Tafuta

Vatican News
Mchango wa Vatican kwenye Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa: Ushirikiano wa Kimataifa, Umaskini, Maboresho ya Elimu, Athari za Mabadiliko ya Tabianchi, Haki na Amani. Mchango wa Vatican kwenye Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa: Ushirikiano wa Kimataifa, Umaskini, Maboresho ya Elimu, Athari za Mabadiliko ya Tabianchi, Haki na Amani.  (AFP or licensors)

Mchango wa Vatican: Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, 2019

Kardinali Pietro Parolin amekazia: Umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana katika kupambana na umaskini duniani; Umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika ujenzi wa misingi ya amani na usalama; maboresho ya elimu; mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na mbinu mkakati wa umoja na mshikamano katika sera za maendeleo fungamani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliofunguliwa hapo tarehe 22 Septemba 2019 na kuhitimishwa rasmi tarehe 30 Septemba 2019 imekuwa ni fursa kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kupembua kwa kina na mapana kuhusu: mustakabali wa ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kupambana na hatimaye, kutokomeza umaskini; umuhimu wa kujizatiti katika kuboresha kiwango cha elimu, mpango mkakati wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na hatimaye kufikia uwajibikaji wa pamoja ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hotuba yake, amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana kwa hali na mali katika kupambana na umaskini duniani, unaoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu; Umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika ujenzi wa misingi ya amani na usalama; maboresho ya elimu inayotolewa; mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na mbinu mkakati wa umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa, ili kuendeleza mchakato wa uchumi fungamani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kati ya changamoto changamani zinazoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia ni: ukosefu wa haki, amani na utulivu unaosababishwa na vita, kinzani na migogoro mbali mbali hasa huko Mashariki ya Kati, Venezuela na Nicaragua. Kwa upande wa Afrika kuna Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Sudan ya Kusini pamoja na mgogoro kati ya Ethiopia na Eritrea. Umoja wa Mataifa unapojiandaa kwa ajili ya kumbu kumbu ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwake, hapo mwakani, yaani 2020, iwe ni fursa ya kujizatiti katika sheria, kanuni na taratibu za Umoja wa Mataifa. Vita, kinzani, migogoro pamoja na vitendo vya kigaidi ni kati ya mambo yanayochangia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, kwa sasa idadi yao ni takribani milioni 70. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwajengea na kuwashirikisha wanawake katika sera na mikakati ya kutafuta suluhu ya vita na migogoro; kujenga na kudumisha utamaduni wa haki na amani pamoja na umuhimu wa kuzingatia utawala wa sheria na kuondokana na utamaduni wa kifo!

Mkataba wa Umoja wa Mataifa unaotaka kudhibiti utengenezaji, usambazaji na matumizi ya silaha za nyuklia ni muhimu sana katika mchakato wa Umoja wa Mataifa wa kutaka kujenga, kudumisha na kuimarisha amani na utulivu; mambo msingi katika utekelezaji wa mikakati ya maendeleo endelevu. Bila kuzingatia mambo haya, ajenda ya Maendeleo kimataifa ifikapo mwaka 2030, iliyozinduliwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, itakuwa ni ndoto ya mchana. Umoja wa Mataifa hauna budi kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kushikamana kwa hali na mali katika kupambana na umaskini duniani, unaoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi ya milioni 731 wanaoishi katika kiwango cha juu kabisa cha umaskini duniani; hali inayoweza kurekebishwa kwa kujikita katika sera na mikakati ya maendeleo fungamani ya binadamu. Maboresho ya huduma ya afya, elimu, maji safi na salama, hifadhi ya jamii pamoja na mapambano dhidi ya baa la njaa ni kati ya mambo ambayo yanayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa.

Kiwango cha ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana ni cha hali ya juu. Kumbe, kuna haja ya kuwekeza katika utengenezaji wa fursa za ajira. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujizatiti katika kuboresha kiwango cha elimu kwa kutambua kwamba, kuna zaidi ya watoto milioni 61 ambao hawakupata fursa ya kuanza masomo ya shule ya msingi na kuna zaidi ya watoto milioni 202 sehemu mbali mbali za dunia ambao hawana nafasi ya kuendelea na masomo. Watoto milioni 130 wanasoma katika mazingira duni sana na kwamba, wasichana na wanawake, bado wanabaguliwa katika masuala ya elimu kutokana na kukomaa kwa mfumo dume. Elimu bora ni haki ya watoto wote duniani. Kanisa Katoliki litaendelea kuchangia maboresho katika sekta ya elimu  kwa kutoa: elimu, malezi na kanuni maadili na utu wema. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushikakama ili kusaidia mchakato wa maboresho ya elimu sehemu mbali mbali za dunia, sanjari na kudumisha misingi ya haki jamii, amani na utulivu wa ndani.

Jumuiya ya Kimataifa anasema Kardinali Pietro Parolin, haina budi kushikamana katika utekelezaji wa mpango mkakati wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo inaendelea kusababisha majanga kwa watu na mali zao. Ili kufanikisha mpango huu, kuna haja ya kujikita katika teknolojia rafiki pamoja na kuhamisha teknolojia, mambo yanayohitaji uaminifu, ujasiri na uwajibikaji wa pamoja. Kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019, kuna adhimishwa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, inaongozwa na kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani". Lengo ni kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji, zitakazokidhi mchakato wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ukanda wa Amazonia, Bonde la Congo na misitu iliyoko Kusini Mashariki mwa Bara la Asia imo hatarini kutoweka. Kumbe, ni dhamana na wajibu wa kila raia kuhakikisha kwamba, anashiriki katika kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira bora nyumba ya wote.

Jumuiya ya Kimataifa inahitaji uwajibikaji wa pamoja ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Hapa kuna haja ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu; uchumi shirikishi pamoja na huduma bora za kijamii. Kanisa litaendelea kuchangia katika mchakato wa huduma ya afya. Takwimu za Kanisa Katoliki zinaonesha kwamba, Kanisa linamiliki asilimia 26% ya miundo mbinu yote ya afya duniani, na hivyo linachangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Juhudi zote hizi hazina budi kwenda sanjari na uhuru wa kidini pamoja na uhuru wa kuabudu bila kusahau huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Umoja wa Mataifa hauna budi kuwa ni daraja linalowaunganisha watu wa Mataifa mbali mbali, changamoto ni kuendelea kujizatiti katika kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga familia kubwa ya binadamu. Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 183. Kanisa Katoliki anasema Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwamba, litaendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Karfdinali Parolin: UN
03 October 2019, 16:54