Tafuta

Vatican News
Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot anasema, majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda! Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot anasema, majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda! 

Kardinali Guixot: Majadiliano ya kidini ni vinasaba vya Kanisa

Majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa Katoliki ili kujenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano kati ya watu wa mataifa na wala si kwa bahati mbaya kwamba, Kanisa katika mikakati na vipaumbele vyake katika mchakato wa uinjilishaji linaendelea kukazia majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani. AMANI!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Miguel Ángel Ayuso Guixot, M.C.C.I, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, Mfalme El Hassan Bin Tal wa Yordan ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya kifalme ya Majadiliano ya Kidini huko Amman pamoja na viongozi mbali mbali wa Kanisa na Dini ya Kiislam, Jumanne, tarehe 8 Oktoba 2019 huko Jimbo kuu la Firenze, wameshiriki katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokutana na na Sultani Al Malik Al Kamil yaani kati ya mwaka 1219 hadi mwaka 2019 na huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa: uwazi, ukarimu umoja na udugu wa kibinadamu kati ya Wakristo na Waislam, changamoto inayoendelea kuvaliwa njuga na waamini wa pande hizi mbili. Kardinali Miguel Ángel Ayuso Guixot anaendelea kufafanua kwamba, mkutano kati ya viongozi hawa wawili ulisaidia pia mchakato wa unabii uliotekelezwa na Meya wa Mji wa Firenze Giorgio la Pira (1904 – 1977) kutiwa kwa saini ya makubaliano ya amani kati ya viongozi wa dini ya Kiislam, Kiyahudi na Wakristo kuhusu ufunguzi wa taasisi ya majiundo makini ya majadiliano ya kidini na mwingiliano wa kitamaduni.

Majadiliano ya kidini yanakita mizizi yake katika utambulisho makini wa waamini pamoja na mambo msingi yanayofumbatwa katika imani yao. Ni katika muktadha huu, wanaweza kutambua na kukiri tofauti zao msingi na mambo yanayowaunganisha kama ndugu wamoja. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa mkwaju kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu kama familia kubwa ya binadamu. Kardinali Miguel Ángel Ayuso Guixot katika hotuba yake anasema, adui mkubwa wa mchakato wa majadiliano ya kidini ni woga na wasiwasi usiokuwa na msingi wala mashiko; mambo yanayochangia watu wa dini mbali mbali kushindwa kufahamiana na hatimaye kuishi kwa amani, umoja na udugu. Watu wanapaswa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na hivyo tofauti zao za kidini si sababu msingi ya malumbano na kinzani zinazoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhimiza umuhimu wa waamini wa dini mbali mbali kufahamiana, kuheshimiana na kushirikiana kwa dhati katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa Katoliki ili kujenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano kati ya watu wa mataifa na wala si kwa bahati mbaya kwamba, Kanisa katika mikakati na vipaumbele vyake katika mchakato wa uinjilishaji linaendelea kukazia majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani. Waamini wanaweza kujenga na kudumisha umoja, udugu na urafiki kwa kusaidiana katika hija ya maisha yao hapa duniani. Baba Mtakatifu wakati wa hija yake ya kitume nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati alikazia umuhimu wa watu kuishi katika umoja, upendo na mshikamano kwa sababu majadiliano ya kidini, udugu wa kibinadamu, haki na amani ni mambo msingi ya maisha ya watu wa Mungu.

Kwa njia ya majadiliano ya kidini, watu wanakutana, wanazungumza, wanafahamiana na hivyo kuanzisha mchakato wa kutembea bega kwa bega kama ndugu wamoja. Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuwa ni shuhuda na chombo cha amani, kwa kufyekelea mbali yale yote yanayosababisha: chuki, kinzani na mipasuko ya kidini na kiimani. Ni matamanio halali ya Baba Mtakatifu Francisko kuona Kanisa linajikita katika ufukara, kwa kujenga na kudumisha urafiki na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa linataka kuendesha majadiliano na watu wa dini mbali mbali katika mwanga wa Injili, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ushirikiano huu unatambua na kuthamini amana na utajiri wa maisha ya kiroho unaobubujika kutoka katika dini mbali mbali duniani! Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, takribani miaka 50 iliyopita walitoa tamko kuhusu majadiliano ya kidini kwa watu wa nyakati hizi linalojulikana kama “Nostra Aetate."

Hili ni tamko linalokazia pamoja na mambo mengine: Dhamana ya Kanisa katika kuhamasisha umoja na upendo kati ya watu wa mataifa; kwa ajili ya mafao ya wengi, ili kusimama kidete kutangaza na kushuhudia pamoja utu na heshima ya binadamu. Kanisa Katoliki linatambua mambo ya kweli na matakatifu katika dini mbali mbali, lina heshimu na kuthamini namna yao ya kutenda na kuishi; sheria na mafundisho yao. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanakaza kusema, Kanisa litaendelea kutangaza kwamba Yesu Kristo ni njia, ukweli na uzima na ambaye ndani mwake mwanadamu anapata utimilifu wa maisha ya utauwa na upatanisho kati yake na Mwenyezi Mungu. Mama Kanisa anawahamasisha watoto wake kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; ustawi na mafao ya wengi. Kanisa linatambua kwamba, bado kuna changamoto nyingi na vikwazo vya kufanyiwa kazi, lakini hadi hapa linapenda kumshukuru Mungu.

Mtakatifu Paulo VI, tarehe 28 Oktoba 1965 wakati akifunga maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican alikaza kusema, Mtaguso ni kielelezo cha Kanisa linalosali, Kanisa linalojadiliana, Kanisa linalokua na Kanisa linaloendelea kujijenga, ili kukoleza mchakato wa majadiliano ya upendo na walimwengu. Waamini wa dini mbali mbali wanahamasishwa kusimama kidete ili kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani zao; kulinda na kudumisha haki, amani, upendo na mshikamano; sanjari na kukuza uhuru wa kidini. Elimu ya dini na malezi, ni muhimu sana katika kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili. Wakati huo huo, waamini wa dini ya Kiislam wanaofanya kazi katika taasisi za Kanisa Katoliki wanasema, wanaendelea kufurahia huduma yao na kwamba, wanajisikia wako nyumbani na wala hawajawahi kutengwa wala kunyanyaswa kwa misingi ya kidini. Kila mtu anaheshimiwa kama binadamu na kwamba, tofauti zao za kiimani ni utajiri mkubwa unaoweza kutumika kwa ajili ya kudumisha amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Majadiliano ya Kidini
09 October 2019, 15:33