Tafuta

Vatican News
Mama Kanisa anawachangamotisha watoto wake kuhakikisha kwamba, wanamwilisha chachu ya utakatifu wa maisha katika uhalisia wa maisha yao. Mama Kanisa anawachangamotisha watoto wake kuhakikisha kwamba, wanamwilisha chachu ya utakatifu wa maisha katika uhalisia wa maisha yao.  (AFP or licensors)

Utakatifu unaomwilishwa katika maisha ni wito kwa waamini wote!

Mababa wa Kanisa wanasema, utakatifu ni wito kwa watu wote wa Mungu. Ili kufikia azma hii, wanapaswa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu pamoja na kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao Matunda ya Roho Mtakatifu. Huu ni mchakato wa utakatifu unaosimikwa katika maisha ya kila mmoja, kwa kutumia karama na mapaji yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 13 Oktoba 2019, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewatangaza watakatifu wapya. Hawa ni: Kardinali John Henry Newman, muasisi wa Kituo cha Michezo cha Mtakatifu Filippo Neri kilichoko nchini Uingereza. Sr. Giuseppina Vannini, Muasisi wa Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Camillus; Maria Theresa Chiramel Mankidiyan, Muasisi wa Shirika la Watawa wa Familia Takatifu; Sr. Dulce Lopes Pontes wa Shirika la Watawa Wamisionari wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na Mama wa Mungu pamoja na Margarita Bays, Bikira na mtawa wa Utawa wa tatu wa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Hawa ni wale ambao wametembea katika imani na kwa sasa wanakuwa waombezi wa watu wa Mungu. Kati yao kuna watawa watatu wanaoonesha kwamba, maisha ya kitawa ni hija ya upendo kuekelea katika vipaumbele vya maisha ya watu, vinavyosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Mtakatifu Margarita Bays anaonesha umuhimu wa sala inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku; uvumilivu na sadaka ambayo imemwezesha Mwenyezi Mungu kumkirimia kuweza kuishi mng’ao wa Fumbo la Pasaka. Kardinali John Henry Newman ni shuhuda wa utakatifu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku, kwa kujikita katika amani na utulivu wa ndani; kwa kuwashirikisha wengine ile furaha inayofumbatwa katika utu wema, upendo, kiasi na fadhila pasi na kujitafutia makuu. Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu anasema, hawa ni waamini ambao wamepandikiza mbegu ya utakatifu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, utakatifu ni wito kwa watu wote wa Mungu, ili waweze kuwa wakamilifu kama Baba yao wa Mbinguni alivyo mkamilifu. Ili kufikia azma hii, wanapaswa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu pamoja na kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao Matunda ya Roho Mtakatifu sanjari na kuomba neema ya kusamehe na kusahau.

Huu ni mchakato wa utakatifu unaosimikwa katika maisha ya kila mmoja, kwa kutumia vipawa, majukumu na hivyo kusonga mbele bila kusitasita katika safari ya imani iliyo hai, iamshayo matumaini na kutenda kwa mapendo. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa ni mfano na kielelezo cha utakatifu wote. Kardinali Giovanni Angelo Becciu, anaendelea kufafanua kwamba, Kanisa limebahatika kuwa na umati mkubwa wa watakatifu wanawake. Hawa ni wale ambao anasema Mtakatifu Yohane Paulo II waliobahatika kutumia karama na mapaji yao, kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa; wakajikita kikamilifu katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Watakatifu wapya waliotangazwa na Papa Francisko ni waamini waliojipambanua kwa njia ya Injili ya huduma ya upendo kwa jirani zao, kiasi kwamba, wanaweza kuitwa kuwa ni “Wanawake wa Injili ya Upendo inayosimikwa katika haki, udumivu na ujasiri”. Injili ya upendo ni chapa inayotawala watakatifu wengi kama ilivyokuwa kwa Mama Theresa wa Calcutta. Ni wanawake wa shoka ambao wamejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia na jamii katika ujumla wake.

Wanawake kimsingi ni watu waliobahatika kuwa na: karama ya ukarimu, wana uwezo wa kulinda na kutunza; kusamehe, kusahau na kuwafariji: yatima, wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kardinali Giovanni Angelo Becciu anakaza kusema, kati ya watakatifu wapya yumo pia. Kardinali John Henry Newman, aliyekuwa mwamini wa Kanisa Anglikani, akaoongokea katika Kanisa Katoliki, kielelezo makini cha moyo wa utulivu katika tofauti. Ni kiongozi ambaye amechangia sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa Anglikani. Katika tafakari na mawazo yake ya kitaalimungu, alifafanua kwa kina na mapana Ukristo na chanzo cha uwepo wa Makanisa mbali mbali. Aliwataka wakristo kutafuta na hatimaye kuumbata ukweli wa maisha. Ni kiongozi aliyesimika maisha yake katika majadiliano ya kina, akajitaabisha kumtafuta Mungu katika uhalisia wa maisha yake, katika amani na utulivu wa ndani; kwa kuwaheshimu na kuwathamini watu wote.

Ni Jaalimu mahiri wa taalimungu, kiongozi aliyebobea katika historia ya Mababa wa Kanisa, ndiyo maana hata Kanisa Anglikani linamshukuru Mtakatifu Kardinali John Henry Newman kwa mchango na mawazo yake katika maisha na utume wa Kanisa Anglikani. Kwa hakika, amekuwa ni daraja la majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa Anglikani. Kardinali John Henry Newman ana mchango mkubwa katika mchakato wa utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Ni kiongozi mwenye mawazo mapana na imani thabiti; mnyenyekevu na mtiifu katika mchakato wa kuutafuta na kuumbata ukweli. Kardinali Giovanni Angelo Becciu, anaendelea kufafanua kwamba Sr. Giuseppina Vannini, Muasisi wa Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Camillus katika maisha na utume wake, alijisadaka kwa ajili ya wagonjwa na maskini wa mji wa Roma. Ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa wale wote wanaoteseka na kusetwa kwa magonjwa na upweke unaowafanya hata kuchungulia kifo! Baba Mtakatifu Francisko anataka kuona Kanisa ambalo ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu hasa kwa maskini. Watawa wa Mtakatifu Camillus wanaendelea kuchangia katika huduma kwa wagonjwa sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, huduma ya upendo inapaswa kuwa ndio utambulisho wao kwa wagonjwa.

Maria Theresa Chiramel Mankidiyan, Muasisi wa Shirika la Watawa wa Familia Takatifu, lililokita mizizi yake nchini India. Katika maisha na utume wake, amejipambanua kuwa ni mwanamke wa shoka katika majadiliano ya kidini; akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na maskini. Akashuhudia upendo wa Mungu kwa ujasiri na imani thabiti. Maisha yake, yalichachushwa kwa toba, wongofu wa ndani, kufunga na kusali, ili kudhibiti vilema na mapungufu yake ya kibinadamu. Leo hii, Shirika lake lina zaidi ya watawa 2000 na wanovisi 200, matendo makuu ya Mungu. Hili ni Shirika ambalo limewekeza sana katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Mtakatifu Maria Theresa Chiramel Mankidiyan ni shuhuda wa majadiliano ya kidini yanayofumbatwa katika huduma ya upendo kwa watu wote bila ubaguzi hata kidogo.

Sr. Dulce Lopes Pontes wa Shirika la Watawa Wamisionari wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na Mama wa Mungu anakumbukwa sana kwa huduma ya upendo kwa maskini nchini Brazil. Alikuwa mtawa maarufu sana nchini Brazil katika karne ya XX, kiasi cha kuitwa kuwa ni “Mama Theresa wa Brazil”. Alianzisha huduma ya elimu kwa ajili ya wafanyakazi; akajisadaka kwa ajili ya maskini. Akabahatika kutembelewa na Mtakatifu Yohane Paulo II, mwezi Oktoba 1991 na kuonja mateso na mahangaiko ya maskini nchini Brazil. Upendo wa Sr. Sr. Dulce Lopes Pontes uliboreshwa zaidi na mahusiano pamoja na mafungamano yake na Kristo Yesu kwa njia ya: Tafakari na Sakramenti za Kanisa, chemchemi ya amana na utajiri wake wa maisha ya kiroho. Katika Ekaristi Takatifu, alijifunza kuwa Ekaristi kwa kujimega bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani zake.

Margarita Bays, Bikira na mtawa wa Utawa wa tatu wa Mtakatifu Francisko wa Assisi alisimika chachu ya utakatifu kama mama wa nyumbani na fundi cherehani; akajimega kwa ajili ya huduma kwa maskini kijijini kwake, sala na tafakari ya Neno la Mungu, vikipewa kipaumbele cha kwanza katika maisha yake. Alipopata mwanya, alijitahidi kuwatembelea, kuwasalimia na kuwahudumia wagonjwa. Alipenda sana kutoa katekesi kwa watoto wadogo, kiasi kwamba, utakatifu wake ulimwilishwa katika maisha ya kawaida. Katika maisha yake, aliamua kubaki Bikira kwa kujiweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu, ili kuwahudumia maskini zaidi. Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa upendo. Waamini watambue kwamba, Heri za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu na ni utambulisho muhimu wa Wakristo unaopaswa kumwilishwa na wote, kila mmoja kadiri ya wito, utume na dhamana yake katika maisha.

Utakatifu

 

 

16 October 2019, 11:29