Jeshi la Polisi nchini Italia limeanza kufanya uchunguzi ili kubaini watu walioiba na hatimaye, kuitupa mtoni Sanamu ya "Pachamama" kutoka Ukanda wa Amazonia Jeshi la Polisi nchini Italia limeanza kufanya uchunguzi ili kubaini watu walioiba na hatimaye, kuitupa mtoni Sanamu ya "Pachamama" kutoka Ukanda wa Amazonia  Tahariri

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Watu wanajimwambafai!

Watu wasiojulikana, wameiba na hatimaye, kutupa mtoni Sanamu ya “Pachamama” yaani “Dunia Mama” inayomwonesha mwanamke mwenye mimba, alama ya uhai. Sanamu ilikuwa imehifadhiwa kwenye Kanisa la “Santa Maria in Trasportina na ilitumika kwenye maonesho ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, tarehe 4 Oktoba 2019. Watu wanataka kujimwambafai!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, Jumatatu tarehe 21 Oktoba 2019 aliwaambia waandishi wa habari mjini Vatican kwamba, katika mazingira ya kusikitisha, watu wasiojulikana, wameiba na hatimaye, kutupa mtoni Sanamu ya “Pachamama” yaani “Dunia Mama” inayomwonesha mwanamke mwenye mimba, alama ya uhai. Sanamu hii ilikuwa imehifadhiwa kwenye Kanisa la “Santa Maria in Trasportina, liliko mjini Roma. Itakumbukwa kwamba, Sanamu hii ilitumika kwenye maonesho ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, tarehe 4 Oktoba 2019 kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko na tena wakati wa Ibada ya Njia ya Msalaba iliyoadhimishwa Jumamosi, tarehe 19 Oktoba 2019. Dr. Paolo Ruffini amefafanua kwa kusema kwamba, Sanamu ile ni alama ya uhai, zawadi ya maisha na kilio cha “Dunia Mama”.

Kitendo cha kuiba na hatimaye kuitupa kwenye Mto Tevere, mita chache tu kutoka kwenye Kanisa hilo ni kufuru na ni jambo linalokwenda kinyume kabisa cha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene. Tukio hili limewahuzunisha waamini na watu wenye mapenzi mema wanaofuatilia maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019 yanayoongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Lengo la Sinodi hii ni kubainisha njia mpya za uinjilishaji Ukanda wa Amazonia, kwa kusikiliza na kujibu kwa ufasaha kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini; kwa kupembua matatizo, changamoto na fursa zilizopo ili kutoa mapendekezo yatakayofanyiwa kazi na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake kuhusu tukio hili la kusikitisha anakaza kusema, ni uhalifu wa hali ya juu kabisa unaoonesha ile dhana ya baadhi ya watu kutaka “kujimwambafai” katika jamii kama walivyoshuhudia katika video ya tukio hilo ambayo imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Ni watu wanaojidai kwamba, ni “wana harakati na watetezi wa Mapokeo ya Kanisa”. Lakini cha kushangaza ni kitendo cha kuiba na kuitupa Sanamu hii mtoni; Sanamu inayoonesha zawadi ya uhai na utakatifu wa maisha. Hii ni alama muhimu sana kwa watu wa Ukanda wa Amazonia, wanaotumia alama hii kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya kazi ya Uumbaji.

Hii ni changamoto kwa wale waotaka “kujimwambafai” kuwa ni “wanaharakati wa kutunza na kuendeleza Mapokeo ya Kanisa” kujisomea tena changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Kardinali John Henry Newman katika insha yake ijulikanayo kama “Essay on the Development of Christian Doctrine” iliyochapishwa kunako mwaka 1878. Katika insha hii Mtakatifu Newman anafafanua kuhusu mchakato wa Kanisa linalowajibika kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ya Kristo Yesu katika maisha na vipaumbele vya watu, kwa kutumia: alama, mila, mavazi, desturi na tamaduni zao njema, bila kusahau siku kuu na maadhimisho kadiri ya kalenda ya maisha yao. Kwa maneno mengine, huu ni mchakato wa Kanisa kusoma alama za nyakati. Watu hawa wanaojimwambafai kwa kujiita kuwa ni wanaharakati wamesahau kwamba, Kanisa katika maisha, utume na historia yake, limeendelea kuziinjilisha tamaduni, ili kuitamadunisha Injili ya Kristo. Kwa mfano wimbo wa “Kyrie Eleison” yaani “Bwana Utuhurumie” una asili yake katika tamaduni za kipagani!

Wanajimwambafai
23 October 2019, 10:29