukanda wa Amazonia halina budi kusoma alama za nyakati tayari kuinjilisha mazingira ya mijini bila kusahau changamoto ya maji safi na salama kama sehemu ya haki msingi za binadamu.

Hati ya Kutendea kazi

 

07 October 2019, 15:43