Tafuta

Kongamano la Kimisionari Kimataifa Nchini Nigeria: Ushuhuda wa Kristo Yesu aliueyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu pamoja na Kanisa lake ni mambo msingi! Kongamano la Kimisionari Kimataifa Nchini Nigeria: Ushuhuda wa Kristo Yesu aliueyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu pamoja na Kanisa lake ni mambo msingi! 

Kongamano la Kimisionari Kitaifa Nigeria: Ushuhuda wa imani!

Kongamano la Kimisionari Kitaifa huko mjini Benin, nchini Nigeria, kuanzia tarehe 22-26 Oktoba 2019. Kauli mbiu: “Kanisa la Kristo katika utume nchini Nigeria”. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia pamoja na changamoto zake, watu wa Mungu wana kiu na mwanga wa Injili ya matumaini. Kanisa kwa asili linaitwa na kutumwa kutangaza Injili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwezi Oktoba 2019, umetengwa maalum na Mama Kanisa kwa ajili ya kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari duniani, kwa namna ya pekee mwaka huu 2019, Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume "Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa: Kanisa la Kristo katika utume”. Kanisa linataka kuendeleza utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake. Waamini wanakumbushwa kwamba, uinjilishaji mpya unafumbatwa katika ushuhuda, kielelezo cha imani tendaji. Maadhimisho haya ambayo kwa sasa yanafikia kilele chake umekuwa ni muda wa: sala, katekesi, tafakari na matendo ya huruma!

Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, Katibu Mwambata, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, amekuwa nchini Nigeria kuhudhuria Kongamano la Kimisionari Kitaifa huko mjini Benin, nchini Nigeria, kuanzia tarehe 22-26 Oktoba 2019. Kauli mbiu: “Kanisa la Kristo katika utume nchini Nigeria”. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia pamoja na changamoto zake, watu wa Mungu wana kiu na mwanga wa Injili ya matumaini. Kanisa kwa asili linaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Maadhimisho ya Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 yamekuwa yakiratibiwa na Mashirika  ya Kipapa ya Kimisionari ambayo ni rasilimali ya umisionari ndani ya Kanisa kwani yanatoa huduma kwa Kanisa la kiulimwengu, kama mtandao wa dunia nzima wa kumuunga mkono Baba Mtakatifu katika majukumu yake ya kimisionari kwa kujikita katika: sala,  kwa kukuza na kuhimiza roho ya kimisionari, na ukarimu kutoka kwa wakristo duniani kote.

Michango mbali mbali humsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro katika juhudi zake za uinjilishaji kwa baadhi  ya Makanisa yenye uhitaji maalum. Mashirika haya ambayo kimsingi yako chini ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, ambalo linajihusisha pamoja na mambo mengine mchakato wa uinjilishaji katika nchi za kimisionari. Huduma ya kuwaandaa mapadri wazalendo inatekelezwa na Shirika la Kipapa la Mtakatifu Petro Mtume. Katika mchakato wa kuhamasisha mtazamo wa kimisionari kwa watoto, lipo Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu na hatimaye, shughuli za kuhamasisha na kutia moyo ukuzaji wa Imani ya Kikristo lipo Shirika la Kipapa la Umoja wa Wamisionari. Mashirika yote haya yamekuwa yakichangia kwa hali na mali katika maisha na utume wa Kanisa tangu kuanzishwa kwake, wakati wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na viongozi wakuu wa Kanisa waliofuatia baadaye hadi kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, amefafanua maana ya utume wa kimisionari ambao kimsingi ndio asili ya Kanisa. Lengo ni kuwafundisha na kuwabatiza watu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili hatimaye, waweze kukutana katika maisha yao na Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu daima unakwenda sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Kanisa linamtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ndicho kiini cha Injili. Uinjilishaji mpya unafumbatwa katika ushuhuda wa maisha, ili kupyaisha, kuimarisha na kumwilisha imani katika matendo, kielelezo cha ukomavu wa imani katika Kristo Mfufuka. Uinjilishaji na utamadunisho ni sehemu ya vinasaba vya Mama Kanisa kwani kimsingi, anawajibika kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili; kwa kusimama kidete katika wongofu wa kitamaduni unaothamini tamaduni, mila na desturi njema za watu wa Mungu.

Kwa njia hii, Kanisa litaweza kuunda utamaduni wa Kikristo unaofumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili. Huu ni mchakato ambao umesimikwa katika historia ya maisha na utume wa Kanisa. Familia zinapaswa kuinjilishwa, ili nazo ziweze kuinjilisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya Kikristo. Changamoto hii inakwenda sanjari na utume wa familia unaopania kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili hatimaye, familia zenyewe ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia inayokita mizizi yake katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Familia zinapaswa kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, madhabahu ya sala, upendo na msamaha wa kweli mambo yanayopata chimbuko lake kutoka katika Neno la Mungu. Kanisa nchini Nigeria, halina budi kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kuimarisha: imani, matumaini na mapendo. Kanisa nchini Nigeria, liendelee kuonesha ukarimu wa kimisionari kwa kuwatoa na kuwatuma mapadre na watawa kwenda kuinjilisha, lakini ukarimu huu hauna budi kuanzia kwanza nyumbani nchini Nigeria na Bara la Afrika katika ujumla wake.

Katika hotuba yake, Askofu mkuu Giampietro Dal Toso amefafanua kwa kina na mapana kuhusu: historia, asili, dhima na karama ya Mashirika mbali mbali ya Kipapa Kimisionari. Kuna uhusiano wa karibu kati utambulisho wa Kanisa la Kiulimwengu na utambulisho wa Kanisa mahalia; imani na utume wa Kanisa. Amewataka Maaskofu mahalia kujenga na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari. Katika Ibada ya Kufunga Kongamano la Kimisionari Kitaifa nchini Nigeria, Askofu mkuu Giampietro Dal Toso amesema, umefika wakati wa kujikita katika mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha matakatifu na adili, huku Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu akipewa kipaumbele cha kwanza. Kristo Yesu ni chemchemi na utimilifu wa maisha. Kanisa halina budi kutangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo. Kanisa lijitahidi kuifahamu historia yake ili liweze kuwaelekeza watu katika toba na wongofu wa ndani, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika safari ya maisha yao.

Kama Kanisa na kwa mwamini mmoja mmoja, anapaswa kufanya mang’amuzi katika maisha yake ili kuweza kugundua sauti ya Mungu inayozungumza kutoka katika undani wa maisha. Matukio mbali mbali yawe ni ya uchungu, furaha au matumaini, yawasaidie waamini kusoma alama za nyakati, tayari kukutana na Kristo Yesu hata katika matukio kama haya. Toba na wongofu wa ndani ni mchakato endelevu katika maisha ya Wakristo, kwani “Wamebatizwa na kutumwa: Kanisa la Kristo katika utume”. Wanatumwa kama wamisionari sehemu mbali mbali za dunia, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Wanatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Itakumbukwa kwamba, Mwezi Oktoba, ni mwezi wa Rozari Takatifu: muhtasari wa huruma ya Mungu katika hija ya maisha ya mwanadamu hapa ulimwenguni. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wamisionari sehemu mbali mbali za dunia, wanaokumbana na matatizo pamoja na changamoto katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Waamini wanahimizwa kuendelea kusali Rozari Takatifu. Ikumbukwe kwamba, Injili na Amani ni sawa na chanda na pete, vinatembea kwa pamoja!

Kongamano la Kimisionari Nigeria
30 October 2019, 14:59