Tafuta

Vatican News
Makardinali wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Makardinali wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!  (Vatican Media)

Makardinali wawe ni vyombo na mashuhuda wa majadiliano

Utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana ni msingi wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni tunu ambayo inapaswa kuendelezwa na kudumishwa; kwa kuheshimiana na kuthamianiana kama ndugu wamoja licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza. Kama viongozi wa Kanisa wanao wajibu wa kuendeleza Ukatoliki wa Kanisa unaofumbatwa katika mchakato wa ubunifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali José Tolentino Calaça de Mendonça, Mhifadhi mkuu wa Nyaraka za Kanisa na Mkutubi mkuu wa Maktaba ya Kanisa Katoliki. Alizaliwa tarehe 15 Desemba 1965 nchini Ureno. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 28 Julai 1990. Papa Francisko tarehe 26 Juni 2018 akamteuwa kuwa Mhifadhi mkuu wa Nyaraka za Kanisa na Mkutubi mkuu wa Maktaba ya Kanisa Katoliki na kumpandisha hadhi ya kuwa Askofu mkuu na kuwekwa wakfu tarehe 28 Julai 2018. Amewahi kuwa Gombera wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wareno kilichoko mjini Roma. Kwa miaka mingi amekuwa ni Jaalim, Mlezi na Kiongozi kwenye Vyuo vikuu vya Kipapa huko Brazil na tangu mwaka 2011 amekuwa ni mjumbe wa Baraza la Kipapa la Utamaduni. Kardinali José Tolentino Calaça de Mendonça ni mtunzi mahiri wa mashairi na mwanataalimungu wa “kutupwa” anasema, ukardinali wake anataka kuutumia kwa ajili ya kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Hii ni sehemu ya amana, utajiri na urithi alioupokea kutoka kwa wazazi wake ambao kwa asili ni Wareno. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko kuna haja ya kujizatiti katika mchakato wa ujenzi wa madaraja na utamaduni wa watu kukutana. Kuna baadhi ya wanasiasa kutokana na ubinafsi, uchoyo na utandawazi usioguswa na mahangaiko ya wengine, wameanza kujenga kuta za utengano pamoja na kuchochea chuki dhidi ya wageni kama mpango mkakati wa kutaka kujijengea umaarufu usiokuwa na tija wala mvuto! Dhamana na wajibu wa Wakristo ni kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, changamoto endelevu inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana ni msingi wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni tunu ambayo inapaswa kuendelezwa na kudumishwa; kwa kuheshimiana na kuthamianiana kama ndugu wamoja licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza.

Kama viongozi wa Kanisa wanao wajibu wa kuendeleza Ukatoliki wa Kanisa unaofumbatwa katika mchakato wa ubunifu. Habari Njema ya Wokovu iwaunganishe watu wa Mungu, ili kusikiliza na hatimaye, kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha yao. Ni wakati muafaka wa kusikiliza Neno la Mungu ambalo wakati mwingine linajikita katika “kimya kikuu”, ili kutoa nafasi kwa mwamini kuzama katika undani wa maisha yake, ili kuangalia na kutekeleza mpango wa Mungu kadiri ya hali na mazingira yake. Kardinali José Tolentino Calaça de Mendonça anasema, atendeleza kipaji na karama yake ya ushairi, kwani hii ndiyo iliyomfikisha hapo alipo kama “Malenga”. Anapenda kuwasaidia waamini na watu wenye mapenzi mema kujenga utamaduni wa kusoma Neno la Mungu na kusikiliza kwa makini; ili kutoa nafasi kwa Neno la Mungu kupyaisha maisha na vipaumbele vya waja wake. Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake.

Huu ni muhtasari wa kiu na matamanio halali ya binadamu: kiroho na kimwili, kimsingi hizi ni “Heri za Kiu”, sheria inayogusa undani wa maisha ya binadamu, kiini cha maisha na utume wa Kristo Yesu hapa duniani; mchungaji mwema aliyethubutu kuwaacha kondoo wengine wote na kuanza kumtafuta kondoo aliyepotea. Kristo Yesu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; upendo uliomwilishwa katika Fumbo la Umwilisho na kupata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Jamii inawahitaji mashuhuda na vyombo vya amani inayomwilishwa kila siku katika uhalisia wa maisha ya watu! Hawa ni watu wenye uwezo wa kupenda na kupendwa; kutangaza na kushuhudia ukweli kwa kutambua kwamba, Kanisa ni kama Hospitali iliyoko kwenye uwanja wa mapambano, tayari kuganga na kuponya majeraha ya watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali katika maisha.

Kanisa linahamasishwa kuonesha ari na moyo wa kimisionari ili kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na huduma kwa maskini, ili hata wao waweze kushiriki katika karamu ya yule mwanakondoo. Kanisa halina budi kuendelea kujipyaisha daima katika sera, mikakati na mipango yake ya shughuli za kichungaji kwa kusoma alama za nyakati, ili kuzima kiu ya uwepo wa Mungu katika maisha ya watu! Wakristo wanapaswa kuwa ni Jumuiya  ambayo ni chemchemi ya furaha na matumaini kwa watu wa Mataifa. Iwe ni mahali panapowakutanisha watu ili kujibu kilio chao cha ndani: kiroho na kimwili; kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; huruma, upendo na mshikamano wa huduma makini! Mang’amuzi ya kiu ya imani, yawasaidie waamini kujikita katika tafiti moyo ili kutambua kiu na matamanio yao halali ya kumwona Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, waamini wanajipatanisha na kiu yao kwa kutambua kwamba, kiu yao ni kiini cha heri maishani! Huu ni muhtasari wa tafakari iliyotolewa na Padre Josè Tolentino de Mendonca kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican, Ijumaa, tarehe 23 Februari 2018 huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma.

Kardinali Jose: Umoja
08 October 2019, 15:05