Baraza Kuu la Mamlaka ya Habari za Kifedha Mjini Vatican AIF limesema bado lina imani na Dr. Tommaso Di Ruzza katika utendaji wake wa kazi. Baraza Kuu la Mamlaka ya Habari za Kifedha Mjini Vatican AIF limesema bado lina imani na Dr. Tommaso Di Ruzza katika utendaji wake wa kazi. 

Baraza la Habari za Kifedha AIF: Bado lina imani na Dr. Di Ruzza!

Baraza Kuu la Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican, AIF, linasema kwamba, bado lina imani na Dr. Tommaso Di Ruzza, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican. Ametekeleza dhamana na wajibu wake kwa: nidhamu, weledi na uadilifu mkubwa katika kushughulikia shutuma za wizi na ubadhirifu wa mali ya Kanisa. Uchunguzi wa ndani kwa sasa unaendelea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Usimamizi wa fedha za Kanisa katika: ukweli, uwazi, uadilifu na weledi ni kati ya mambo yanayoendelea kupewa msukumo wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko ili kweli rasilimali fedha iweze kutumika kiaminifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Baraza Kuu la Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican, AIF, linasema kwamba, bado lina imani na Dr. Tommaso Di Ruzza, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican. Ametekeleza dhamana na wajibu wake kwa: nidhamu, weledi na uadilifu mkubwa katika kushughulikia shutuma za wizi na ubadhirifu wa mali ya Kanisa. Kwa sasa Dr. Tommaso Di Ruzza pamoja na wafanyakazi wengine wanne wanachunguzwa na Mahakama ya Vatican kuhusiana na mashitaka makuu mawili yaliyotolewa mwezi Julai na Agosti 2019 kutoka katika Benki Kuu ya Vatican, IOR na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa Hesabu za Vatican kwa mujibu wa utekelezaji wa majukumu yao.

Uchunguzi huu umepelekea kukamatwa kwa nyaraka muhimu zinazohusishwa na majukumu yaliyotekelezwa na Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican, AIF, kutokana na wasi wasi wa uwepo wa mamlaka kutoka nje katika vitega uchumi vinavyohusika na fedha ya Kanisa. Dr. Renè Bruehart, Rais wa Baraza la Mamlaka ya Habari za Kifedha Vatican, AIF anasema, baada ya kushauriana na wajumbe wa Mamlaka, wameamua kuanzisha uchunguzi wa ndani, ili kufanya upembuzi wa kina na mapana kuhusu shughuli zilizotekelezwa na Mamlaka ya Habari za Kifedha Vatican, AIF. Kimsingi Dr. Tommaso Di Ruzza na wafanyakazi wenzake, wametenda kwa niaba ya Taasisi ya AIF kadiri ya Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. Pili, watuhumiwa wamezingatia taratibu zote. Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican, AIF, itaendelea na shughuli zake kitaifa na kimataifa na kwamba, Baraza Kuu la Mamlaka ya Habari za Kifedha mjini Vatican, AIF, likikamilisha uchunguzi wake wa ndani, litakuwa na uwezo wa kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu shutuma za wizi na ubadhirifu wa fedha ya Kanisa. Kuvuja kwa habari za watuhumiwa na hatimaye, picha zao kuchapishwa kwenye vyombo vya habari ni kosa la kimaadili.

Mamlaka ya Fedha, AIF
24 October 2019, 14:30