Tafuta

Mauaji, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali duniani zimeongezeka maradufu katika kipindi cha mwaka 2017-2019. Mauaji, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali duniani zimeongezeka maradufu katika kipindi cha mwaka 2017-2019. 

Mauaji ya Wakristo Duniani yameongezeka 2017-2019

Tangu mwaka 2017 - 2019 kumekuwepo na ongezeko kubwa la uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kidini; hali inayojikita katika: vita, chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani; pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyotishia misingi ya haki, amani na mafungamano ya kijamii. Takwimu zinaonesha kuwa wahanga wakuu wa madhulumu ya kidini sehemu mbali mbali za dunia ni Wakristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Taarifa ya Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji zilizowasilishwa Alhamisi, tarehe 24 Oktoba 2019 inaonesha kwamba, tangu mwaka 2017 hadi mwaka 2019 kumekuwepo na ongezeko kubwa la uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; hali inayojikita katika: vita, chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani; pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyotishia misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii. Takwimu zinaonesha kwamba, wahanga wakuu wa madhulumu ya kidini sehemu mbali mbali za dunia ni Wakristo. Kuna Mapadre 18 na Mtawa mmoja waliokuwawa duniani katika kipindi cha Mwaka 2019, kati yao kuna Mapadre 15 waliouwawa kikatili Barani Afrika, Burkina Faso na Kenya zinaongoza. Takwimu hizi ni changamoto kwa Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha umoja na mshikamano unaofumbatwa katika uekumene wa damu.

Taarifa hii ni uchunguzi uliofanywa kwenye Mataifa 20 na kati ya mataifa haya: Misri, Eritrea, India, Iran, Iraq na Siria yanaongoza kwa: dhuluma, nyanyaso na mauaji ya Wakristo duniani. Serikali ya Eritrea hivi karibuni imetaifisha shule na hospitali zilizokuwa zinamilikiwa na kuendeshwa na Makanisa mbali mbali ya Kikristo nchini humo. Wakristo huko Mashariki ya Kati ni watu wanaodhulumiwa kana kwamba, wao ni wananchi wa “Kundi B” kwa sababu ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Taarifa inaonesha kwamba, kumekuwepo na maboresho makubwa ya uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu katika nchi kama Cameroon, Burkina Faso na Sri Lanka. Uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee kwani ni sehemu muhimu sana ya haki msingi za binadamu. Maboresho ya mahusiano na mafungamano ya kidiplomasia ni mbinu mkakati unaoweza pia kusaidia kudumisha uhuru wa kidini.

Udhibiti wa biashara haramu ya silaha, sera na mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi kimataifa ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa. Sri Lanka inaongoza kwa mauaji ya Wakristo duniani, kwa kuwa na idadi ya Wakristo 253 waliouwawa wakati wa Sherehe ya Pasaka kwa mwaka 2019. Mauaji kwa kisingizio cha udini ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa pamoja na kuhakikisha kwamba, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na vyombo vya mawasiliano ya jamii, vinawajibika barabara kufichua maovu haya yanayoendelea kujificha katika jamii. Uhuru wa kidini ambao wakati mwingine unajulikana kama uhuru wa kuabudu unafumbatwa katika mambo makuu matatu yanayopaswa kuzingatiwa na wote: kwanza kabisa kuna umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; Pili, kulinda na kudumisha amani na utulivu kama chachu muhimu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Tatu, majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi ni mbinu mkakati unaoweza kuleta suluhu ya changamoto mbali mbali zinazoiandama familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati, kiasi cha amani na utulivu kushindwa kutawala katika akili na nyoyo za watu ili kujenga jamii inayosimikwa katika utu na ustaarabu.

Kanisa Hitaji

 

25 October 2019, 16:31