Tafuta

Vatican News
Kardinali Leonardo Sandri anawataka Wakristo kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa njia ya matendo zaidi. Kardinali Leonardo Sandri anawataka Wakristo kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa njia ya matendo zaidi. 

Kardinali Sandri: Wakristo imani inashuhudiwa kwa vitendo!

Hiki ni kielelezo cha uekumene wa damu unaoshuhudiwa na Wakristo wote bila ubaguzi. Kanisa kuu la Mtume Bartolomeo linahifadhi masalia ya waungama na wafiadini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waamini ambao wameamua kujisadaka kwa ajili ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kuna wafiadini kutoka Algeria, waliotangazwa kuwa wenyeheri tarehe 18 Desemba 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, Alhamisi, tarehe 24 Oktoba 2019 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Bartolomeo Mtume, linalohifadhi masalia ya wafiadini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana na madhulumu dhidi ya Wakristo. Lakini, ikumbukwe kwamba, kilio cha watu wanaodhulumiwa, kunyanyaswa na kuteswa, kinamfikia Mwenyezi Mungu na iko siku atajibu sala zao. Kardinali Sandri amelishukuru Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji kwa kazi kubwa linalofanya, kama kielelezo cha mshikamano wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Makanisa hitaji. Hiki ni kielelezo cha uekumene wa damu unaoshuhudiwa na Wakristo wote bila ubaguzi. Kanisa kuu la Mtume Bartolomeo linahifadhi masalia ya waungama na wafiadini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waamini ambao wameamua kujisadaka kwa ajili ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Kuna wafiadini kutoka Algeria, waliotangazwa kuwa wenyeheri tarehe 18 Desemba 2018. Hawa ni waamini ambao wamekita imani na matumaini yao kwa Kristo Yesu. Ni watu ambao wamekuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kama ilivyokuwa kwa Kardinali Posadas Ocampo aliyeuwawa kikatiliki nchini Mexico kutokana na chuki za kidini. Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuondokana na chuki na uhasama na badala yake kujenga utamaduni wa kusamehe na kusahau; kwa kujenga upendo wa dhati, usiokuwa na mipaka. Damu ya mashuhuda wa imani sehemu mbali mbali za dunia, ni mbegu ya Ukristo kama wanavyosema Mababa wa Kanisa. Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji limekuwa ni msaada mkubwa kwa ajili ya Makanisa mahalia huko Mashariki ya Kati kama sehemu ya ushuhuda wa mshikamano katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.  Kuna baadhi ya nchi ambazo zimeamua kutaifisha au kufunga shule na hospitali zinazomilikiwa na kuendeshwa na Makanisa huko Mashariki ya Kati.

Vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati inatishia misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Lakini, ikumbukwe kwamba, Wakristo wana haki ya kuendelea kuishi huko Mashariki ya Kati, eneo ambalo watu wake wanalikimbia, kiasi cha kutishia uwepo wa imani ya Kikristo katika eneo hili. Siku ya Sala ya Kiekumene kwa ajili ya kutafakari na kuombea amani huko Mashariki ya Kati, iliyoadhimishwa tarehe 7 Julai 2018, Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo walipenda kujielekeza zaidi huko Mashariki ya Kati kwa kuangalia madhara ya vita  Siria na Iraq, hali ambayo imesababisha vifo, uharibifu mkubwa wa miundo mbinu pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum hata katika nchi zao wenyewe. Wakati wa mkutano wao wa faragha, sala, tafakari na chakula cha pamoja, viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo walionesha moyo wa furaha na shukrani kwa Makanisa kuweza kukutana kwa ajili ya kutafakari na kusali, ili kuombea amani huko Mashariki ya Kati, wazo ambalo walilianzisha wao wenyewe na hatimaye, kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko.

Ilikuwa ni siku yenye mvuto na mashiko katika maisha na utume wa Kanisa huko Mashariki ya Kati na hatua kubwa katika majadiliano ya uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa familia ya Mungu kama sehemu ya mchakato wa maisha na utume wa Kanisa. Huu ni ushuhuda wa umoja na mshikamano wa Kanisa, changamoto ambayo imevaliwa njuga na Mababa wa Kanisa tangu baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ili wote wawe wamoja chini Kristo Mchungaji mkuu. Tazama inavyopendeza ndugu wakikaa kwa umoja na upendo! Mashariki ya Kati ni Ukanda ambao kwa sasa umegeukwa kuwa ni uwanja wa vita, mateso na mahangaiko matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Kanisa litaendelea kusali kwa ajili ya kuombea haki, amani na utulivu huko Mashariki ya Kati kama alivyofanya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wa Makanisa.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu ambao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, maisha ni matakatifu. Hati inazungumzia kuhusu mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kardinali Leonardo Sandri anaendelea kufafanua kwamba, Hati nii ni kielelezo cha matumaini mapya, kumbe, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wana wajibu wa kuisoma, kuitafakari na hatimaye, kujitahidi kumwilisha maudhui yake katika uhalisia wa maisha, ili kudumisha misingi ya haki na amani. Vita sehemu mbali mbali za dunia ni kielelezo cha uchu wa mali na madaraka. Katika muktadha kama huu kuna haja kwa Wakristo kusimama kidete ili kutangaza, kushuhudia na kutetea imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kuna wakati watahitajika kuonesha ushuhuda kiasi hata cha kuweza kuyamimina maisha yao kwa ajili ya imani yao. Kuwa Mkristo katika ulimwengu mamboleo kuna gharama kubwa ya maisha na hii ni chachu ya kuenea kwa Ukristo sehemu mbali mbali za dunia. Jambo la msingi ushuhuda wa imani, “marturia”.

Kardinali Sandri: Dhuluma

 

 

25 October 2019, 16:52