Tafuta

Siku kuu ya Deepavali kwa Mwaka 2019 inaongozwa na Kauli mbiu : Waamini: wajenzi wa udugu na wanaoishi kwa amani na utulivu. Siku kuu ya Deepavali kwa Mwaka 2019 inaongozwa na Kauli mbiu : Waamini: wajenzi wa udugu na wanaoishi kwa amani na utulivu. 

Siku kuu ya Deepaval 2019: Wajenzi wa udugu, amani na utulivu!

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linawatakia heri na baraka waamini wa dini ya Kihindu wanapoadhimisha Siku kuu ya “Deepavali”. Ni matumaini ya Baraza kwamba, Siku kuu hii itawasaidia waamini kuang’aza nyoyo, nyumba, familia na jamii ili zipate: furaha, amani, ustawi na maendeleo. Siku kuu hii iejenge na kuimarisha moyo wa udugu wa kibinadamu kati yao. Deepavali! Diwali!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini katika maadhimisho ya Siku kuu ya “Deepavali” au “Diwali” yaani “Sherehe mwanga” kwa waamini wa dini ya Kihindu ambayo inaadhimishwa tarehe 27 Oktoba 2019 unaoongozwa na kauli mbiu “Waamini: wajenzi wa udugu na wanaoishi kwa amani na utulivu”. Hii ni siku kuu ambayo inawahamasisha waamini wa dini ya Kihindu kujikita katika ukweli dhidi ya uongo, ili mwanga wa maisha yao, uweze kulifukuzia mbali giza la kifo, ili zawadi ya maisha iweze kung’ara zaidi. Kwa kawaida Siku kuu hii inadumu kwa muda wa siku tatu, kielelezo pia cha mwanzo wa Mwaka Mpya kwa waamini wa dini ya Kihundu. Hiki ni kipindi cha upatanisho wa kifamilia pamoja na kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka alizowakirimia waja wake Ujumbe huu umetiwa mkwaju na Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot, MCCJ, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini pamoja na Monsinyo Indunil Kodithuwakku Janakaratne Kankanamalage, Katibu wa Baraz la Kipapa la Majadiliano ya Kidini.

Viongozi wakuu wa Baraza la Kipapa wanawatakia heri na baraka waamini wa dini ya Kihindu wanapoadhimisha Siku kuu ya “Deepaval” au “Diwali” yaani “Sherehe mwanga”. Ni matumaini ya Baraza kwamba, Siku kuu hii ya mwanga itawasaidia waamini kuang’aza nyoyo zao, nyumba na familia zao, ndugu na jamaa zao, ili waweze kupata furaha, amani, ustawi na maendeleo. Wakati huo huo, Siku kuu hii isaidie kujenga na kuimarisha moyo wa udugu wa kibinadamu kati yao. Licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika sekta mbali mbali za maisha ya mwanadamu; kuna haja pia ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kitamaduni; kwa kukoleza ushirikiano na mshikamano wa kidugu. Lengo ni kuondokana na  utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; chuki na uhasama wa kidini na kiimani. Ni wakati wa kugundua jirani yako kuwa ni ndugu yako, licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza kati yenu.

Kushindwa kugundua udugu wa kibinadamu ni mwanzo wa harakati za kusambaratisha mafungamano ya kijamii. Ni katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, linapenda kuwashirikisha waamini wa dini ya Kihindu umuhimu wa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu ili kuweza kuishi kwa amani na utulivu. Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, utu na heshima ya binadamu; amani na maridhiano kati ya watu! Hati hii ni matunda ya uvumilivu, busara na hekima inayopania kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, ili kudumisha amani duniani! Waamini wa dini mbali mbali wanahamasishwa kujikita zaidi katika kanuni maadili na utu wema mintarafu mafundisho ya dini zao.

Kwa njia hii, waamini wataweza kuwa ni vyombo na wajenzi wa misingi ya haki na amani; umoja na udugu, chemchemi na dhamana ya dini mbali mbali duniani. Waamini wanapaswa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu kati yao; kwa njia ya majadiliano na mahusiano ya kawaida kati ya waamini wa dini mbali mbali. Waamini wasikubali hata mara moja kuvurugwa kwa kupandikiziwa mbegu za chuki na uhasama.  Waamini watambue kwamba, ndani mwao, kuna mbegu ya wema, uzuri na utakatifu ambayo imefichika na kwamba, wanapaswa kuivumbua na kuimwilisha kama mbegu ya umoja na mshikamano; chachu ya ujenzi wa umoja, mshikamano na amani. Inawezekana kabisa kujenga udugu wa kibinadamu na watu wakaishi kwa amani na utulivu, kwa ajili ya mafao ya wengi. Waamini wa dini mbali mbali wawe ni wajenzi na madaraja ya udugu wa kibinadamu, ili kuishi kuweza kuishi kwa amani na utulivu.

Hivi karibuni, Jumuiya ya Kimataifa imeadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 150 tangu alipozaliwa Mahtma Gandhi. Ni kiongozi aliyeshuhudia kwa ujasiri ukweli, upendo na amani katika maisha yake. Ni kati ya wadau wakuu waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu, amani na utulivu. Mahtma Gandhi awe ni mfano bora wa waamini kuishi kwa amani na utulivu. Waamini wa dini mbali mbali kwa kuzingatia mafundisho ya dini zao, wawe na ujasiri wa kuweza kushirikishana mang’amuzi haya kwa ajili ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu, amani na utulivu. Hii ni changamoto kwa waamini wa dini, imani na madhehebu mbali mbali pamoja na watu wote wenye mapenzi  kujizatiti kikamilifu, ili hatimaye, kuwajibika katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ili kuishi kwa amani na utulivu.

Siku Kuu ya Diwali

 

22 October 2019, 15:39